Katika enzi hii ya mageuzi ya kidijitali, ambapo taarifa inasafiri kwa kasi ya mwanga, swali moja linabaki: Je, mfumo wa kisheria wa Zanzibar unakwenda sambamba na mabadiliko haya?
Hili ndilo swali lililowaleta pamoja wanahabari wa Zanzibar katika mafunzo maalum ya sheria yaliyoongozwa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania Zanzibar (TAMWA ZNZ), wakiongozwa na Dk. Mzuri Issa.
Kwa zaidi ya miongo miwili, wanahabari wa Zanzibar wamekuwa wakililia sheria rafiki za habari, sheria zinazotambua na kuheshimu uhuru wa kujieleza huku zikiendana na maendeleo ya kisayansi na teknolojia. Kwa sasa, matumaini yao yamewekwa kwa Kamati ya Ufundi ya Taifa (NTC), ambayo mswada wa sheria mpya ya habari uko mikononi mwake.
Changamoto za Sheria za Zikizopo
Sheria ya Usajili wa Magazeti na Vitabu ya mwaka 1988, pamoja na marekebisho ya mwaka 1997, imeelezwa kuwa kandamizi na isiyoendana na wakati. Kwa mfano, kifungu cha 27(1) kinampa mamlaka afisa wa polisi kupekua na kukamata machapisho yoyote yanayoonekana kwenda kinyume na sheria.
Kwa mujibu wa mkufunzi wa mafunzo hayo, Bi Hawra Shamte, vifungu hivi havina nafasi katika karne ya 21 na vinahitaji kufutwa mara moja.
Matumaini na Mapendekezo
Afisa Programu wa TAMWA ZNZ, Zaina Mzee, amewataka wanahabari kuendelea na harakati za kutetea sheria rafiki za habari. Sheria hizi si tu zitahakikisha uhuru wa kujieleza bali pia zitaimarisha utoaji wa huduma za kijamii na maendeleo kwa ujumla.
Wanahabari waliopata mafunzo hayo, akiwemo Berema Nassor na Thuwaiba Habibu, wamependekeza mswada huo urejeshwe kwa wadau wa habari kabla ya kuidhinishwa, ili kuhakikisha changamoto zao za muda mrefu zinapatiwa ufumbuzi.
Kauli za Serikali
Waziri wa Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo, Tabia Maulid Mwita, amethibitisha kuwa mswada wa sheria mpya ya habari uko kwenye hatua za mwisho katika Kamati ya Ufundi ya Taifa.
Ameeleza dhamira ya kuwasilisha mswada huo kwenye Baraza la Wawakilishi hivi karibuni, hatua inayoweza kuwa mwanzo wa mageuzi makubwa katika sekta ya habari Zanzibar.
Kupatikana kwa sheria mpya ya habari Zanzibar ni tumaini jipya kwa wanahabari na taifa kwa ujumla.
Sheria hiyo inatarajiwa kuleta mwanga mpya wa uhuru wa habari, kuimarisha uwajibikaji, na kuchochea maendeleo endelevu.
Hata hivyo, safari bado ni ndefu, na juhudi za wanahabari na wadau wengine zinahitajika ili kuhakikisha sheria hiyo inawiana na mahitaji ya wakati.
Je, historia itaandika ushindi wa haki ya habari Zanzibar? Muda utasema.
0 Comments