Ikiwa imebaki miezi tisa pekee kufikia kwenye uchaguzi mkuu nchini Tanzania 2025 wanawake wameonyesha utayari wa hali ya juu wa kugombea nafasi mbalimbali za uongozi.
Uchaguzi huo unategemewa kuwa na ushindani mkali, lakini licha ya mafanikio madogo yaliyopatikana katika kuhimiza usawa wa kijinsia katika siasa, bado wanawake wanakutana na changamoto nyingi katika jitihada zao za kushika nafasi za juu za uongozi, kutokana na vikwazo vya kijamii, kiuchumi, na kiutamaduni.
Changamoto hizo za kijinsia, mtazamo hasi wa jamii, na upungufu wa rasilimali za kuendeshea kampeni za kisiasa, bado ni kikwazo kikubwa kwa wanawake wengi hao.
Ingawa vyama vya siasa vimeanzisha mikakati ya kuwawezesha wanawake, bado kuna upungufu wa ufanisi katika utekelezaji wa mipango hii.
Mikataba ya kimataifa kama vile Itifaki ya SADC, CEDAW, na Itifaki ya Maputo inasisitiza umuhimu wa kuleta usawa wa kijinsia katika siasa, lakini utekelezaji wake ni changamoto kubwa.
Wataalamu wengi wanasisitiza kuwa licha ya mikataba hii kuwa na lengo zuri, bado inakuwa vigumu kwa baadhi ya nchi kuitekeleza kikamilifu kutokana na mila na desturi za kijamii zinazozuia wanawake kushiriki katika siasa licha ya uwezo mkubwa walionao wanawake hao.
Amina Halil, alisema uwezo wa wanawake huonekana pale wanapopewa dhamana ya uongozi, akitolea mfano Rais wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan namna anavyoongoza nchi kwa weledi mkubwa.
“Unaona hasa mabadiliko ya kiuchumi, miradi mikubwa ya kimaendeleo, busara na hekma zake ambazo sifa hizi utazipata kwa mwanamke, ipo haja kuwaunga mkono wanawake watakaojitokeza uchaguzi mkuu ujao kwa kweli hatutupi nafasi ila tunawekeza”, alisema Amina.
Ikiwa chama cha ACT-Wazalendo kimeshafungua pazia la watia nia kutangaza ni za kugombea nafasi mbalimbali za uongozi Mwanamke mmoja kutoka kwenye chama hicho Mjini Unguja ambae hakupenda kutajwa jina lake alisema kwa kawaida chama chao kila jimbo kinasimamisha mwanamke na mwanamme nyakati za chaguzi kuu kutoka tangu CUF mpaka sasa ACT Wazalendo.
“Mimi niliwahi kugombea jimbo kupitia chama changu na nia nnayo nitasimama tena Allah akiniweka hai 2025 nawataka hata wanachama wa chama chengine kuwaunga mkono wanawake wanaosimama kutaka uongozi majimboni”, alisema.
Mwanamke mwengine aliyejitambulisha kwa jina la Fatma pekee,ambaye ni mwanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM), alisema kuwa wanawake wanahitaji kujitokeza kugombea majimbo na kushiriki katika siasa, lakini akatoa wito kwao kujitahidi kuongeza ufanisi wao katika siasa ili kushindana na wanaume waliokuwa madarakani kwa muda mrefu.
"Kuna wanaume wanaojiona kama wamiliki wa majimbo yao, lakini wanawake wanahitaji kuwa na mikakati madhubuti ya kuweza kuwashinda. Mwaka ujao tunataka kuona wanawake wakishika majimbo kwa ufanisi, si kwa hofu ya kushindwa," alisema Fatma.
Shemsa Abdalla Ali ni Mwenyekiti wa umoja wa wanawake Tanzania UWT Mkoa wa Kusini Unguja alisema licha ya mkoa huo kuwa na viongozi wengi wanawake lakini wote wakiwa si wa majimbo hivyo jumuiya inaandaa mpango madhubuti wa kuwa na wawakilishi na wabunge wanawake wa majimbo.
“katika mkoa wetu tuna viongozi 10 kwa ngazi ya uwakilishi na ubunge lakini wote ni wa viti maalumu lakini kwenye uchaguzi huu tutahakikisha tunapata viongozi wanawake kutoka Majimboni. Alisema Shemsa
Wakati wananchi wakiwa wanataka kuona wanawake wakishiriki katika siasa, kuna wasiwasi kuhusu uwezo wao kushindana na wanasiasa wa kiume waliokuwa madarakani kwa muda mrefu. Haji Makame alieleza: “Wanawake wanahitaji uwekezaji zaidi katika elimu na rasilimali ili waweze kufanya vizuri kwenye majukumu ya kisiasa, na si tu kuingia kwa kuhamasishwa na shinikizo la kisiasa.”
Asha Khamis kutoka Amaan aliongeza: “Tunapozungumzia usawa wa kijinsia, tunapaswa kuhakikisha kwamba wanawake wanapata nafasi ya kugombea na kushinda kwa uwezo wao, sio tu kwa sababu ya mkakati wa kisiasa."
Hakuna shaka kuwa ili kufikia usawa wa kijinsia, wanawake wanahitaji kujiandaa kwa namna ya kipekee na kujipanga vizuri zaidi katika kupata nafasi za uongozi.
Naibu Katibu Mkuu wa UWT Zanzibar, Tunu Juma Kondo, alisema: “Tunaendelea kutoa mafunzo kwa wanawake, lakini lengo letu ni kuhakikisha kwamba wanajiandaa kifikra, kiuchumi, na kimkakati ili waweze kushindana kwa haki katika uchaguzi ujao."
Kuelekea uchaguzi wa 2025, kuna matumaini kwa wanawake kuongeza idadi yao katika nafasi za uongozi. Hata hivyo, bado ni safari ndefu kwa wanawake kufikia usawa wa kijinsia, kwani changamoto zinazozunguka suala hili ni kubwa.
Ingawa vyama vya siasa na wadau mbalimbali wanajitahidi kuwawezesha wanawake, jamii bado inapaswa kubadilisha mtazamo wake na kukubali kwamba wanawake wana uwezo wa kushika nafasi za uongozi, bila kujali changamoto zinazozunguka ushiriki wao.
0 Comments