Ticker

6/recent/ticker-posts

Wadau na Serikali kuendelea kusisitiza juu wasichana kushiriki Michezo



Na – Najjat Omar.

Katika miaka ya hivi karibuni, suala la ushiriki wa wasichana na wanawake katika michezo limekuwa likipata mwamko mkubwa visiwani Zanzibar. Hata hivyo, bado kuna changamoto za kijamii na kitamaduni zinazokwamisha maendeleo ya vipaji vya watoto wa kike kwenye michezo mbalimbali. Jamii imekuwa ikiweka vikwazo, ikihusisha michezo na dhana potofu kama uhuni, hali ambayo imechangia wasichana wengi kuacha kushiriki michezo wakiwa na umri mdogo.

Utafiti wa Shirika la Maendeleo la Ujerumani, uliofanywa Zanzibar mnamo Juni 2023, umebaini kuwa ukosefu wa uhamasishaji, mitazamo ya kidini, na dhana ya kwamba michezo ni kwa wavulana pekee bado ni vikwazo vikubwa vinavyorudisha nyuma wasichana. Licha ya changamoto hizi, kuna juhudi za makusudi kutoka kwa wadau wa michezo kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa ushiriki wa wasichana.

"Kwa sasa hamasa ni kubwa kwa jamii kuelewa kwamba watoto wa kike pia wanatakiwa kupata fursa ya kucheza michezo,"Amesema Hashimu Pondeza, Mkurugenzi wa Shirika la Jukwaa la Majadiliano la Vijana -CYD, alipohudhuria hafla ya kuadhimisha Siku ya Mtoto wa Kike mnamo Oktoba 20, 2024."Ndio maana mmeona wachezaji watoto wa kike hapa wanacheza wakiwa wamevaa hijabu na nguo ndefu, lakini wanashiriki michezo kama kawaida. Tunataka jamii ielewe kwamba michezo inawaongezea ujasiri, uelewa, na fursa mbalimbali za kimichezo."Amesema Hashim.

Katika hafla hiyo, walimu na wanafunzi kutoka shule sita za mjini na vijijini walikusanyika kusherehekea kwa kucheza mechi za mpira wa pete na maonesho ya kuonesha picha walizozichora zinahusu masuala ya ushirikishwaji wa michezo wa wasichana na wavulana za kuchora. Michezo hii ilikuwa njia mojawapo ya kuwaimarisha watoto wa kike kiakili na kimwili, huku ikiwapa nafasi ya kuonyesha uwezo wao.


"Naona kwamba michezo ni muhimu sana kwa watoto wa kike kwani inawachangamsha akili na kuwasaidia kufanya vizuri kwenye mitihani yao,"Amesema Bimkubwa Hemed, Mwalimu wa Sayansi kutoka Skuli ya Bububu huku akiongezea kuwa "Pia, michezo ni chanzo cha afya bora na inaweza kuwapatia fursa za ajira, kwani wapo watu waliopata ajira kupitia michezo tu."Alihitimisha mazungumza Biubwa.

Utafiti wa Women’s Sport Foundation nchini Marekani unaonyesha kuwa wasichana wengi huacha kushiriki michezo wanapofikia umri wa miaka 14, tofauti na wavulana ambao huendelea. Sababu kuu inayotajwa ni ukosefu wa hamasa na msaada kutoka kwa familia. Hii ni hali ambayo imekuwa ikishuhudiwa pia Zanzibar, ambapo wasichana wengi wanajikuta wakihofia kuhukumiwa, kupoteza ujasiri, au kukosa usalama wa kushiriki michezo.

Kwa upande mwingine, baadhi ya wasichana wanaofanikiwa kuvuka vikwazo hivi wamekuwa wakipata mafanikio makubwa na kuhamasisha wenzao kushiriki. Salama Omar, mwanafunzi wa Skuli ya Sekondari Kianga aliyeshiriki kwenye mechi hizo, amesema kuwa ana ndoto za kuwa kiongozi katika michezo."Jamii inanichukulia vizuri na mama yangu ananiunga mkono. Natamani kuwa Rais wa Klabu ya Michezo ili niweze kusaidia wasichana wengine kuingia kwenye michezo," Amesema kwa matumaini Salama. 

Juhudi za kuhakikisha ushiriki wa wasichana katika michezo pia zinaungwa mkono na viongozi wa kitaifa. Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Anna Athanas Paul,aliweka wazi dhamira ya serikali kusaidia kukabiliana na changamoto zinazoikumba jamii ya watoto wa kike."Tuko hapa leo kusherehekea, lakini pia kutambua changamoto ambazo watoto wa kike wanakabiliana nazo duniani kote. Tunajidhatiti kujenga mustakabali ambapo kila mtoto wa kike anaweza kukuwa, kustawi, na kuwa kiongozi,"Amesema Anna wakati wa hafla hiyo.

Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) yakisisitiza usawa wa kijinsia, lengo namba tano likiwa na nia ya kuwawezesha wanawake na wasichana wote, ni wazi kwamba juhudi za kuwawezesha watoto wa kike kushiriki michezo ni hatua muhimu kuelekea usawa huo. Khairat Haji, Afisa Program kutoka TAMWA -Z, amesisitiza kwamba ni muhimu jamii kubadilika na kuona kwamba michezo ni haki ya kila mtoto, bila kujali jinsia.”Tunasherehekea sikku hii ya mtoto wa kike kwa kuzingatia suala la usawa na kuona kila mtoto ana haki kushiriki kwenye michezo bila ya ubaguzi wowote” Amesema Khairat akifungua shughuli hio.

Siku ya Mtoto wa Kike Duniani huadhimishwa kila mwaka tarehe 11 Oktoba. Siku hii ilianzishwa na Umoja wa Mataifa mwaka 2012,huku wadau wakiutambua mwezi wa Oktoba ukiwa mwezi wa kusheherekea mafanikio na hatua za mtoto wa kike duniani.

Post a Comment

0 Comments