Na Nihifadhi Abdulla:
Kila mwaka, mijadala kuhusu nafasi ya wanawake katika uongozi imekuwa ikipamba moto nchini Tanzania, hususan Zanzibar. Wananchi kutoka maeneo mbalimbali wamesema wanawake wana jukumu muhimu si tu kushiriki katika uongozi, bali pia kuwahamasisha wenzao kushiriki na kuweka ushawishi wa mabadiliko chanya. Huku baadhi yao wakiona hatua kubwa zimepigwa, wengine wanaamini bado kuna changamoto za kiutamaduni na kijamii zinazokwamisha juhudi hizo.
Sophia Ngalapi ni Mkuu wa Kitengo cha Mawasialiano kutoka Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania -TAMWA-Z, amesema juhudi za wanawake kujitokeza kuwania nafasi za uongozi bado zinakabiliwa na changamoto kadhaa, lakini matumaini yapo.“Nafasi ya mwanamke katika jamii yetu ni kubwa, lakini imekuwa vigumu kwa wanawake wengi kujiamini na kuthubutu kuchukua nafasi za uongozi. Hii ni changamoto ya mfumo dume, lakini pia inatokana na ukosefu wa usaidizi wa kijamii na kifamilia,” Amesema Sophia Ngalapi.
Baadhi ya wananchi waliozungumza katika Makala hii waliunga mkono kauli ya Sophia, huku wakitoa maoni tofauti kuhusu jinsi ya kuboresha hali hiyo.Fatma Abdallah, mama wa watoto wawili kutoka Kijiji cha Unguja Ukuu, amesema wanawake wanapaswa kuwa mstari wa mbele kuhamasishana na sio kutumika kuwahamasisha wanawake wengine wawachague wanaume.“Mimi naamini mwanamke akisimama, wanawake wengine wataiga. Tuna mifano mingi ya wanawake waliofanikiwa, kama Rais Samia Suluhu Hassan. Lakini pia sisi wa vijijini tunahitaji msaada wa mafunzo na mikakati ya kushirikishwa zaidi kwenye siasa na maendeleo ya jamii,” Anamaliza Fatma.
Kwa upande wake Ashura Seif, mfanyabiashara wa ukili kutoka Saaten Zanzibar, anahisi wanawake bado wanakosa mshikamano wa kweli katika kusaidiana kwenye upande wa kisiasa. “Tatizo letu ni sisi wenyewe, hatusaidiani. Mwanamke anapojaribu kujitokeza, wenzake wanamkatisha tamaa au kumsema vibaya.” Amesema Ashura huku akishauri kuwa tunahitaji kubadilika na kuungana ili kufanikisha maendeleo,” Amesema Asha kwa msisitizo.
Hata hivyo, si wote wanaoona changamoto tu. Rehema Mwalimu, mkaazi wa Kilimani anaamini kuwa mabadiliko yanawezekana kama kila mwanamke atachukua jukumu la kumhamasisha mwenzake mwenzake kwenye kuwachagua.“Wakati wa uchaguzi uliopita, nilihamasisha wanawake wenzangu kumi kupiga kura kwa mwanamke aliyegombea nafasi ya udiwani. Tuliona mabadiliko na sasa tuna diwani mwanamke anayetutetea vizuri. Hili linatufundisha kuwa umoja wetu ni muhimu,” Amehitimisha Rehema.
Kwa upande wa wanaume, wengi wanakubaliana na umuhimu wa wanawake katika uongozi lakini wanasisitiza kuwa juhudi zaidi zinahitajika kubadilisha fikra za jamii.
Omar Juma ni Mwalimu wa Madrasa amesema kuwa uongozi wa mwanamke unakuwa na msimamo na wanaweza kuchaguliwa “Wanawake wengi wanajitahidi, lakini bado kuna ukosefu wa elimu kwa jamii nzima kuhusu umuhimu wa uongozi wa wanawake. Wanaume wanapaswa kuwa sehemu ya mabadiliko haya, siyo kuwazuia wanawake.” Mwalim Omar amesema
Juma Ali, fundi ujenzi kutoka Unguja Ukuu, anahisi kuwa wanawake wanapaswa kuwa tayari zaidi kukabiliana na changamoto za uongozi na wasiwe dhaifu kwenye kupambana.“Uongozi ni kazi ngumu. Mwanamke anayejitokeza lazima awe na ujasiri wa kuvumilia changamoto, hasa za watu kumdharau. Lakini naamini wanawake wana uwezo sawa na wanaume, tatizo ni mfumo dume ambao unawafanya waogope,” Amesema Juma.
Kauli mbalimbali za wananchi zinaonyesha kuwa juhudi za kuwahamasisha wanawake kujitokeza katika uongozi bado zinahitaji katika kijamii. Sophia Ngalapi anahitmisha kwa kusema mabadiliko hayawezi kufanikiwa bila ushirikiano wa wanawake, wanaume ,wadau na serikali.
“Tunapenda kuona zaidi wanawake wakijitokeza si tu kuwania nafasi za uongozi, bali pia kuwasaidia wanawake wenzao kujiamini. Tunahitaji kuendeleza juhudi za kutoa elimu, kuongeza hamasa, na kupambana na changamoto za kijamii zinazorudisha nyuma maendeleo ya wanawake” Amehitimisha Sophia.
Ni dhahiri kuwa safari ya wanawake kuleta ushawishi mkubwa katika uongozi ni ndefu, lakini inawezekana iwapo jamii nzima itashirikiana kwa dhati kuondoa vikwazo vilivyopo.
0 Comments