Na Amrat Kombo, Zanzibar
Mwanamke ni nguzo muhimu katika ujenzi wa familia. Ana jukumu kubwa katika kulea watoto, kuwafundisha maadili mema, na kuwa mfano bora kwa vizazi vijavyo. Kwa kuongeza, wanawake wamekuwa mstari wa mbele katika masuala ya elimu, biashara, siasa, na hata katika sekta ya afya na teknolojia.
Ingawa mara nyingi hawathaminiwi vya kutosha, wanawake wameendelea kupigania nafasi zao, huku wakionyesha nguvu, ujasiri, na ustahamilivu katika kutimiza majukumu yao.
Mwandishi wa Makala hii amekutana na mwakilishi wa jimbo la konde wa chama cha Mapinduzi CCM Zawadi Amour ambae ni mtoto wa kwanza katika familia ya watoto tisa,aliwahi kuwa mwalimu katika skuli ya Pangale na Konde “A” kuanzia mwaka 2000 hadi 2020. Nakufanikiwa kuibua taharuki ya kudhalilishwa wanafunzi tisa wa skuli ya msingi ya konde.
“ Wakati nasomesha skuli ya msingi ya konde nilifanikiwa kugundua vitendo vya ukatili na udhalilishaji ambavyo vinafanyika katika skuli hiyo,nikabahatika kuwapata wanafunzi tisa waliofanyiwa vitendo hivyo, sikuridhika na idadi hiyo niliendelea kutoa elimu ya kujilinda na vitendo vya udhalilishaji nikabahatika kupata tena wanafunzi 35 . Amesema Zawadi
“ Nilifatilia kesi hii nikagundua baadhi ya walimu wa skuli na madrasa ndio wanaohusika na vitendo hivyo, licha ya kugundua uovu huo kinachosikitisha jamii yangu haikuniunga mkono na kujigawa makundi, wapo ambao waliniona nimefanya jambo jema na wapo ambao walinitenga na kunisema vibaya, na yote haya hawakuwa na elimu ya kuripoti vitendo hivi na kuniona kama nawadhalilisha watoto hao.” Ameongezea Zawadi
Katika mwaka 2019 alianza kujishirikisha katika harakati za kisiasa kwa ajili ya kutetea taharuki iliyotawala katika kijiji chao, hakukata tamaaa aliendelea kutumia nguvu ya uongozi wake ili kupambana na wahusika wa vitendo hivyo hadi kuwafikisha mahakamani na kupewa adhabu, jamii ndio ikaanza kumuelewa lengo lake hadi sasa wamepata uwelewa wa kuripoti vitendo hivyo.
Mwandishi wa Makala hii alipata tetesi yakuwa kuna mwanamke mwengine ambae ameleta mabadiliko katika jamii yao , hakusita na kupata shauku ya kuongea na mama huyo.
Siwema Mshenga Issa mwenye umri wa miaka 45 mkaazi wa Bubwini Makoba ambae ni mjumbe wa kamati ya utekelezaji katika jimbo la bubwini kupitia chama cha mapinduzi CCM , aliyeanzisha kikundi cha ulinzi wa mazingira katika kijiji hicho mwaka 2004 na miongoni mwa sababu ya kuanzisha kikundi hicho ni kushamiri magonjwa ya mripuko katika kijiji chao.
“ Katika mwaka 2004 Magonjwa ya mripuko yalishamiri katika kijiji chetu, kila mtu akiwa na wasiwasi wa maradhi hayo, watoto wetu tuliwazuia kwenda skuli ili wasijenunua au kula vyakula vyenye vimelea vya wadudu, kila mzazi hofu ya mtoto wake ilimtanda, ujasiri niliokuwa nao katika uongozi wangu ulinifanya nianzishe kikundi cha ulinzi wa usafi wa mazingira.” Amesema Siwema
“ Nilipokuja na wazo hilo katika kijiji changu wapo ambao waliniunga mkono na wengine kunipinga ,ila sikukata tamaa tukaweka kamati mbili mmoja ilishughulikia kufanya usafi maeneo ya pwani na nyengine maeneo ya nchi kavu.tukiwa na wananchama 30 lakini kwasasa tupo wanachama 26 ,wanawake 10 na wanaume 16 na upungufu huu umetokana na wengine kufariki Ameongezea Siwema
Licha ya kujitolea kwake ili kunusuru maambukizi ya magonjwa hayo yasitawale katika kijiji chao, walikutana na changamoto mbalimbali katika kijiji chao ikiwemo kutopata mapokezi mazuri wanapokwenda majumbani kutoa elimu na mara nyingi wanaowapa usumbufu ni wanaume.
“ Bado jamii inamchukulia mwanamke ni chombo cha starehe, hii ni changamoto kubwa inawafika mabinti zetu wakienda kutoa elimu ya usafi wa mazingira majumbani, baadhi ya wanaume kutaka kuwarubuni, vilevile baadhi ya watu kuendelea kutupa taka ovyo pamoja na kukataa miti” Amesema Siwema
Baada ya changamoto zote hizo waliweza kukabiliana nazo na kufanikiwa kuondokana na maradhi ya mripuko na wananchi wa kijiji hicho kuweza kumkubali rai yake na kuona hawakukosea kuchagua kiongozi huyo.
Licha ya kuwa mwanamke anajitoa kuwa mstari wa mbele katika kuleta maendeleo katika jamii lakini bado jamii haijamkubali mwanamke kuwa kiongozi na nahii inatokana na takwimu mbalimbali zilizopo.
Kwa mujibu wa Sensa ya watu na makaazi ya mwaka 2022 inaonesha Zanzibar ina watu 1,889,773 kati ya hao wanaume ni 915,492 na wanawake ni 974,281 sawa na asilimia 51.6 ya wakaazi wote Zanzibar .
katika majimbo 50 ya Zanzibar wanawake ni wanane 8 sawa na asilimia 16,wabunge wa Jamuhuri ya Muungano kutoka Zanzibar kwenye 50 wanawake ni wanne tu 4 sawa na asilimia nane 8,mawaziri ni sita 6 sawa na asilimia 33 na makatibu ni saba sawa na asilimia39.
Kwa upande wa wakuu wa mikoa mwanamke ni mmoja sawa na asilimia 20,wakuu wa wilaya wanne sawa na asilimia 36 na masheha wanawake 79 sawa na asilimia 20, wanaume 309 sawa na asilimia 80 kwa masheha wote wa Unguja na Pemba ambao ni 388.
Mikataba mbalimbali ya kimataifa imeweka makubaliano kati ya mataifa ambayo yanaweza kusaidia kuboresha hali ya wanawake hasa wale wenye uchumi mdogo .Na hii ni muhimu kwasababu wanawake wengi wanakabiliwa na vikwazo vya uchumi ili kufikia uongozi.
Mfano wa mikataba hiyo ni mkataba wa umoja wa mataifa kuhusu haki za kisiasa na kiraia (ICCPR), mkataba wa umoja wa mataifa kuhusu haki za wanawake (CEDAW)pamoja na mkataba wa malengo endelevu (SDGs) na mikataba hii inaimarisha sera za kitaifa .
Hivyo, mikataba hii ni shindikizo kwa serikali kuundaa sera zinazosaidai wanawake wenye uchumi mdogo kwa kueka sheria ambazo zitaondoa vikwanzo vya kiuchumi kwa wanawake, vilevile baaadhi ya mikataba kutoa rasili mali kwa kuwezesha katika kuwapa elimu na mafunzo ili kuweza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi
Kalamu ya mwaandishi huyu ilifunga safari hadi tume ya uchaguzi Zanzibar ili kujua fursa mbalimbali za mwanamke katika tume hiyo na kubahatika kukutana na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa tume hiyo, Thabit Idarous.Amesema wanawake wamepewa fursa mbalimbali za uchaguzi tofauti na historia ya nyuma kwani walikuwa wananyimwa haki hiyo.“ Kutoka mwaka 2015 hadi 2020 wamejitokeza wanawake takriban 80 kupitia nafasi mbalimbali ikiwemo mwakilishi ikilinganishwa na wanaume zaidi ya 400 waliojitokeza kugombea.”Amesema Thabit
“ Changamoto kubwa ipo katika vyama vya siasa ,hivyo vitakapofanya marekebisho ya sera maalumu ambayo itatoa ushawishi wa kuongeza idadi ya viongozi wanawake kwenye majimbo, itasaidia kuwa na muaroubaini wa tatizo hilo.” Ameongezea
Katibu Mkuu wa Chama cha demokrasia cha Umoja wa Watu Hamad Ibrahim amekiri kuwa wanawake wanaushawishi wa kuleta mabadiliko katika jamii, lakini bado wanakabiliwa na changamoto kadhaa zinazowazuia kushiriki katika nafasi za uongozi .“Wanawake ndio washawishi wakuu katika kuhamasisha wanawake wenzao katika mambo mbalimbali ikiwemo kushiriki katika mabaraza ya kisiasa na serikali, lakini kinachosikitisha nafasi ya ushiriki katika uongozi ni mdogo kutokana na wao wenyeo kuwa na hofu ya kushika nafasi hiyo.”Amesema Hamad
Ukiachia sababu ya hofu inayowakwamisha ushiriki wao, vilevile kuna vikwazo vya kijamii na kiutamaduni ambavyo baadhi ya jamii ina mitazamo ya kihistoria ya nyuma kuwa mwanaume ndio anastahiki kuwa kiongozi na mwanamke kuwa mtekelezaji au msaidizi.
0 Comments