NA AMRAT KOMBO, ZANZIBAR
KATIKA jamii zetu zilizojaa mfume dume ilikuwa ni vigumu wanawake kujipenyeza moja kwa moja katika majukwa ya siasa hivyo kulianzishwa viti maalumu ili kutoa fursa kwa wanawake kushiriki siasa na kufikia uwiano wa asilimia 50 kwa 50 kwenye nafasi za maamuzi.
Nafasi za viti maalumu zimewekwa kwa lengo la kuwajenga wanawake kuwa na maarifa na kupata uzoefu ili iwe rahisi kwao kugombea kwenye majimbo ya uchaguzi.
Kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 wanawake wengi wanapaswa kujitokeza katika majimbo ya uchaguzi sio viti maalumu kwani idadi ya wawakilishi wa kuchaguliwa ni ndogo ikilinganishwa na wanaume.“Kwa mujibu wa takwimu za Baraza La Wawakilishi (BLW) idadi ya wajumbe ni 78 kati yao wanawake 29 na wanaumea 48, wawakilishi wa majimbo kupitia uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 ni nane, wanaume 42, huku wanawake wa viti maalumu ni 18”.
Kwa mwaka 2020 wanawake walihamasika na kufikia zaidi ya wagombea 300 waliojitoeza kwenye nafasi ya urais, ubunge, uwakilishi na udiwani kupitia vyama mbali mbali vya siasa vyenye ushindani.
Hali hiyo inadhihirisha haja ya wanawake kuongezeka katika majimbo ya uchaguzi 2025 kwani idadi ya wawakilishi wanawake wa kuchaguliwa ni ndogo ambayo hailingani na idadi ya wakaazi wa Zanzibar.
Takwimu za sensa ya watu na makaazi ya mwaka 2022 idadi ya wanawake Zanzibar imefikia 974,281 sawa na asilimia 51.6 ,umefika wakati kwa kundi hilo kuacha kujibweteka nafasi ya viti maalumu badala yake kujitosa katika majimbo ya uchaguzi.
WANAWAKE WANAOTAMANI KUJIFUNZA VITI MAALUMU NA KUONDOKA
Habiba Ali Mohammed,(54) kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) amesema nafasi za viti maalumu zinapatikana kwa shida wanawake wakifika hapo hawataki kujifunza na kuondoka hubaki katika maisha yao yote."Inashangaza Mwanamke mmoja anaing’ang’ania nafasi kwa miaka 20 hajui kama kuna kundi kubwa la wanawake wanasubiri nafasi hiyo ili wajifunze kama yeye" amesema Habiba
Habiba alitoa rai kuwa ifike wakati Chama Cha Mpinduzi na vyama vyengine kuweka sheria maalumu itakayo ainisha muda wa nafasi za viti maalumu ili kusaidia wanawake wengine kushika nafasi hizo kwa muda ili waliopata uzoefu wende majimboni.
Salama Salmini Shuwari. (sio jina halisi) mwanachama kutoka ACT Wazalendo anasema sio vizuri mwanamke kukaa zaidi ya awamu mbili katika viti maalumu na kusahau lengo la kuanzishwa nafasi hizo na kudai kuwa usawa wa kijinsia utachukua muda hadi kufikiwa ikiwa wanawake wataogopa kwenda majimboni.
USHUHUDA WA WAWAKILISHI WA MAJIMBONI
Asha Abdallah Mussa, Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda, anasema yeye hajapita kwenye viti maalumu ametoka kwenye udiwani wa wadi na kwenda moja kwa moja jimboni, haoni haja ya wanawake kuogopa nafasi za majimbo.“Wanawake wengi wanakimbilia nafasi za viti malumu jambo ambalo linawakosesha fursa ya kupata viti vingi katika bunge na baraza la wawakilishi na kudai kuwa miaka mitano pekee inatosha kupata uzoefu na hapo mwanamke akimbilie jimboni”.
Rukia Ramadhani Mapuri, Mwakilishi wa Jimbo la Amaani, anasema suala la uthubutu kwa wanawake hakuna ugumu kwa sababu wakijaribu wanaweza na wapo wawakilishi na wabunge wanawake ambao wanahudumia katika majimbo ya uchaguzi.“idadi ya wanawake majimboni imefikia 8 tunapaswa kuzikimbilia nafasi hizi kupambana ili kufikia usawa wa 50/50, siri kubwa ya mafanikio kuepuka majungu na fitina”
WANAWAKE WANAOTUMIKIA NAFASI ZA VITI MAALUM
Mwakilishi wa viti maalumu Salha Mwinjuma, amesema kama fursa inaruhusu kuendelea na viti maalumu basi ataomba viti maalumu na sio uwoga wa kwenda jimboni bali ni namna ya kujipanga, pia hawezi kwenda jimbo lolote analotaka lazima agombee sehemu aliyokuwa na vinasaba nayo ikiwemo makaazi, au alipozaliwa ili kuwatumikia watu anaowafahamu.
Mbunge Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Mkoa wa Magharibi kichama Tauhida Galosi Nyimbo,amesema kwake suala la kuhofia kwenda jimboni halipo, ni namna ya Chama chake kitakavyoweza kujipanga kwani hawezi kuchukua uwamuzi peke yake.
VIONGOZI WA VYAMA VYA SIASA
Naibu Katibu Mkuu Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Zanzibar Tunu Juma Kondo amesema umefika wakati wanawake kujitokeza katika majimbo na kuondoa hofu kwani Jumuiya hiyo kwa kushirikiana na Chama Cha Mapinduzi CCM itahakikisha inawasimamia wanawake kushinda kwenye majimbo ili kufikia usawa wa asilimia 50/50.“Hakuna ubaya mwanamke kwenda jimboni moja kwa moja ni haki ya kila mmoja lakini anapopata fursa ya viti maalumu atumie muda mchache kujifunza na kuelekea jimboni”
Amesema changamoto ya wanawake kungangania viti maalumu inatajwa na ipo kwani wapo wasiotaka kuondoka hata baada ya kukaa vipindi viwili au zaidi.“Endapo utaratibu wa viti maalumu utafuatwa kama ulivyokusudiwa wengi wangelikua wabunge na wawakilishi majimboni na kuongeza idadi ya wanawake katika vyombo vya maamuzi”.
Miongoni mwa mikakati ya CCM ni kuhamasisha waliokaa zaidi ya awamu mbili kuelekea jimboni kwani wamepata uzoefu na wana nguvu ya kutosha kupambana majimboni
Halima Ibrahim kutoka ngome ya wanawake ACT wazalendo amesema katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika hivi karibuni wameandaa programu ya kuhamasisha wanawake kuingia majimboni na sio viti maalumu.
WANAHARAKATI
Mkurugenzi wa Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA-ZNZ) Dk. Mzuri Issa, amesema nafasi za viti maalumu wanazopata wanawake ni kwaajili ya kujifunzia kuelekea majimboni sio kubaki kwa muda mrefu kama baadhi wanavyofanya."Dhamira ya kuanzishwa nafasi hizo ni kuwapa fursa wanawake wengi kujifunza kwa ajili ya kuelekea majimboni sio kujibweteka hapo kwa muda wote" amesema Dkt mzuri
" Kuna mtu unakuta yupo amegombea miaka mitano hii na mitano mengine na bado yupo hapo hapo wakati inatakiwa mtu agombee miaka mitano tu ajifunze, kisha atoke aende jimboni." Ameongezea Dkt mzuri
Hata hivyo alizitaka taasisi zote zinazohusika kusimamia sheria kutilia nguvu suala hilo kwa ajili ya kuwasaidia wanawake kujifunza vizuri kwa lengo la kushindana kwenye majimbo ili kutoa fursa kwa wanawake kuwa viongozi kuanzia viti maalumu na majimboni ili kufikia dhana ya usawa wa kijinsia katika uongozi.
HISTORIA YA VITI MAALUMU
Viti maalumu vya wanawake ni nafasi zinazotolewa kwa utaratibu unaopatikana katika nchi mbali mbali unaolenga kuongeza idadi ya wanawake katika bunge na mabaraza katika siasa za nchi mbali mbali ingawa baadhi ya wanawake wanatumia muda mrefu kwenye nafasi hizo.
Kuna nchi nyingi duniani zilichukua hatua za kuongeza nafasi za wanawake serikalini kulingana na mkataba kuhusu ufutaji wa ubaguzi wote wa wanawake (Convention on the Elimination of All Forms of Discrimination Against Women) ulioanzishwa mwaka 1981 na kuimarishwa na azimio la mkutano mkuu wa Umoja wa Mataifa mwaka 2011 ambao uliosainiwa na mataifa 189.
Nchi za Afrika zinazotumia utaratibu wa viti maalumu vya wanawake katika bunge ni Algeria, Burundi, Djibouti, Eritrea, Eswatini, Guinea, Kenya, Lesotho, Libya, Muritania, Morocco, Niger, Rwanda, Sierra Leone, Somalia, Sudan Kusini, Tanzania, Uganda na Zimbambwe.
Mfano tamko la nchi za Jumuiya ya Maendeleo Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) linaunga mkono masuala hayo.
0 Comments