NA AHMED ABDULLA:
Katika karne ya 21, teknolojia
imekuwa nguzo muhimu katika maisha ya kila siku, na mitandao ya kijamii ni
sehemu kuu ya mabadiliko hayo.
Mitandao ya kijamii ni majukwaa
yanayomuunganisha mtu na kundi la watu kwa haraka na urahisi kwa kutumia
teknolojia ya mawasiliano.
Kulingana na takwimu kutoka Mamlaka
ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), hadi kufikia Mwezi Septemba 2024, takribani
Watanzania milioni 41.4 kati ya milioni 61.7 wanatumia huduma za intaneti,
hivyo mitandao ya kijamii inakuwa sehemu muhimu ya mawasiliano.
Zanzibar, kama sehemu ya Tanzania,
haiko nyuma katika kujiunga na dunia ya kidijitali. Hata hivyo, licha ya kuwepo
kwa fursa nyingi katika teknolojia hiyo lakini bado wanasiasa wanawake visiwani
Zanzibar hawajatumia ipaswavyo mitandao
hiyo, hasa katika muktadha wa kisiasa.
Moja ya
fursa zinazotokana na mitandao ya kijamii kwa wanasiasa ni kupunguza matumizi
makubwa ya fedha kwenye kufanya kampeni ambapo Murtadh Mbarak Saleh kijana anayeamini
kwenye matumizi ya mitandao ya kijamii anasema mitandao hiyo inapunguza
matumizi makubwa ya fedha kwa wagombea
wa nafasi za kisiasa.
“Mitandao
ya kijamii inapunguza matumizi makubwa ya fedha wakati wa kufanya kampeni kwa
kuwafikia watu wengi kwenye mkutano mmoja” anasema Murtadh
Murtadh
anaendelea kwa kusema “Wanasiasa Wanawake wataondokana na changamoto ya
matumizi makubwa ya fedha pindi wakitumia mitandao hiyo wakati wanaposaka
uongozi na hii itasaidia kufikia asilimia 50 kwa 50 ambayo dunia inaitamani”
Farida Mohameed ni mkurugenzi wa
taasisi ya Zanzibar Youth Talk anaitaja faida ya pili ya mitandao ya kijamii
kuwa ni kuwafikia hadhira wengi kwa muda mfupi.
“Kama vijana tumekuwa tukifanya
kampeni zetu kupitia mitandao ya kijamii na imeleta tija kubwa” Anasema Farida
Aidha anawasisitiza wanawake kwa
kusema “Tuache visingizio tuitumie vye mitandao ya kijamii tufikie malengo yetu
ikiwemo ya kisiasa”
Hizo ni miongoni mwa fursa chache
zinazotokana na matumizi ya Mitandao ya Kijamii kwa wanasiasa lakini wanasia
wanawake hawajaichangamkia fusra hiyo.
Suhaila Ussi Pondeza, mjumbe wa
Kamati ya Utekelezaji ya Umoja wa Wanawake wa Chama cha Mapinduzi Tanzania
(UWT) Wilaya ya Amani Kichama ambapo kwa kanuni ya jumuiya hiyo nafasi hiyo
huchaguliwa kwa kupigiwa kura na wajumbe, anakiri kuwa licha ya kuwa na kurasa
za mitandao ya kijamii, hajazitumia kikamilifu katika harakati zake za kisiasa.
Anasema, “Mitandao ya kijamii ina
fursa kubwa hasa kwetu wanasiasa wanawake sasa nitaitumia kikamilifu.”
Hii inaonyesha kuwa ingawa
wanatambua umuhimu wa mitandao ya kijamii, wanawake wengi bado hawajachukua
hatua madhubuti kutumia vyema jukwaa hilo.
Maua Mohammed Mussa, ni mwanasiasa
aliyegombea nafasi ya Ubunge katika Jimbo la Shaurimoyo kwa tiketi ya Chama cha
ACT-Wazalendo mwaka 2020, anazungumzia changamoto ya kutokuwepo kwa elimu ya
kutosha kuhusu matumizi ya mitandao ya kijamii, hasa kwa wanawake.
Anakiri kwamba alikosa fursa nyingi
kwa kukosa ufanisi katika matumizi ya mitandao ya kijamii.
“Tatizo kubwa ni kuwa wanawake wengi
tuna changamoto ya kutokuwa na elimu juu ya matumizi ya mitandao hii,”
anamaliza Maua.
Nchini Tanzania unapokuwa mwanasiasa
ni lazima uwe na chama cha siasa hivyo Zanlight
Blog imewatafuta baadhi ya viongozi wa vya siasa kujuwa mkakati wa vyama vyao juu ya kuwahimiza wanasiasa
wanawake kutumia mitandao ya kijamii kwenye harakati za kisiasa?
Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanawake wa CCM Zanzibar
Tunu Juma Kondo anasema, “Tunawahamasisha wanawake kutumia mitandao ya kijamii
lakini bado hawajashawishika kwa kiasi kikubwa na hii ni kutokana na
kutokuishughulikia mitandao hiyo”
Haji Abeid Haji ni Mkuu wa idara ya
oganezesheni na uchaguzi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA ofisi kuu
ya Zanzibar anasema wamefanya mafunzo ya mara kwa mara kwa vijana na wanawake
wa chama hicho katika kuitumia mitandao ya kijamii.
“katiba ya chama chetu inaitambua
mitandao ya kijamii na ndio mana tunafanya vikao vya mtandao” anasema Haji huku
akiongeza kwa kuwasisitiza wanawake wa chama hicho kujikita katika kutumia
zaidi mitandao ya kijamii kama njia ya kujitangaza na kuelezea kazi zao
wanazozifanya.
Mkurugenzi wa chama cha waandishi wa
habari wanawake Tanzania upande wa Zanzibar TAMWA-ZNZ Dkt. Mzuri Issa anasema
licha ya changamoto zilizopo kwenye matamizi ya mitandao ya kijamii lakini bado
wanawake wanapaswa kusimama imara kwenye kuitumia mitandao ya kijamii hasa
kwenye harakati zao za kisiasa.
“Zipo changamoto kwenye matumizi ya
mitandao ya kijamii lakini kama wanawake ziturudishe nyuma tutumie kwenye
kufanya shughuli zetu za kisiasa ili tuwafikie watu wengi kwa muda mfupi”
anamaliza Dkt. Mzuri
Mtaalamu
wa mitandao ya kijamii visiwani Zanzibar Mukrim Mohammed anaeleza fursa nyingi
zitokanazo na matumizi ya mitandao hiyo.
Moja ya
fursa hizo aanitaja kuwa ni kuwa inamsaidia mwanasiasa anayetumia mitandao ya
kijamii katika kujichanganya na wanachi wake hali inayomrahisishia kutambulika
kwa haraka.
“Hii
inatokana na fursa wanayoipata wananchi wako katika kutoa maoni yao kwenye
majukwaa ya mitandao hiyo” anasema Mukrim
Aidha anavishauri
vyama vya siasa kuandaa mafunzo ya kuwajengea uwezo wanachama wao hasa wanawake
kwenye kutumia kwa usahihi majukwaa ya mitandao ya kijamii.
“Na
wakishapata hayo mafunzo wawe na uthubutu wa kuwavutia hadhira kwenye majukwaa
yao ili kazi zao zionekane kwa haraka na wafikie malengo yao ya kisiasa” Anaongeza
Mukrim
Kwa muktadha huo, ni wazi kuwa
mitandao ya kijamii ina fursa kubwa kwa wanasiasa wanawake hivyo, kuna haja ya
kuimarisha mikakati ya kuwaelimisha wanawake kuhusu matumizi bora ya mitandao
ya kijamii.
Serikali, vyama vya siasa, na
mashirika ya kiraia yanapaswa kushirikiana katika kutoa elimu ya matumizi
sahihi ya mitandao ya kijamii kwa wanawake na kuwahamasisha kutumia mitandao
hayo ili kufikia malengo yao.
Hata hivyo, kupitia juhudi za
kuhamasisha, kuwapa elimu, na kuboresha ufanisi katika matumizi ya mitandao
hiyo, wanawake wana nafasi ya kuleta mabadiliko makubwa katika siasa na jamii.
Ni jambo jema kuona kwamba wanawake
kama Suhaila Ussi Pondeza, Maua Mohammed Mussa, na viongozi wengine wanatambua
umuhimu wa mitandao ya kijamii, na ni matumaini kwamba kwa kufanya matumizi
bora ya mitandao hiyo, wataweza kufikia malengo yao na kuleta mabadiliko chanya
katika jamii na siasa za Zanzibar.
0 Comments