Ticker

6/recent/ticker-posts

Ukimya Unaua: Mapambano Dhidi ya Udhalilishaji Zanzibar Yanahitaji Hatua za Dharura



NA AHMED ABDULLA, Zanzibar:

Katika giza la usiku, wakati familia nyingi zikitarajia usalama majumbani mwao, maelfu ya watoto Zanzibar wanakabiliana na hofu isiyoweza kusemwa. 

Vitendo vya udhalilishaji vimekithiri, vikiwaathiri zaidi watoto na wasichana.

Ripoti iliyowasilishwa na Chama Cha Waandishi Wa Habari Wanawake Tanzania upande wa Zanzibar TAMWA-ZNZ kwenye Mjadala wa kutafuta suluhisho la kumaliza vitendo vya udhalilishaji na Ukatili kwa watoto ikiwa ni maadhimisho ya siku 16 za kupinga vitendo hivyo ilieleza Takwimu za Ofisi ya  mtakwimu Mkuu Zanzibar zinaonyesha hali ya kutisha: kati ya kesi 1,582 za ukatili wa kijinsia zilizoripotiwa mwaka huu kuanzia mwezi Januari hadi Oktoba, 1,337 zilihusisha watoto kati yao wasichana ni 1,095 na wavulana ni 242.

Khairat Haji, Afisa wa Programu kutoka TAMWA-ZNZ, alifichua ukweli huu wa kutisha akisema, "Idadi ya 693 ya kesi hizi zilihusisha watoto wa umri wa miaka 15 hadi 16." Wakati ambapo watoto wanapaswa kuwa salama nyumbani, wengi hukumbwa na madhila kati ya saa 9:00 Mchana na saa 3:00 usiku, akiongeza kuwa changamoto ya kupata haki bado ni kubwa.

Familia na UKimya Wa Kuumiza

Licha ya juhudi za kuhamasisha, familia nyingi huchagua ukimya au maafikiano ya kifamilia, jambo linalowafanya watoto kuwa wahanga zaidi. 

Jesse Mikofu, mwandishi wa habari mkongwe, alisema, "Familia lazima ziwe wazi kuhusu matatizo haya. Watoto wanahitaji nafasi salama ya kuelezea madhila wanayopitia. Kimya kinazidi kuwafanya kuwa wahanga wa kuteswa."

Hata hivyo, muhali katika jamii hutengeneza mazingira ya kuwalinda wahalifu. 

Sabahi Bakari, mtetezi wa haki za binadamu, alieleza kuwa, "Familia za wahanga na watuhumiwa mara nyingi hukutana na kuafikiana, jambo linalowanyima wahanga haki na kuruhusu ukatili kuendelea."

Ubunifu Katika Kutatua Changamoto

Jaji Nayla Abdulbasit wa Mahakama ya Zanzibar ameonyesha kuwa zipo njia za kusaidia watoto kuelezea madhila yao bila woga. 

Kupitia matumizi ya vinyago, watoto wanaweza kueleza kile walichopitia kwa njia ya ubunifu. 

"Kwa kutumia vinyago, watoto wanapata nafasi ya kuzungumza bila woga wa kuonyesha unyanyasaji waliopitia," alisema Jaji Nayla.

Aidha, michezo inatajwa kuwa njia mbadala ya kupambana na ukatili.

Nasra Juma Mohammed, kocha wa soka, alisema, "Michezo inasaidia watoto kuwa na ujasiri na kujijengea uwezo wa kujitetea. Ni njia ya kupambana na ukatili."

Hitaji la Ushirikiano wa Jamii

Katika maadhimisho ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia mwaka huu, kauli mbiu inasisitiza ushirikiano wa jamii nzima kumaliza vitendo vya udhalilishaji. 

Mwatima Issa, Mjumbe wa Bodi ya TAMWA-ZNZ alisema, "Vita hii si ya Serikali au mashirika pekee, bali ni jukumu letu sote."

Mchungaji Shukuru Maloda aliongeza kuwa viongozi wa dini wana jukumu kubwa katika kutoa elimu kwa jamii kuhusu madhara ya ukatili. 

Wakati huo huo, Sgt. Rahima Ali Salum wa Polisi wa Zanzibar alisisitiza umuhimu wa familia kufuata sheria badala ya kupokea fidia isiyo rasmi.

Wakati jamii inapotafakari kauli mbiu ya mwaka huu, ujumbe wa Jaji Nayla unapaswa kutia moyo kila mmoja:

"Tunapaswa kuhakikisha watoto wanajisikia salama, kusikilizwa, na kulindwa. Haki si fursa; ni dhamana kwa kila mtoto."

Vitendo vya udhalilishaji havipaswi kuwa sehemu ya maisha ya watoto wetu. 

Tunapokabiliana na changamoto hizi, hatua za haraka zinahitajika. 

Ukimya unaua; ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha kuwa sauti za watoto zinasikika na haki inapatikana kwa wote.


Post a Comment

0 Comments