Na Thuwaiba Habibu, Zanzibar
Ni zaidi ya
miongo miwili sasa wanahabari wamekuwa wakililia sheria ambazo ndani yake vimo vifungu
vinavyokandamiza uhuru wa kupata na kutoa habari zirekebishwe.
Wakati jamii ikishuhudia sheria nyingi za nchi zikibadilishwa mara kwa
mara, nyingine muda mchache tu baada ya kupitishwa na Baraza la Wawakilishi,
lakini hizi zinazogusa habari zimekuwa na safari ya zaidi ya miaka 20 na mwanga
wa kupatikana ufumbuzi haujachomoza.
Kwa miaka hiyo
yote waandishi wa habari wa Visiwani Zanzibar wamekuwa wakililia marekebisho ya
sheria za habari ili angalau wapate nafasi ya kufanya kazi kwa usalama kama
wenzao wa sekta nyingine.
Kilio cha waandishi wa habari wa Zanzibar kutaka
sheria za habari zifanyiwe marekebisho kinatokana na misukosuko wanayokumbana
nayo kila siku wakati wakiwa kazini.
Ikiwa ni pamoja na kuporwa vifaa vya kazi kama kamera,
simu, chombo cha kunasia sauti, vitabu vyao wanavyoandikia habari, kalamu na
hata fedha na wakati mwingine kubugudhiwa
kwa kupigwa au kufunguliwa mashitaka.
Mwandishi wa habari na Mjumbe wa (ZAMECO) Jabir
Idirisa anasema yeye ni miongoni
mwa waandishi waliokumbana na mashtaka kwa kufungulia kesi ambayo aliishi nayo
kwa muda wa miaka 6 kuanzia Januari 2016 hadi Septemba 2021 akituhumiwa
kufanya uchochezi kwa kutimiza wajibu wake wa kutoa taarifa ambayo ni haki ya
wananchi.
"Lazima kuwepo kwa sheria rafiki ambayo inaondoa
hali ya kudhibiti sana vyombo vya habari
na itakuwa imewapa uhuru waandishi wa kufanya kazi zao."
Anasema waandishi wanapitia shida kubwa japo kuwa wao
ndio wachagizaji wa maendeleo nchini.
Mwandishi wa habari Amrat Kombo anasema kuwapo kwa
sheria isiyo rafiki yenye vifungu vinavyokwaza uhuru wa habari kunawatia hofu waandishi juu ya usalama wa
maisha yao.
Ameelezea sheria mbili kuu zinazohusu masuala ya
habari; ambazo ni Sheria ya Usajili wa Wakala wa Habari, Magazeti na Vitabu,
Na. 5 ya mwaka 1988 kama ilivyorekebishwa na Sheria Na. 8 ya mwaka 1997; na pia
Sheria ya Tume ya Utangazaji ya mwaka 1997 pamoja na marekebisho yake ya mwaka
2010; akisema kuwa hizo bado ni dhaifu katika kulinda uhuru wa habari visiwani
hapa.
Kutokana na sheria hizo, waandishi wamekuwa wakipitia changamoto kadhaa kwani
kila kitu kuhusu uhuru wa habari kimedhibitiwa.
Haya yanafanyika wakati Tanzania ikiwa imeridhia
mikataba mingi ya kikanda na kimataifa inayosisitiza umuhimu wa uhuru wa habari
na wa kujieleza.
Mikataba hii ni pamioja na ule wa Kimataifa wa Haki za
Binadamu (UDHR) wa 1948 ambao umebainisha umuhimu wa kuwapo kwa uhuru wa
kujieleza kwa kila binadamu.
Vile vile mkataba
haki za kiraia na kisiasa wa 1966
(ICCPR) ambao unaeleza kuwa kama italazimika kuwapo vikwazo ni mambo mawili tu;
nayo ni kwa ajili ya kuheshimu faragha ya mtu na usalama wake.
Mikataba yote imeeleza wazi wazi kuwa kila mtu ana
haki ya kujieleza, kupokea maoni na kusambaza maoni yake bila ya vikwazo.
Afisa Programu
wa Tamwa – Znz, Zaina Mzee
aliwasihi wanahabari kutokata tamaa na kuendelea kudai haki yao ya kuwa na
uhuru wa kukusanya na kusambaza habari kwa usalama.
"Endeleeni kufanya uchechemuzi ili tuweze kupata
sheria mpya na rafiki ya habari ambayo itatufanya tuweze kufanya kazi zetu
vizuri."
Mwana habari Mkongwe, Hawra Shamte alisema lazima kuwe
na msisitizo wa upatikanaji wa sheria mpya za habari ili uhuru wa habari na haki ya kujieleza
ipatikane na kuchangia maendeleo.
Pia amesema upo
umuhimu wa kuwepo mashirikiano na
watunzi wa sera na serikali kufufua sekta hii ili kuwapa nafasi wandishi
kuandika vizuri habari na kuelimisha umma juu ya masuala mbali mbali .
Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Tanzania,
Zanzibar (TAMWA ZNZ), Dkt. Mzuri Issa alieleza mchakato wa mabadiliko ya sheria
za habari umekuwapo kwa miaka mingi lakini bado sheria hizo ambazo nyingi ni za
muda mrefu zimekwama kurekebishwa na kukosesha uhuru kwa vyombo vya habari,
waandishi na hata wanajamii, kwani uhuru wa kujieleza, uhuru wa maoni na uhuru
wa kusambaza taarifa ni wa kila mmoja wetu.
“Sisi wengine tangu tuko waandishi chipukizi
tunazungumzia kupata hizi sheria mpya za habari, tangu 2008 kwa kweli ni muda
mrefu, tunahitaji kusimamia jambo hili kwa umoja wetu na hatimaye tupate sheria
mpya.
0 Comments