Na Nahifadhi Abdulla.
Wanawake wamekuwa wahanga wa vitendo vya ukatili wa kijinsia, unyanyasaji wa kisiasa, na ukosefu wa usalama wakati wa uchaguzi katika maeneo mbalimbali duniani, na Zanzibar haijawahi kuwa tofauti.
Huku uchaguzi mkuu wa 2025 ukikaribia, kuna haja ya kuimarisha hatua za kulinda usalama wa wanawake si tu kama wapiga kura bali pia kama washiriki wa moja kwa moja katika mchakato wa uchaguzi, wakiwemo wagombea, mawakala, na wanaharakati wa kisiasa.
Ripoti ya Umoja wa Mataifa kuhusu ukatili wa kijinsia wakati wa uchaguzi inaonyesha kuwa ukosefu wa usalama kwa wanawake katika mazingira ya kisiasa huathiri ushiriki wao na kushusha viwango vya uwakilishi wa kijinsia. "Hakuna demokrasia inayoweza kufanikiwa bila usawa wa kijinsia na ushiriki wa wanawake," ilisema ripoti hiyo.
Zanzibar, ikiwa sehemu ya mfumo wa kisiasa unaokua, inapaswa kuwekeza zaidi katika kulinda wanawake na kuhakikisha wana nafasi sawa na wanaume katika uongozi na mchakato wa uchaguzi.
Katika chaguzi zilizopita, wanawake waliripotiwa kukumbana na vitisho vya kimwili na vya kiakili, unyanyasaji wa maneno, na wakati mwingine vurugu za moja kwa moja. Vitendo hivi vinawalenga zaidi wanawake walio mstari wa mbele katika siasa au wale wanaoshiriki kampeni za wagombea.
Utafiti wa Kituo cha Uongozi wa Wanawake wa Afrika (AWLN) unasisitiza kuwa wanawake wanakumbana na aina tatu za ukatili wa kisiasa: ukatili wa kimwili, kiuchumi, na kisaikolojia. Hali hii mara nyingi hutokana na mfumo dume uliojikita katika siasa za nchi nyingi za Afrika, ikiwemo Zanzibar.
“Wanawake wanapotishiwa kwa sababu ya kushiriki katika siasa, wananyimwa nafasi yao ya msingi katika jamii. Hili siyo tu suala la haki za binadamu, bali pia ni suala la maendeleo ya kidemokrasia,” alisema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, katika tamko lake kuhusu haki za wanawake katika siasa.
Kwa Zanzibar, kuna haja ya kuweka mikakati madhubuti kuhakikisha wanawake wanakuwa salama wakati wa uchaguzi. Mikakati hii inaweza kujumuisha,
Elimu ikiwa kama sehemu muhimu katika kupambana na vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake. Serikali, mashirika yasiyo ya kiserikali, na vyombo vya habari vinapaswa kushirikiana kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa kulinda wanawake wakati wa uchaguzi. Hii itasaidia kupunguza vitendo vya unyanyasaji wa maneno na kimwili vinavyolenga wanawake.
Pili Kuimarisha Vyombo vya Usalama hili linapaswa kupewa mafunzo maalum ya kushughulikia kesi za ukatili wa kijinsia wakati wa uchaguzi. Umoja wa Mataifa unapendekeza kuwa polisi wanapaswa kuwa na vitengo maalum vya kushughulikia matukio ya ukatili wa kijinsia ili kuhakikisha wanawake wanaweza kutoa ripoti bila woga.
Suala la Sheria Kali Dhidi ya Ukatili wa Kisiasa ziwekwe ili ziweze kusimamia ukatili wa kisiasa ni njia moja ya kuzuia matukio haya. Zanzibar inaweza kuiga mifano ya nchi kama Rwanda, ambapo sheria zinatoa adhabu kali kwa watu wanaotenda ukatili wa kisiasa dhidi ya wanawake.
Na la mwisho ni kuundwa wa Mabaraza ya Kusaidia Wanawake,Mabaraza ya kijamii na vikundi vya ulinzi vya wanawake vinaweza kusaidia katika kushughulikia changamoto za usalama wakati wa uchaguzi. Mabaraza haya yanaweza kutoa msaada wa kisaikolojia na hata usaidizi wa kisheria kwa wanawake wanaokumbana na vitisho.
Pia tunaweza kujifunza kwa nchi nyingine ambazo zimefanikiwa kulinda usalama wa wanawake katika mchakato wa uchaguzi. Katika nchi kama Sweden, ushiriki wa wanawake katika uchaguzi ni wa hali ya juu kutokana na kuwepo kwa mazingira salama na shirikishi.
Katika nchi za Afrika kama vile Afrika Kusini, mashirika ya kiraia yamekuwa yakishirikiana na serikali kuhakikisha wanawake wanapewa ulinzi wa kutosha wakati wa uchaguzi. Ripoti ya Umoja wa Mataifa kuhusu usalama wa wanawake wakati wa uchaguzi inasisitiza kuwa, “ushirikiano kati ya serikali, vyombo vya usalama, na mashirika ya kiraia ni muhimu katika kuhakikisha wanawake wanashiriki kikamilifu katika siasa.”
Ili Zanzibar iweze kufanikisha uchaguzi wa 2025 ulio salama ikiwa hatua za haraka zitchukuliwe kulinda usalama wa wanawake. Ulinzi huu haupaswi kuwa wa muda mfupi tu wakati wa uchaguzi, bali unapaswa kuwa sehemu ya mabadiliko ya mfumo wa kisiasa kwa ujumla.
Wanawake ni msingi wa maendeleo ya jamii, na usalama wao ni kigezo muhimu cha demokrasia imara. Kama alivyosema Eleanor Roosevelt, “Haki za binadamu zinaanza nyumbani, katika maeneo ya karibu na pale ambapo hakuna mahakama ya kimataifa inayoweza kuzifikia.” Hivyo, ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha Zanzibar inakuwa mfano wa kuigwa katika kulinda haki za wanawake na kujenga jamii inayozingatia usawa wa kijinsia.
0 Comments