NA
AMRAT KOMBO, ZANZIBAR:
Nchi nyingi zimeridhia mikataba na matamko ya usawa
wa kijinsia, uwezeshaji wanawake kwenye uongozi na nafasi za maamuzi kama
ilivyoainishwa katika Tamko la Haki za Binadamu la mwaka 1948.
Zanzibar nayo ikiwa sehemu ya Jamuhuri ya Muungano
wa Tanzania ambayo imesaini mikataba ya kikanda na kimataifa, lakini safari ya
utekelezaji wake ni ndefu na hii inaonekana katika shehia, wadi, majimbo, taifa
kutokana na kutokuwepo fursa sawa katika kugombea uongozi.
Mikataba iliyosainiwa na hali halisi ya uongozi kwa
wanawake Zanzibar ni wazi kuwa mikataba ya kikanda na kimataifa haijazingatiwa
vyema hapa nchini katika kutoa fursa sawa ya uongozi kati ya wanaume na
wanawake.
TAKWIMU ZA UCHAGUZI 2020.
Katika uchaguzi mkuu wa 2020 watu walioteuliwa na
vyama kugombea nafasi ya ubunge kwa upande wa Zanzibar wanaume 257 na
walioshinda 46, wanawake walikua 81 na walioshinda wanne.Walioteuliwa kugombea
nafasi ya wawakilishi Zanzibar wanaume
190 na walioshinda 42 ambapo wanawake walikuwa 61 na walioshinda ni 8 na
wanaume walioteuliwa na vyama kugombea udiwani 276 na walioshinda 85 ambapo
wanawake walikua 74 na walioshinda ni 25.
MIKATABA NA ITIFAKI INASEMAJE?
Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika
(SADC) ambayo mkataba wake ulitiwa saini mwaka 2008 inaeleza kutaka kuondoa
utafauti na kuwatenga wanawake katika nyanja mbalimbali za maendeleo na
kusaidia kuwepo usawa wa kijinsia katika nchi wanachama na kufikia asilimia
50/50 kwenye maamuzi, serikali na taasisi binafsi.
Mkataba mwengine wa kimataifa wa (CEDAW) wa 1979
ambao unapinga aina zote za udhalilishaji na kusisitiza ushiriki wa wanawake
katika siasa na maisha ya kijamii.
Kwa mfano itifaki ya Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za
Kusini mwa Afrika (SADC) mkataba wake wa kikanda uliotiwa saini mwaka 2008 na
nchi wanachama wake ikiwemo Tanzania, wenye vifungu 43 unaelekeza nchi hizo
kuzingatia suala la haki na usawa kati ya wanaume na wanawake katika suala la
uongozi.
Kifungu cha nambari 12 kinasisitiza ushiriki sawa
wanawake na wanaume kufikia asilimia 50/50 kwenye Nyanja za maamuzi, serikalini
na taasisi binafsi.Katika Itifaki ya Maputo ambayo makubaliano yake yalifanyika
tarehe 11, Julai 2003 nchini Msumbiji, kipengele nambari 9 kinahimiza ushiriki
sawa wa wanawake na wanaume katika siasa na vyombo vya kutoa maamuzi. Aidha
jukwaa la Mpango wa Utekelezaji wa Beijing mwaka 1995 kifungu nambari 7
kinataka ushiriki katika vyombo vya maamuzi kwa kuzingatia uwiano wa kijinsia
kwenye ngazi zote za uongozi.
KATIBA YA ZANZIBAR
Katiba ya Zanzibar ya 1984, imeweka wazi kuwa kila
Mzanzibari anayo haki na uhuru wa kushiriki kwa ukamilifu katika kufikia uamuzi
juu ya mambo yanayohusu taifa lake na
katika marekebisho ya 2010 imeeleza kutakuwa na wajumbe wa Baraza la
Wawakilishi (BLW) asilimia 40 wa wajumbe kwa kila jinsia.
DIRA NA SERA ZA ZANZIBAR
Dira ya Zanzibar ya 2050 imeelezea jinsi gani
masuala ya usawa wa jinsia juu ya kuondoa unyanyasaji na kuimarisha mifumo ya
uwezeshaji wanawake, ikiwa pamoja na kuinua na kutoa nafasi za uongozi kwa
wanawake.
Vile vile imelenga kuongeza fursa na kuwawezesha
katika vyombo vya kutoa maamuzi na kwenye shughuli za uchumi, kijamii, siasa,
ngazi za utawala na huduma za sheria.
Sera ya jinsia inaeleza ushiriki wa wanawake katika
vyombo vya utoaji maamuzi katika ngazi zote ni mdogo hivyo serikali kwa
kushirikiana na wadau wengine imeahidi kufanya juhudi kuona makundi yote na
yaliyopembezoni yanapata fursa hiyo.
MTAZAMO WA VYAMA VYA SIASA
Asha Abdallah mkaazi wa mahonda ambae pia mwakilishi
wa jimbo hilo.na kujuzwa kuwa bado
utekelezaji wa mikataba kuwainua wanawake imeachwa nyuma ,kutokana na ushiriki mdogo wa
wanawake katika kushika nafasi mbalimbali za uongozi ,kwa mfano wawakilishi
wanawake mwaka 2015 ilikuwa 7 na mwaka 2020 wako 8 hii inaonesha dhahiri kuwa
mikataba imeachwa nyuma.
Naibu Mkurugenzi kutoka ADC, Mtumwa Faiz Sadik,
amesema ili kuzipatia ufumbuzi changamoto wanazopitia wanawake ni lazima kuwepo
mipango mizuri ya kutekeleza mikataba na maazimio ya kimataifa.”Mikataba
haitekelezwi ipasavyo na kuchangia kutofikiwa usawa kati ya wanawake na wanaume
katika kuwania uongozi licha ya wanawake kujipanga na kuhamasika kugombea
katika uchaguzi mkuu wa hivi karibuni.
Kiongozi wa ACT Wazalendo, Juma Duni Haji, amesema
chama hicho kinafuata sheria na mikataba iliyoridhiwa na kusistiza hakina mfumo
dume na kutoa mfano wa sekretieti ambayo ni chombo kikubwa kuwekewa uwiano wa
wajumbe, wanaume 10 na wanawake 10.
KINACHOKWAMISHA
Naibu Katibu Mkuu Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT)
upande wa Zanzibar, Tunu Juma Kondo, amesema ipo haja ya kuzingatia mikataba ya
usawa kwenye uongozi kati ya wanawake na wanaume na kusisitiza kwamba hivi sasa
wanawake wameelimika, wanafahamu mambo ya siasa, uchumi na maendeleo, ni vyema
mikataba itekelezwe.”Mfano mzuri ni wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mama Samia Suluhu Hassan, ambaye anaifanya kazi yake kwa bidii kuimudu nyadhifa
hioo kuu nchini kwa uadilifu mkubwa, kutokana na kutouwepo sheria inayotaka
kuwepo fursa zenye hadhi sawa kwa wanawake na wanaume kunaifanya nchi kutotekeleza
kwa ufanisi baadhi ya mikataba iliyoridhia inayohusu usawa katika
uongozi.”Amesema Tunu
NINI KIFANYIKE.
Mwanaharakati maarufu wa haki za wanawake Daktari
Ananilea Nkya ameishauri serikali na wadau wa masuala ya sheria kuona umuhimu
wa utekelezaji mikataba iliyosainiwa.” Naomba kuwashauri serikali pamoja na
wadau mbalimbali wa masuala ya sheria kuzingatia sheria zilizowekwa kwenye
mikataba na wasiipe kisogo kwani utekelezaji wa mikataba hiyo itakuwa njia ya
kuwainua wanawake katika siasa.vilevile nawashauri wanawake wenzangu kugombea
nafasi mbalimbali katika uchaguzi wa mwaka 2025 ili kufikia azma ya kuanzishwa
mikataba ya kitaifa na kimataifa.”Amesema Ananilea
Kwa upande wake mwanaharakati wa Chama Cha Habari
Wanawake Tanzania – Tamwa Zanzibar mkurugenzi wa chama hicho Dkt Mzuri Issa
amesema umefika wakati kuondoa vikwazo vinavyokwamisha mikataba hiyo.”Ni vyema
vyama vya siasa kuwekwa sheria rafiki zitakazotoa muongozo wa matamko hayo ili
kuzingatiwa mikataba hayo ipasavyo.
Karne hii ya sasa inawapasa viongozi wa vyama vya siasa kubadilisha
katiba zao kuendana na mikataba iliyoridhiwa ili kufikia uwiano wa 50/50 kwenye
siasa na serikali kwa ujumla".Ameongezea Dkt Mzuri
0 Comments