NA AMRAT KOMBO:
Katika jamii ya sasa ukosefu wa mafunzo ya uongozi unachukuliwa kuwa ni tatizo linaloweza kuathiri maendeleo ya kisiasa. Na wahenga wanasema kiongozi asiye na mafunzo ni kama meli isiyo na kipande cha mwanga,hawakuishia hapo waliendelea kusema kujifunza ni ufunguo wa mafanikio.
Mwandishi wa gazeti hili alikutana na Aisha Haji Mzee ni kijana mwenye umri wa miaka 25, mwenye mtoto mmoja ,alithubutu kugombea nafasi ya uongozi katika Jimbo la Mwanakwerekwe, ila hakufanikiwa kushinda nafasi hiyo,kama anavyoeleza.
“Niligombea nafasi ya Uwakilishi katika Jimbo la Mwanakwerekwe nikiwa na umri wa miaka 21 ikiwa ni mara yangu ya kwanza kugombea nafasi hiyo,kwa bahati mbaya sikufanikiwa kushinda”.Amesema Aisha.
Vilevile ameelezea kuwa ukosefu wa mafunzo sio sababu ya kushindwa kushika nafasi hiyo bali mtazamo hasi juu ya mwanamke kwa jamii ndio sababu iliofanya akose nafasi hiyo.
“Safari yangu ya kugombea uongozi sikuwahi kupata mafunzo yoyote ila sikuwa na wasiwasi kwani nilikuwa najiamini ” Amesema Aisha
“Jamii ilikuwa haijanikubali,na sio sababu ya mimi kukosa mafunzo ya uongozi ndio ikawa chanzo cha kukosa nafasi hiyo, bali waliniona umri wangu ni mdogo na sitoweza kuleta maendeleo.” Ameongezea Aisha
Kalamu ya mwandishi ilipiga hodi hadi Uroa na kukutana na Maryam Ussi Khamis mweye umri wa miaka 53, aliwania nafasi ya udiwani na kueleza kuwa ukosefu wa elimu ya uongozi ndio kilikua kikwazo cha kutofanikiwa kufikia lengo lake.
“Katika mwaka 2020 niligombea nafasi ya udiwani katika wadi ya Uroa kwa bahati mbaya sikufanikiwa kupata ,kwasababu sikuweza kuwashawishi wananchi ”.Amesema Maryam
“Sikuwahi kupata mafunzo ya uongozi wakati nagombea nafasi hiyo, niliingia kwa hamasa ya chama changu, sikuwa na ujuzi wowote katika suala la uongozi “Ameongezea Maryam
Katibu wa siasa itikadi na uwenezi wadi ya kijitoupele kupitia chama cha CCM Riziki Abdallah Ali hakupishana mbali na kalamu ya mwaandishi wetu iliyogonga hodi kupata nukuu chache juu ya uthibiti ya kauli hii
“Ukosefu wa mafunzo ni chanzo kwa wanawake kushindwa kuwania nafasi za uongozi” alikuwa na hayo yakusema.
"Madarasa ya itikadi ya uongozi ni sehemu muhimu katika kuendeleza uelewa wa viongozi na watu wanaotaka kuwa viongozi.” Amesema Riziki.
Madarasa hayo yanatoa mafunzo kuhusu mbinu, dhana,pamoja na mifano ya uongozi bora ili kuweza kuwasaidia katika mapambano ya kugombea nafasi ya uongozi.Muamko wa wanawake kushiriki katika nafasi ya uongozi umeongezeka tofauti na miaka ya nyuma, ongezeko hilo linatokana na takwimu za sasa ,ambazo kwenye darasa la itikadi washiriki 104 kati ya hao wanawake 83 na wanaume 21 kulinganisha na takwimu zilizopita washiriki 76 kati ya hao wanawake ilikuwa 22 na wanaume ilikuwa 54.
Vilevile amekiri kuwa ukosefu wa mafunzo ya uongozi kwa wanawake ni chanzo cha kushindwa kushika nafasi ya uongozi.
"Wanawake ambao hawajapatiwa mafunzo ya uongozi wanakuwa hawana nguvu ya kujiamini,kubuni mbinu mbalimbali za kugombea, pamoja na ujuzi wa kuwashawishi watu." Amesema Riziki.
Naye Naibu Katibu wa chama cha ACT Wazalendo Zanzibar Omar Ali Shehe amesema kwa upande wa chama chao wanatoa mafunzo ya uongozi kwa wanawake kwa kuandaa makongamano mbalimbali ambayo yatasaidia kupata ujuzi.
“Tunatoa mafunzo ya uongozi kwa kuandaa makongamano ambayo yatawasaidia kupata mbinu ya kugombea nafasi ya uongozi na hii ndio njia bora ambayo inamfanya mwanamke aweze kujiamini wakati anapoenda kugombea.”Amesema Omar
Amethibitisha kuwa madarasa ya itikadi katika chama chao hayapo kwasasa, kwasababu bado muamko wa kueka madarasa hayo hawana.
“Katika chama chetu hatuna madarsa ya itikadi kwasababu bado hatuna muamko wa kueka madarsa hayo kwani tukitaka kutoa mafunzo ya uongozi tunanjia mbalimbali za kufanya ikiwemo mikutano pamoja na semina za uongozi.” Ameongezea Omar
Pamoja na hayo naye Mkurugenzi wa Chama cha waandishi wa habari wanawake TAMWA – ZANZIBAR Dkt Mzuri Issa amesema wanatoa mafunzo mbalimbali ya kuwajengea uwezo wanawake katika kushiriki nafasi za uongozi, ingawa mwanzo ilikuwa muamko ni mdogo lakini kwasasa wanawake wamehamasika kutokana na hamasa wanayopatiwa.
“Sisi tunatoa elimu na kuwahamasisha wanawake kushiriki katika nafasi za uongozi, mwanzo muamko ulikuwa ni mdogo kutokana na ukosefu wa elimu kwa wanawake wanaotaka kugombea, lakini sasa wanawake wameamka na wamehamasika”. Amesema Dkt Mzuri
Vile vile ameeleza kuwa takwimu zinaonesha kwa kipindi hichi wametoa mafunzo kwa zaidi ya wanawake 100 na kati ya hao wamefanikiwa kushinda kwenye chaguzi mbalimbali.
“Tumetoa mafunzo ya uongozi kwa wanawake zaidi ya 100 kati ya hao wanawake 6 wamebahatika kuingia katika majimbo, hali hii ni faraja kwetu kwani tunaona umuhimu wa kuwapatia mafunzo wanawake hao.”Ameongezea Dkt Mzuri
Kwa mujibu wa Sensa ya watu na makaazi ya mwaka 2022 inaonesha Zanzibar ina watu 1,889,773 kati ya hao wanaume ni 915,492 na wanawake ni 974,281 sawa na asilimia 51.6 ya wakaazi wote Zanzibar.Licha ya wingi huo bado kuna upungufu wa wanawake kushiriki katika nafasi za uongozi kutokana na kukosa mafunzo ya uongozi.
Na katika majimbo 50 ya Zanzibar wanawake ni wanane 8 sawa na asilimia 16,wabunge wa Jamuhuri ya Muungano kutoka Zanzibar kwenye 50 wanawake ni wanne tu 4 sawa na asilimia nane 8,mawaziri ni sita 6 sawa na asilimia 33 na makatibu ni saba sawa na asilimia 39.
Mwandishi alibahatika kufanya mahojiano na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar Hamza Hassan Juma amesema ni muhimu kushiriki katika mafunzo ya uongozi kwasababu inasaidia kujifunza mambo mbalimbali ikiwemo kujulikana na watu tofauti pamoja na kupata ujuzi.
“Madarasa ya umoja wa vijana yanamsaidia kijana kushiriki katika mchakato wa kufanya maamuzi katika nchi yao, vilevile anapata kujulikana na wengi, kujiamini pamoja na kupata ujuzi.” Amesema Hamza amethibitisha kuwa wanawake wengi wanashindwa kushika nafasi ya uongozi kwasababu ya kukosa mafunzo ya uongozi tangu wakiwa vijana na kupelekea kutojiamini.
“Lazima vijana washiriki katika madarsa ya itikadi kwasababu yanamjenga tangu akiwa kijana hadi utuzima wake, na kumsaidia katika mapambano ya kugombea nafasi za uongozi bila ya wasiwasi wowote.”Amesema Hamza.
0 Comments