NA AHMED ABDULLA:
Waandishi wa habari wamepewa wito wa kuandika zaidi kuhusu mabadiliko ya tabia nchi ili kuongeza uelewa miongoni mwa jamii na kupunguza athari zake, ambazo mara nyingi huwaathiri wanawake zaidi.
Wito huo ulitolewa na Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA ZNZ), Dk. Mzuri Issa, wakati wa mafunzo ya siku mbili yaliyofanyika Tunguu. Mafunzo hayo yalilenga kuwawezesha waandishi kuandika habari kuhusu wanawake na uongozi katika jitihada za kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabia nchi.
Dk. Mzuri alibainisha kuwa, pamoja na waandishi kuandika habari mbalimbali, uandishi kuhusu mabadiliko ya tabia nchi bado haujapewa kipaumbele cha kutosha. Alisema hali hiyo inachangia kuongezeka kwa athari hizi kwa jamii kila siku.
“Tunazo sera, mikataba na miongozo ya kitaifa, kikanda, na kimataifa kuhusu kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi. Ni muhimu waandishi wa habari kutumia nyenzo hizi kuelimisha jamii kuhusu njia za kukabiliana na athari za mazingira,” alisema Dk. Mzuri.
Kwa upande wake, Meneja Mawasiliano wa TAMWA ZNZ, Sophia Ngalapi, alisema utafiti wa hivi karibuni umebaini kuwa habari zinazohusiana na mabadiliko ya tabia nchi ziko kwa kiwango kidogo katika vyombo vya habari. Alieleza kuwa kupitia mafunzo hayo, waandishi watajengewa uwezo wa kuandika habari hizi kwa kiwango kikubwa zaidi.
Aidha, mkufunzi wa mafunzo hayo, Ali Nassor Sultan, alisisitiza kuwa mabadiliko ya tabia nchi yanayotokana na shughuli za binadamu pamoja na mabadiliko ya asili yameleta athari kubwa katika nyanja mbalimbali za maisha kama vile uchumi na jamii. Alisema ni muhimu kwa waandishi kuonesha athari hizo kwa jamii ili kuhamasisha hatua za tahadhari.
Washiriki wa mafunzo hayo walishukuru kwa elimu hiyo na kueleza kuwa wamepata maarifa muhimu yatakayowasaidia kuandika habari zitakazoleta mabadiliko chanya katika jamii.
Mafunzo hayo
yaliyoandaliwa na TAMWA ZNZ kwa kushirikiana na Community Forest Pemba (CFP) na
Community Forest International (CFI), yamefadhiliwa chini ya mradi wa miaka
miwili unaolenga kuimarisha uelewa wa mabadiliko ya tabia nchi, kilimo
mchanganyiko, upandaji wa mikoko, na uwezeshaji wa wanawake katika uongozi wa
masuala ya mazingira.
0 Comments