Na Khadija Mohammed:
Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA) Zanzibar, kwa kushirikiana na Community Forest Pemba (CFP) na Community Forest International (CFI), pamoja na msaada wa Serikali ya Canada, wameanzisha mradi wa ZanzAdapt, unaolenga kuboresha uongozi wa wanawake katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Kama sehemu ya utekelezaji wa mradi huu, TAMWA Zanzibar imeandaa mkutano wa tathmini na wadau wa mazingira ili kuwasilisha mfumo mpya wa kidijitali wa kukusanya taarifa. Mfumo huu unatarajiwa kusaidia waandishi wa habari walioko katika mradi huo kurekodi na kuhifadhi taarifa kwa urahisi, huku ukiwa na uwezo wa kuhakikisha usalama wa data na kuepuka upotevu wa taarifa.
Mkutano huo ulifanyika katika ofisi za TAMWA Zanzibar zilizopo mkoa wa Kusini Unguja. Lengo kuu la mkutano ni kuhakikisha kuwa taarifa zinazotolewa na washiriki zinabaki salama na zinaweza kufikiwa kwa urahisi, huku waandishi wa habari wakihamasishwa kutumia teknolojia ya kisasa kuhamasisha mabadiliko katika jamii.
Akiwasilisha mada kuhusu mfumo huo, Afisa Tathmini na Ufuatiliaji kutoka TAMWA Zanzibar, Ndg. Moh'd Khatibu Mo'hd, alisema:
"Lengo kuu la kuanzisha mfumo wa kidijitali ni kuhakikisha kwamba taarifa zote zinarekodiwa na zinaweza kufikiwa na kila mtu kwa njia rahisi. Mfumo huu unazingatia mabadiliko ya kisayansi na kiteknolojia, na ni muhimu kwa waandishi wa habari na wadau kutoka sekta mbalimbali kuutumia ili kuhifadhi taarifa kwa usahihi, badala ya kutegemea mifumo ya zamani."
Aidha, Afisa Mawasiliano wa TAMWA Zanzibar, Ndg. Nafda Hindi, alieleza kuwa mfumo wa kidijitali utasaidia kwa kiasi kikubwa kutatua changamoto zilizopo katika uhifadhi wa taarifa, na kuongeza ufanisi na utendaji kazi wa washiriki:
"Mfumo huu ni muhimu kwa ufanisi wa kazi yetu na kwa ulinzi wa mazingira. Utatusaidia kutatua changamoto za zamani na kuongeza ufanisi katika kazi zetu za kila siku." Alisema Nafda
TAMWA Zanzibar imejizatiti kuhakikisha kuwa wanawake wanashirikishwa kikamilifu katika harakati za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Kwa kushirikiana na mradi wa ZanzAdapt, TAMWA inalenga kufikia malengo yake ya kuinua wanawake kiuchumi na kijamii, huku ikisisitiza umuhimu wa wanawake katika usimamizi wa mazingira na uongozi wa kijamii.
Kwa hiyo, kuanzishwa kwa mfumo huu wa kidijitali ni hatua muhimu katika kuleta mabadiliko chanya, na TAMWA Zanzibar iko tayari kushirikiana na washiriki mbalimbali katika kuhakikisha kuwa lengo kuu la mradi linatimia, na wanawake wanaweza kunufaika na maendeleo katika muktadha wa mazingira.
0 Comments