Ticker

6/recent/ticker-posts

Gharama Za Fomu Ya Ugombea, Zimezima Ndoto Za Wanawake Kugombea Nafasi Za Uongozi.


NA AMRAT KOMBO,ZANZIBAR:

Kama ilivyo mataifa mengine ya Kidemokrasia ulimwenguni Tanzania-ZANZIBAR nayo hufanya uchaguzi kila baada ya miaka mitano.

Zanzibar inatarajia kufanya uchaguzi mkuu hivi karibuni na wanawake wanatarajiwa kushiriki kwa wingi, ingawa wanasiasa wanawake bado wanakabiliwa na changamoto ya kiuchumi hivyo kushindwa kufikia usawa wa kijinsia na uwiano wa 50 kwa 50 kwenye nafasi za siasa na uongozi.

Hali hiyo huwafanya wanasiasa wanawake kuwa katika wakati mgumu kwani wanahitaji kukabiliana na changamoto hiyo ili kuimarisha ushiriki wao katika siasa hasa katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

Wanawake wanatamani kupunguziwa gharama za bei ya kuchukua fomu za kugombea nafasi za uongozi ili kufikia malengo ya usawa wa kijinsia katika uchaguzi wa mwaka 2025.

Licha ya kuwa wamekua wakijitahidi kujiimarisha katika siasa lakini bado wanakumbana na kikwazo cha ukosefu wa rasilimali fedha kuanzia hatua ya kuchua fomu za kugombea, kuendesha kampeni hivyo kupelekea upungufu wa nafasi mbali mbali za uongozi.

Kupitia chaguzi zilizopita Zanzibar, tunashuhudia wanaume ndio hujitokeza kwa wingi kuchukua fomu za kugombea nafasi za uongozi tofauti na wanawake, hali hiyo inatajwa ni kutokana na ukosefu wa rasilimali fedha.

Baadhi ya vyama vya siasa ikiwemo Chama Cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA, katika uchaguzi wa 2020 gharama za kuchukua fomu ya kuomba nafasi ya urais ni shilingi milioni moja 1,000,000, fomu ya uwakilishi na ubunge ni shilingi laki mbili na elfu hamsini 250,000 na udiwani ni shilingi 50,000.

TAKWIMU

Kwa mujibu wa Takwimu za sensa ya watu na makaazi ya mwaka 2022 Zanzibar, idadi ya watu imefikia 1,889,773 kati yao wanawake ni 974,281 sawa na asilimia 51.6.

Idadi ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi (BLW) hadi kufikia 2010 lina wajumbe 78 kati yao wanawake 29 na wanaume 48, hiyo inadhihirisha ukweli wa jambo hilo.

Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 Zanzibar wanawake wengi wameonesha ujasiri wa kushiriki ambapo wanawake 294,231 sawa na asilimia 51 walijiandikisha kama wapiga kura ikilinganishwa na wanaume 272,121 ambao ni sawa na asilimia 49.

Aidha takriban wanawake 250 waliteuliwa na vyama vyao vya siasa na kuwa wagombea wa kushindania nafasi mbali mbali ikiwemo uwakilishi, ubunge na udiwani licha ya kuwa wengine waliishia njiani kutokana na rasilimali fedha kuwa kikwazo kwao.

WANAWAKE WA VYAMA VYA SIASA WALIOKOSA FEDHA YA KUCHUKUA FOMU

Nadhira Ali Haji (50) mwanasiasa mwanamke kutoka chama cha wananchi CUF, katika uchaguzi mkuu mwaka 2020 aliandika historia ya kuwa mwanamke wa kwanza kutangaza nia ya kugombea nafasi ya urais wa zanzibar lakini dhamira yake hiyo ilizima kama mshumaa baada ya kukosa fedha za kuchukua fomu ya kugombea nafasi hiyo.

Lakini anadai kuwa nia yake imeficshwa na chama chake kushindwa kumsaidia fedha kwa ajili ya kuchukua fomu ya kugombea nafasi ya urais uchaguzi wa mwaka 2020.”Nia yangu ya kugombea nafasi hiyo imetokana na uwezo wangu wa kujiamini, na uwajibikaji kwa moyo thabiti kwa lengo la kufikia usawa na fursa sawa kwenye nafasi za uongozi na maamuzi.”Amesema Nadhira

“Sikushawishiwa na mtu bali niliona wakati umefika wa nguvu ya wanawake wa CUF ilishuhudiwa hapo, baada ya kumuona mwanamke mwenzao anafaa kuwa kiongozi katika nafasi ya urais”ameongezea Nadhira

Mchakato wa kumpata mgombea ndani ya chama hicho ukaanza ambapo wagombea wa nafasi urais kwa zanzibar ndani ya CUF ilifikia watano huku mwanamke akiwa peke yake ingawa hakufanikiwa hatua ya kuchukua fomu kwa kukosa fedha na hakuwa na msaada.“ndoto yangu ilizima kama mshumaa, sikuwa na mtu wa kunishika mkono, sio chama changu, serikali wala jamii inayonizunguka havikuniwezesha”Amesema Nadhira

Mwanamke mwengine ni Pavu Abdallah kutoka chama cha ACT wazalendo amesema hatua ya kupata fedha za kuchukulia fomu ya kugombea ni mtihani mkubwa kwa wanawake, hali hiyo kuwafanya wanawake wengi kukosa uwezo wa kushindana na wanaume ambao mara nyingi wana rasilimali zaidi.“Ukosefu wa rasilimali fedha unawafanya wanasiasa wanawake kuwa nyuma katika kampeni za kisiasa huku familia zao zinawasiwasi kuhusu ustawi wao”Amesema Pavu

Aliyomba serikali na viongozi wa vyama vya siasa kuzingatia masuala ya uchumi wakati wa kutunga sera na sheria zinazolenga kukuza uchumi ili kuboresha ushiriki wao katika siasa na kuchangia maendeleo endelevu Zanzibar.

WANANCHI

Sabrina Masoud na Ameir Ali wanasema, wanawake wanakosa kushiriki nafasi za uongozi kwasababu mbalimbali ikiwemo gharama ya fomu kwani hii ni kikwazo kikubwa kinachowakwamisha wanawake wengi kugombea nafasi za juu ikiwemo uraisi.“Gharama zinazowekwa ni kubwa ukilinganisha na kipato cha wanawake wengi hushindwa kujitokeza kugombea ingawa uthubutu na uwezo wa kuongoza wanao.”Amesema Sabrina

“ Baadhi ya wanawake ni waangalizi wa familia na kuhudumia familia ni vyema serikali kupunguza bei ya fomu za uchaguzi kwa wanawake.”Hawawezi kuacha watoto wakalala njaa au kukosa mahitaji ya lazima, pesa zao zinatumika zaidi kweye majukumu ya familia .”Amesema Ameir

VYAMA VYA SIASA

Fatma Fereji, Katibu wa Ngome ya Wanawake Taifa, ACT wazalendo na Mjumbe wa Kamati Kuu chama hicho, rasiliali fedha ni miongoni mwa changamoto kubwa, kwani wanawake wengi wameachwa nyuma na kushindwa kufikia ndoto zao.”Vyama vya siasa na serikali viwaangalie wagombea wanawake kwa jicho la huruma sana hasa wale ambao hawajawahi kuingia katika Bunge au Baraza la wawakilishi, lazima wanawake wahamasishwe kugombea nafasi za juu kwa kukupunguza gharama ya fomu.”Amesema Fatma

WANAHARAKATI

Mkurugenzi Jumuiya Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA) Jamila Mahmoud amevitaka vyama vya siasa kuunga mkono mwanamke kwenye kupunguza gharama ya fomu ili kuweza kujitokeza kwa wingi katika uchukuaji wa fomu wa nafasi za juu za uongozi . “ Nadhira ameonyesha mfano ya kuwa nguvu za wanawake zikiiungana kuna uwezakano mkubwa wa kuunga mkono harakati za wanawake wenye nia ya kuwa viongozi.

Mwanaharakti Saphia Ngalapi kutoka Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA ZNZ) anasisitiza umuhimu wa kutoa mafunzo kwa wanawake kuhusu masuala ya ujasiriamali na matumizi ya mitandao ya kijamii ili kujenga uwezo wa kifedha.

WIZARA YA MAENDELEO YA JAMII, USTAWI WA JINSIA WAZEE NA WATOTO

Naibu Waziri wa wizara hiyo, Anna Athanas Paul, amesema ipo haja ya kuwawezesha wanawake kibiashara zaidi katika miradi inayowalenga ili kusaidia kunyanyua uchumi wao kufikia azma ya kuwa viongozi “bila ya pesa huwezi kufikia malengo ya kuwa kiongozi ni vyema kuanzishwa miradi mbali mbali itakayowawezesha wanawake ili kukidhi mahitaji yao ikiwemo masuala ya siasa, vilevile gharama ya bei ya fomu ya wagombea kwa wanawake ipungunzwe hii itasaidia kuhamasika kwa wanawake wengi kugombea nafasi za juu ikiwemo uraisi” .Amesema Anna


Post a Comment

0 Comments