Ticker

6/recent/ticker-posts

Ujasiriamali Usiwe Sababu Ya Uharibifu Wa Mazingira



Katika ulimwengu wa leo, ambapo ujasiriamali unachukuliwa kama njia kuu ya kujikwamua kiuchumi, wanawake wa Zanzibar wameonesha kuwa wanaweza kuwa nguvu kubwa ya maendeleo. 

Lakini pamoja na jitihada zao za kuimarisha maisha yao kupitia biashara, wao pia wana jukumu kubwa katika uhifadhi wa mazingira, hasa kwa kutunza miti ya mikoko na kulinda rasilimali za bahari.

Kupitia mradi wa ZanzAdapt, wanawake 20 kutoka maeneo ya Uzi, Bungi, Unguja Ukuu, na N’gambwa, ambao baadhi yao wanajihusisha na kilimo na uhifadhi wa mazingira, wamehitimu mafunzo ya ujasiriamali. 

Mafunzo hayo yamewapa ujuzi wa kuzalisha bidhaa mbalimbali kwa kutumia mazao ya kilimo, huku yakizingatia matumizi endelevu ya rasilimali za asili.

Lakini je, elimu pekee inatosha? Je, wanapata msaada wa kutosha ili kuendeleza biashara zao bila kuathiri mazingira?

Wanawake wamekuwa mstari wa mbele katika uhifadhi wa mazingira, ikiwa ni pamoja na kulinda na kupanda mikoko, ambayo ni muhimu kwa kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi na kuzuia mmomonyoko wa ardhi pwani. 

Hata hivyo, hali duni ya kiuchumi inawalazimu baadhi yao kukata mikoko kwa matumizi kama vile kutengeneza vifaa vya kufungia zao la mwani, hali inayoweza kusababisha kina cha bahari kupanda sehemu ya nchi kavu.

Ili kuleta suluhisho endelevu, wanawake hawa wanapaswa kupewa njia mbadala za kujipatia kipato bila kuharibu mazingira.

Hili ndilo lengo kuu la mradi wa ZanzAdapt, unaowapa maarifa ya ujasiriamali yanayowawezesha kutumia maliasili kwa njia endelevu.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa Community Forests Pemba (CFP), Mbarouk Mussa Omar, mradi wa ZanzAdapt unalenga kuhakikisha wanawake wanapata maarifa na msaada wa kiufundi ili kujitegemea kiuchumi.

"Tunafurahia kuwa sehemu ya mabadiliko haya. Tunaamini kuwa kuwawezesha wanawake ni hatua muhimu kwa maendeleo endelevu ya Zanzibar na kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi," alisema Omar wakati wa hafla ya kuhitimisha mafunzo.

Mafunzo haya ya siku saba, yaliyofanyika katika Chuo cha Sayansi na Teknolojia cha Karume (KIST), yaliwapatia wanawake ujuzi wa kuzalisha bidhaa mbalimbali kama vile jam, juisi, chai ya viungo (masala tea), na achari, kwa kutumia mazao ya kilimo badala ya kutegemea biashara zinazoathiri mazingira.

Kwa mfano, Zainab Waziri, mmoja wa wahitimu, alielezea jinsi mafunzo haya yamebadili mtazamo wake:

“Tumefunzwa kutengeneza bidhaa nyingi za kilimo badala ya kutegemea njia zinazoathiri mazingira. Ujuzi huu utatusaidia kuboresha maisha yetu na ya familia zetu.”

Kwa upande wake, Hidaya Ameir, alisema mafunzo haya yamempa ujasiri wa kuzalisha na kutafuta masoko ya bidhaa zake bila kuathiri mazingira:

“Sasa ninaweza kutumia mazao niliyonayo kwa njia bora zaidi. Mafunzo haya yameniongezea mbinu mpya za biashara na uhifadhi wa mazingira.”

Changamoto Zinazowakabili Wanawake Wajasiriamali wa Mazingira

Pamoja na mafanikio haya, bado kuna vikwazo vinavyowazuia wanawake hawa kufanikisha ndoto zao bila kuathiri mazingira.

Kwa mujibu wa Zulpher Bashir, Afisa wa Biashara ya Kijamii na Usawa wa Kijinsia wa CFP, changamoto kuu ni:

Ukosefu wa mitaji na mikopo – Wanawake hawa wanahitaji fedha za kununua vifaa vya uzalishaji ambavyo havihusishi ukataji wa miti au uharibifu wa mazingira.

Upatikanaji wa masoko – Bila soko la uhakika kwa bidhaa endelevu, wanaweza kurudi katika njia za zamani zisizo rafiki kwa mazingira.

Ukosefu wa teknolojia za kisasa – Vifaa bora vinaweza kusaidia kuzalisha bidhaa endelevu kwa ubora wa juu.

Sabra Khamis, mmoja wa wahitimu, alitoa wito kwa wadau wa maendeleo na serikali:

“Tunashukuru kwa mafunzo haya, lakini tunahitaji msaada zaidi. Tunahitaji mikopo ya kununua vifaa vya kisasa na kutafuta masoko ya bidhaa zetu ili tusilazimike kutegemea shughuli zinazoharibu mazingira.”

Mradi wa ZanzAdapt umeonyesha kuwa wanawake wa Zanzibar wanaweza kuwa nguzo kuu katika ujasiriamali endelevu unaozingatia uhifadhi wa mazingira. 

Kupitia mafunzo haya, sasa wanaweza kutumia rasilimali zilizopo kwa njia bora zaidi bila kuathiri mazingira.

Post a Comment

0 Comments