NA AHMED ABDULLA,Zanzibar
Ukataji wa mikoko unaendelea kwa kasi ya kutisha, na madhara yake yanazidi kuonekana na ardhi inaendelea kumomonyoka, huku jamii za pwani zikiwa katika hatari ya kupoteza kila kitu.
Ukataji wa mikoko si tu tishio kwa mazingira, bali pia ni pigo kubwa kwa uchumi wa jamii zinazotegemea rasilimali hizi pamoja na hewa safi. Je, tutaendelea kushuhudia athari hizi kubwa kimya kimya?
Mikoko si tu miti ya kawaida bali ni nguzo muhimu kwa maisha ya viumbe wa baharini, jamii za pwani, na hata mfumo wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi wa dunia.
Mikoko huzuia mmomonyoko wa ardhi, hufyonza kiwango kikubwa cha hewa chafu, na kutoa hewa safi, Pia ni makazi muhimu kwa samaki na viumbe wengine wa baharini.
Hata hivyo, mikoko imekuwa ikikatwa kwa ajili ya kuni, ujenzi, na shughuli nyingine za kibinadamu, hali ambayo inaathiri kwa kiwango akikubwa mazingira yetu.
Kijiji cha Uzi, kilichopo Zanzibar umbali wa kilomita 34 kutoka Mji Mkongwe kisiwani Unguja, ni mfano halisi wa madhara ya ukataji wa mikokokwani kijiji hiki, kilichozungukwa na maji ya bahari katika maeneo mengi, sasa kinakabiliana na mmomonyoko wa ardhi, kupungua kwa uzalishaji wa mazao ya chakula, na athari kubwa za kiuchumi kwa wakazi wake.
Rahma Nassor Omar, mkulima kutoka kijiji cha Uzi, anaeleza changamoto wanazokabiliana nazo kwa huzuni: “Tunaendelea kutibu majangwa ambayo yanatupunguzia uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara.”
Awadh Mwiga Ngau, mkazi mwingine wa kijiji hicho, anatoa wito wa mshikamano wa pamoja katika kurejesha hali ya kawaida ya kijiji hicho: “Mikoko ilikatwa bila kufikiria athari hizi. Tuungane kutibu jeraha hili,” anasema kwa msisitizo.
Sheha wa Uzi, Othman Mwinyi Haji, anaeleza kuwa kijiji hicho kinaendelea kuteseka na athari za ukataji wa mikoko uliofanyika kipindi cha nyuma:
“Athari za ukataji wa mikoko katika kisiwa cha Uzi zimeleta tafrani kubwa, ikiwemo maji ya chumvi kuingia katika mashamba yetu ya kilimo.” Anasema na kuonyesha matumaini yake baada ya kuanzishwa kwa mradi wa ZANZADAPT: “Baada ya kuja mradi huu, tunamatumaini ya kupungua kwa athari hizi kwa kiasi kikubwa.”
Jumuiya zisiyo za kiserikali na Serikali zimeanza kuchukua hatua kurejesha uoto wa mikoko ambapo Jumuiya ya Community Forest Pemba (CFP), kupitia mradi wa ZanzAdapt, inalenga kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi na kusaidia jamii zilizoathirika katika vijiji vya Uzi, N'gambwa, Unguja Ukuu, na Bungi kisiwani Unguja.
Mbarouk Mussa Omar, Mkurugenzi Mtendaji wa CFP, anaeleza: “Mradi unatoa kipaumbele kwa wakulima wadogo, hasa wanawake, kwa kuwasaidia kupanda miche ya matunda na miti ya misitu.”
Wanawake wamekuwa mstari wa mbele katika jitihada hizi, wakishiriki kwa wingi kwenye upandaji wa mikoko na kushirikiana katika miradi ya kilimo endelevu.
Mahfoudh Shaaban Haji, Mkurugenzi wa Zanzibar Climate Change Alliance (ZACCA), anaeleza: “Tunatoa elimu kwa jamii kuhusu athari za ukataji wa mikoko na mabadiliko ya tabianchi.”
Wanawake katika kijiji cha Uzi, kwa kushirikiana na mashirika haya, wamepewa mafunzo maalum ya uongozi na ujasiriamali ili kuwajengea uwezo wa kushiriki kikamilifu katika juhudi za kulinda mazingira.
Salum Rehani, Mkuu wa Wataalamu wa Kilimo Zanzibar, anasema: “Tunawaelimisha wanajamii kupanda miti inayoweza kuzuia upepo na maji ya kuchukuwa eneo la ardhi. Pia tunahimiza matumizi ya nishati safi badala ya kuni.”
Serikali nayo imechukua hatua kwa kuanzisha mpango wa kuotesha miche milioni moja, ikiwemo ya mikoko, kila mkoa.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, maliasili na Umwagiliaji Zanzibar, Ali Khamis Juma, alisema: “Wananchi wanapaswa kuchangamkia fursa ya kupanda miti hii ili kupunguza maji ya chumvi kuingia mitaani.”
Kwa pamoja, hatua hizi zinaweza kusaidia kurejesha uoto wa asili wa mikoko, kulinda mazingira, na kuboresha maisha ya jamii za pwani.
Wanawake, wakiwa nguzo muhimu katika juhudi hizi, wameonyesha kuwa suluhisho la changamoto za mazingira lipo katika mshikamano wa kijinsia na kujituma kwa pamoja. Mikoko ni uhai, na kulinda uhai ni jukumu letu sote.
0 Comments