Ticker

6/recent/ticker-posts

Mikanganyiko Ya Sheria Ya Habari Na Kifungu Cha Katiba Vinavyokwamisha Uhuru Habari.

 


Na Thuwaiba Habibu, Zanzibar

Ikiwa uhuru wa habari Zanzibar umeainishwa katika katiba  ya mwaka(1984 ) kifungu cha  ( 18 )ya katiba ya Zanzibar inayosomeka kama ifuatavyo.

(18) (1) Bila ya kuathiri sheria nyengine  za nchi,kila  mtu anayo haki ya uhuru wa maoni (kujieleza).kutafuta kupokea na kusambaza habari na mawazo yake  kupitia  chombo chochote cha habari  bila kujali  mipaka ya nchi  na pia anayo haki na uhuru  wa kutoingiliwa mawasiliano yake.

Kifungu hiki cha Katiba kimempa uhuru Mwandishi wa habari  kutafuta , kupokea na kusambaza taarifa .

Lakini kupitia Sheria mbili kuu zinazohusu masuala ya habari; ambazo ni Sheria ya Usajili wa Wakala wa Habari, Magazeti na Vitabu, Na. 5 ya mwaka 1988 kama ilivyorekebishwa na Sheria Na. 8 ya mwaka 1997; na pia Sheria ya Tume ya Utangazaji ya mwaka 1997 pamoja na Marekebisho yake ya mwaka 2010.ambazo zina vifungu  vinavyokinza uhuru  huo na kupelekea waandishi kupata changamoto kadhaa ambazo zinaathiri uhuru wa habari. kikiwemo kifungu cha 26 cha sheria ya Usajili wa Wakala wa Habari  za Magazeti na vitabu ,Na 5 ya mwaka 1997 kinavyosomeka .

"Mali  za vyombo  vya habari zinaweza  kutaifishwa endapo vyombo hivyo vitakiuka masharti ya sheria hii"

Kifungu hiki hakikutaja masharti ya aina gani hivyo kinaweza kutumika wakati chombo kikitoa taarifa ambayo mamlaka hawakuipenda basi wanaweza kukitaifisha.

Nazi haishindani na jiwe  ni msemo wa Kiswahili ambao hutoa tafsiri ya mtoto kutoweza kushindana na mzazi wake  lakini msemo huu umesadifu kwa Zanzibar kwasababu badala ya  katiba kuwa juu ya sheria, mtoto sheria yuko juu ya mama yake katiba,kwasababu  katiba imetoa ruhusa hiyo pale iliposema ; "bila ya kuathiri sheria nyengine  za nchi".

Mwandishi wa habari  Jesse Mikofu anasema Katiba imetoa  maelekezo  na msimamo kama tunavyojuwa katiba ni sheria mama  lakini kila  tulichopewa na Katiba kimenyang'anywa .

"Hii ni sawa  sawa na kupewa  chakula kwa mkono wa kulia  na kunyang'anywa mkono kwa mkono wa kushoto;Mfano ni  kifungu cha 30 cha  sheria ya Usajili wa Wakala wa Habari za Magazeti  na Vitabu, Na 5 ya mwaka  1997 ambayo Waziri amepewa Mamlaka ya kufungia gazeti kwa manufaa ya umma au kwa maslahi  ya Amani na utulivu.

 Hii inatokea kwasababu sheria haikufafanua maslahi ya umma  na Waziri anapimaje.

Mwandishi wa habari kutoka Tiffu Tv Siti Ali anasema sheria  ya habari ndiyo zinakwamisha uhuru wa habari kwasababu zipo kinyume  na katiba,na kupelekea waandishi kukosa pakuegemea na kupata changamoto  nyingi.

"Katiba inatupa uhuru wa kupokea na kukusanya taarifa ila sheria zetu hari zina vifungu ambazo vinakwaza uhuru wa kufanya hivyo." alieleza.

  Mwana habari Mkongwe na Zanzbar ambaye amekuwa mstari wa mbele kuonyesha udhaifu uliopo katika sheria za hivi sasa, Shifaa Said Hassan,   ambaye ni afisa Mwandamizi wa Baraza  la Habari Tanzania (MTC) katika ofisi za Zanzibar

 anasema wadau wa habari wamekuwa wakifanya uchechemuzi  kuwaeleza wenye mamlaka umuhimu wa kuwa na sheria mpya ya habari.

Wajumbe wa Kamati ya Wataalam wa Habari Zanzibar (ZAMECO) wameonana na Tume ya Marekebisho ya Sheria, na Wizara ya Habari kupeleka mapendekezo ya Wanahabari na Wadau wa Habari kuhusu mabadiliko ya Sheria za Habari Zanzibar lakini jitihada hizo zimegonga mwamba.

Tanzania imeiridhia mikataba mingi ya kikanda na kimataifa inayosisitiza umuhimu wa uhuru wa habari na uhuru wa kujieleza. Mikataba hii ni pamioja na ule wa kimataifa wa haki za binadamu wa 1948 ambao umesisitiza uwapo wa uhuru wa kujieleza kwa mataifa yote  lakini hadi wakati huu zanzibar imekosa uhuru huo kwa sababu ya baadhi ya sheria zilizopo.

Mkufunzi wa Chuo Kikuu Zanzibar (SUZA) na Mtetezi wa Masuala ya Habari Said Suleiman anasema kuwapo kwa sheria zenye mapungufu mengi kwa sekta ya habari kunakwaza uhuru wa kukusanya taarifa, kusambaza na hata uhuru wa kujieleza na kutoa maoni na hivyo kukwaza maendeleo ya nchi kwa ujumla.

"Tumeona kuwa sheria za habari zina mapungufu mengi ambayo yanayokwaza uhuru wa habari," anasema Said.

Mwanasheria na Mtetezi wa Masuala ya habari Juma Khamis Juma anasema ni kweli kifungu cha 18 cha Katiba kinatoa uhuru wa habari, lakini kama utakisoma vizuri utagundua kwamba kifungu hiki kinatoa uhuru kwa upande mmoja na kuzuia uhuru huo kwa upande mwingine.

"Ndio maana unakuta vifungu vilivyomo katika sheria za habari vina nguvu zaidi kuliko kifungu cha hiki cha Katiba,"

Changamoto hii inasababisha malalamiko kwa waandishi wa habari na vyombo vya habari. Wataalamu wa masuala ya sheria na habari, wamekuwa wakikizungumzia kwa muda mrefu kifungu hiki cha 18  cha katiba ambacho kinatofautiana na kifungu kama hicho kilichopo katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.

Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Tanzania Zanzibar Dkt Mzuri Issa anasema Katiba zote mbili ya Tanzania na ya Zanzibar zimetoa haki na  uhuru wa kujieleza lakini kupitia Sheria za Habari tulizo nazo, suala hilo limedhibitiwa.

"Ipo haja kwa waandishi  kupata haki yao ya uhuru wa kutafuta, kutoa maoni na kusambaza habari kwa kuwa vyombo vya habari ni daraja linalounganisha serikali na wananchi na vyombo vya habari ndiyo mhimili mkuu wa demokrasia na maendeleo katika nchi.

Post a Comment

0 Comments