Na Ahmed Abdulla, Zanzibar:
Katika muktadha wa dunia ya sasa, usawa wa kijinsia umekuwa ni suala la muhimu sana, hasa linapokuja suala la nafasi za uongozi kwa wanawake.
Miongoni mwa mbinu zinazotumika kukuza uwezo wa uongozi kwa watoto wa kike ni kupitia klabu za jinsia mashuleni.
Klabu hizi zimekuwa zikiwapa watoto wa kike fursa ya kujiandaa mapema kwa majukumu ya uongozi kwa kuwapatia ujuzi, uelewa, na motisha ya kuwa viongozi bora katika jamii zao.
Klabu za jinsia mashuleni hutoa mazingira salama ambapo watoto wa kike wanaweza kujifunza na kushirikiana bila hofu ya kukandamizwa.
Kupitia mijadala, michezo ya kuigiza, na shughuli za kijamii, wanafunzi wanajifunza namna ya kujieleza na kujenga ujasiri wa kushiriki katika maamuzi muhimu.
Ujasiri huu ni nguzo muhimu kwa viongozi wa kesho kwani huandaa watoto wa kike kuwa na sauti na ushawishi katika jamii.
Klabu hizo hujumuisha wanafunzi wa jinsia zote mbili ikiwa ni lengo la kuondoa hofu na uwoga wa kufanya kazi katika maeneo yenye mikusanyiko ya watu wa jinsia toafauti.
Skuli ya sekondari Makoba ni moja ya skuli zilizoanzisha klabu ya jinsia ambazo zimekuwa na mchezngo mkubwa wa kuwasaidia wanafunzi kujitambo na kufahamu vipi wanaweza kusaidiana pale wanapopata vikwazo mbalimbali ikiwemo unyanyasaji na ukatili wa kijinsia.
Lakini mbali na hayo wanafunzi hao wamepata utambuzi kuwa wanawake wananafasi sawa na wanaume kwenye kuijenga serikali ya wanafunzi ya skuli hiyo.
Shadida Mohammed Khamis ni mmoja wa wanaklabu ya jinsia kutoka skuli ya sekondari Makoba Amesema akiwa miongoni mwa wanaklabu mkakati wao ni kuwahamasisha wanafunzi zaidi juu ya uwezo alionao mwanamke katika uongozi.
“Mkakati wetu ni kuhamasisha wanafunzi wa kike na wakiume wafahamu kuwa mwanamke naye anahaki ya kuwa kiongozi” alisema Shadida
Kwa upande wa Ussi Ali Shadhil ambaye naye ni mwanaklabu wa jinsia wa skuli hiyo kwanza alitoa maana ya usawa wa kijinsia katika nafasi za kuongozi kwa kusema usawa wa kijinsia katika uongozi ni pale anapochaguliwa kiongozi bia ya kuangalia toafauti ya jinsia.
“Mwanamke anaweza kwelikweli kuongoza hivyo tutatoa elimu hii kwa walimu na wanafunzi ili kuzingatia usawa wa kijinsia katika chaguzi zetu za skuli pamoja na uteuzi wa nafasi mbalimbali” alisema Ussi
Salma Mgeni Msuri ni Mwalimu wa ushauri na unasihi kutoka skuli ya sekondari makoba yeye alisema baada ya kuanziasha klabu hiyo wanafunzi wamepata uelewa wa namna ya kuepuka matendo maovu ikiwemo udhalilishashi na ukatili wa kijinsia.
“Kuna mwanafunzi mmoja baba yake alitolewa kwenye vyombo vya habari kuwa amefanya matendo yasiyofaa hivyo Yule mwanafunzi ilimuathiri kwasababu mwanafunzi wenziwe walikuwa wakimfanyia dhihaka hivyo kilabu ilifanya kazi yake kwa kuwapa elimu juu ya athari za kumfanyia dhihaka mwanafunzi mwenzao” alisema mwalimi Salma
Akizungumzia suala la uongozi mwalimu Salma alisema kuwa wanafunzi hasa wasichana wako vizuri kwani wale ambao wapo katika serikali ya wanafunzi wamekuwa wakitekeleza majukumu yao kwa ukamilifu.
“Mwanzo wasichana wenyewe walikuwa hawataki kuwa raisi wa serikali ya wanafunzi wa Skuli hii lakini kwa sasa wananiambia wako tayari kuchukuwa nafasi hiyo ya uraisi” alisema
Mwisho alitoa wito kwa skuli nyingine “klabu zinamchango mkubwa kwa wanafunzi kuibua changamoto zao hivyo nazinasihi skuli nyingine zianzishe klabu za jinsia ili wazijuwe changamoto za wanafunzi wao.
Wanajamii maeneo ya Bumbwini Makoba wamekuwa na mapokezi gani juu ya klabu za jinsia katika skuli hiyo?
Kwa upande wa mkazo wa kijiji hicho Makame Shauri Nawaji kuanzishwa kwa klabu ya jinsia katija skuli hiyo ni jambo jema kwani yanawaandaa vyema katika maisha yao baada ya kumaliza elimu yao ya lazima na ni vipi wataitumikia jamii yao.
“Kama mwanafunzi anapokuwa skuli anaona majukumu ya kiuongozi hivyo humpa muelekeo wa namna gani anaweza kutekeleza wajibu wake anapokuwa kiongozi” alisema Makame
Salma Ali ni mzazi wa mwanafunzi Hodaya Vuai Juma ambaye ni mwanmaklabub wa klabu ya jinsia skulini hapo alisema “Mwananu tokea aingie katika klabu hii amekuwa vizuri hata katika mazungumzo yake hatoi maneno machafu”
Aliongezea kwa kusema “Anapokaa na watoto wenziwe huwakataza kufanya mambo yasiyofaa hii inaonyesha uwezo wake wa kuwa kiongozi bora wa baadae”
Katika kuhakikisha lengo la kumfanya mtoto wa kike afikie malengo yake ya kuwa kiongozi hatuwezi kubeza mchango mkubwa unaofanywa na jumuiya zisizo za kiserikali.
Habiba Stumai Said ni Afisa Programu kutoka jukwaa la walimu wanawake wa kiafrika upande wa Zanzibar FAWE-Zanzibar alisema awali ilikuwa watoto wa kike wanashindwa kuwa viongozi kwa sababu ya kutokuwa na uthubutu wa kugombania nafasi za uongozi.
“Klabu hizi zimeundwa mahsusi kwa ajili ya kuwajengea watoto wa kike uwezo wa kujiamini na uwezo wa kuyafikia malengo yao” alisema Habiba
Aliongeza kuwa “Tangu zianzishwe hizi Klabu kuna matokeo mazuri kwani kuna wanafunzi wameanza kujiamini na tunamatarajio ya kupata mafanikio zaidi wa wale wanafunzi waliopata mafunzo ya Uongozi”
Aidha alisema wanamatarajio makubwa kuona usawa wa kijinsia kwenye nafasi za uongozi katika Serikali za wanafunzi kwani wanafunzi wakike wao wenyewe wameshaanza kuwa na hamu ya kuwa viongozi.
“Moja ya jambo ambalo tutajivunia ni kuwa mwanafunzi mwanzo alikuwa hawezi hata kusimama mbele ya watu ila kwasasa anaweza na kufanya kitu ambacho ni kizuri kwa wenzake” alisema
Dkt. Mzuri Issa ni mkurugenzi wa Chama Cha Waandishi Wanawake Tanzania upande wa Zanzibar TAMWA-ZNZ aliimba Serikali kuweka mkazo kwenye uanzishwaji wa klabu za jinsia kwa skuli zote.
“Tunahitaji viongozi waliopikwa kwenye misingi ya usawa wa kijinsia Serikali haina budi kuweka mkazo juu ya uanzishwaji wa klabu za jinsia katika skuli zote” Alisema Dkt. Mzuri Issa
Naibu waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Anna Attanas Paul alisema ni jambo la kujivunia kuona watoto wanajengeka vyema kwenye suala la usawa wa kijinsia wakiwa katika klabu za jinsia za skuli.
“Wizara ninayoitumikia tutashirikiana vyema na wizara ya elimu ili kuona watoto wanaandaliwa na wanakuwa imara kwenye kuzingatia haki na usawa wa kijinsia” Alisema
Klabu za jinsia mashuleni zina mchango mkubwa katika kuwaandaa watoto wa kike kuwa viongozi wa kesho.
Kupitia kujifunza ujasiri, ujuzi wa uongozi, na kuelewa haki zao, watoto wa kike wanajengwa kuwa watu wenye uwezo na ushawishi katika jamii.
Hivyo ni muhimu kwa shule kuendelea kuanzisha na kuimarisha klabu hizi ili kuhakikisha usawa wa kijinsia na kuwawezesha watoto wa kike kufikia malengo yao ya uongozi
0 Comments