Ticker

6/recent/ticker-posts

Wananchi Wahimizwa Kujiandikisha Kwenye Daftari La Mpiga Kura


Wananchi wa makundi mbalimbali wametakiwa kutumia haki yao ya msingi kwa kujiandikisha katika daftari la kudumu la mpiga kura katika awamu ya mwisho ya usajili. 

Wito huo umetolewa na kikundi cha akinamama wa mabadiliko, ambao wamekuwa mstari wa mbele katika kutoa elimu juu ya umuhimu wa ushiriki wa wananchi kwenye mchakato wa uchaguzi.

Naima Salum Hamad, mmoja wa akinamama wa mabadiliko, amesema kuwa lengo lao ni kuhakikisha kila mwenye sifa anajitokeza kujiandikisha ili aweze kushiriki kikamilifu katika uchaguzi. 

"Tunataka wananchi waelewe kuwa haki ya kupiga kura inaanza na kujiandikisha. Bila hilo, hakuna nafasi ya kuchagua viongozi wanaowataka," alisema Naima.

Halima Abdulla Mohammed, ambaye pia ni sehemu ya kikundi hicho, amesisitiza kuwa juhudi zao ni sehemu ya kuunga mkono kampeni za Tume ya Uchaguzi katika kutoa elimu ya masuala ya uchaguzi kwa makundi yote ya jamii.

"Tunataka kuona vijana na wanawake wakitumia haki yao ya kidemokrasia. Mara nyingi, uelewa mdogo umekuwa kikwazo, lakini elimu tunayoitoa itasaidia kuongeza mwamko," alisema Halima.

Wananchi waliopatiwa elimu hiyo wameeleza kuwa sasa wana uelewa mpana wa umuhimu wa kujiandikisha. Najma Khamis Said, mkazi wa Daraja Bovu, Zanzibar, alisema kuwa elimu hiyo imempa msukumo wa kwenda kujiandikisha. 

"Awali, sikuona umuhimu wa kushiriki kwenye masuala ya uchaguzi, lakini sasa nimeelewa kuwa sauti yangu ni muhimu," alisema Najma.

Kwa upande wake, Ahmed Ali Mohammed, mkazi wa Miembeni, Zanzibar, amewataka vijana kuhakikisha hawatumiki kuchafua amani kabla, wakati na baada ya uchaguzi. 

"Kura ni njia bora ya kuleta mabadiliko tunayoyataka. Vijana tunapaswa kuwa mstari wa mbele katika kulinda amani," alisema Ahmed.

Mpango huu wa utoaji elimu umefanyika katika Wilaya za Kati, Kaskazini A na B, Magharibi A na B, pamoja na Wilaya ya Mjini, huku akinamama wa mabadiliko wakiahidi kuendelea na kampeni hii ili kuwafikia wananchi wengi zaidi.

Post a Comment

0 Comments