Ticker

6/recent/ticker-posts

Viunzi Virefu Vya Kuruka Vinavyowakamisha Wanawake Kuwa Viongozi

Muwakilishi wa Jimbo la Mahonda kwa Tiketi ya Chama Cha Mapinduzi Mhe. Asha Abdalla Mussa akiapa kuwatumikia wananchi wa jimbo la Mahonda mbele ya Spika wa baraza la wawakilishi Zubeir Ali Maulid


Na Ahmed Abdulla:

Zanzibar:Uongozi ni eneo ambalo  limekuwa na muamko mkubwa huku suala la  usawa wa kijinsia hasa katika nafasi mbali mbali za uongozi likisemwa mara nyingi ,licha  ya mafaniko kadhaa yaliyopatikana lakini bado wanawake wanaona kuna viunzi virefu vya kuwafikisha kwenye safari ya wao kuwa viongozi.

“Hali ilivyokuwa”

Takwimu za Tume ya Uchaguzi Zanzibar Uchaguzi wa mwaka 2020  Zanzibar katika nafasi ya uwakilishi waliogombea nafasi hiyo wanaume walikuwa ni 190 wanawake walikuwa 61 ambapo walioshinda  kwa upande wa wanaume ni 42 huku wanawake wakiwa ni 8.

Kwa upande wa nafasi za udiwani waliogombea nafasi hiyo wanawawake walikuwa ni 74, wanaume walikuwa ni 276 lakini walioshinda  wanawake walikuwa ni 25 nawanaume walikuwa ni 85.

Katika nafasi ya ubunge waliogombea nafasi hiyo wanaume walikuwa ni 257 na wanawake walikuwa 81 walioshinda katika nafasi hiyo wanaume ni 46  na wanawake 4.



“Nipe nikupe”

Msemo wa Kiswahili unaobeba maana ya rushwa ya ngono hii pia ipo kwenye masuala ya uongozi.

Asha Abdalla Mussa ni Muwakilishi wa Jimbo la Mahonda amesema wakati mwengine mwanamke anarudi nyuma kwenye kugombea nafasi mbalimbali kutokana na vishawishi vingi vikimuhitaji kutoa rushwa ya ngono ili apate nafasi hiyo.

“Licha ya vishawishi vingi lakini nilisimamia msimamo wangu wa kupambana kwa uwezo ili kushika nafasi hii” Amesema Asha huku akitaja kikwazo kingine kuwa ni “Mfumo dume na kukatishwa tamaa kwa kuchafuliwa katika baadhi ya mazingira navyo nilikutana navyo lakini havikunirudisha nyuma bali nilisonga mbele na nikashinda na najivunia kuwa hapa kama kiongozi mwanamke“ Ameiomgezea Asha kwa sauti ya Uthubutu.

Halima Ibrahim  ni Mjumbe wa Kikosi kazi cha Ngome ya Wanawake amesema  wanawake wengi hukutana na changamoto ya rushwa ya ngono jamba ambalo  huwafanya wao kushindwa njiani na badala yake nafasi hushika wanaume“Rushwa ya ngono ni jambo kubwa linawakuta wanawake wanataka kuwa viongozi hili linawatesa na kuwaumiza wanawake sana “Amesema Halima.

“Wanawake hawawezi”

Mfumo dume nao ni miongoni mwa vizingiti vinavyowakabili wanawake katika kutafuta nafasi za uongozi licha ya kuwepo jitihada mbalimbali zinazochukuliwa na Taasisi binafsi lakini bado inaonekaka kuwa hilo ni tatizo ambalo  halijapata muarubaini wake.

Ashraf Saleh Zungo ni Katibu wa Chama Cha Mapinduzi CCM Wilaya ya Kaskazini B amesema bado katika jamii kuna ukandamizaji wa mwanamke kuanzia ngazi za familia

“Mitazamo hii inawachukulia wanawake kuwa hawafai kushika nafas za uongozi wao ni kuolewa ,kuzaa na kulea” Amesema Ashraf kwa kuongeza kuwa “Kipaumbele chao kama CCM ni kutoa fursa mbalimbali kwa wanawake ili waweze kufikia malengo yao ya kutafuta nafasi za uongozi katika ushiriki wao ndani ya chama hicho” Amemaliza.

“Isemavyo Sera”

Sera ya Jinsia ya Zanzibar mwaka 2014 namba 4.1 ushiriki wa wanawake katika vyombo vya utoaji maamuzi  katika ngazi zote ni mdogo hivyo Serikali  kwa kushirikiana  na wadau wengine  watachukuwa juhudi za maksudi kuona ushiriki  na ushirikishwaji  wa makundi yote wanawake na wanaume katika ngazi za maamuzi, huku mikakati ya kisera itafanyika ikiwa ni pamoja na kuinua usawa wa kijinsia  kwa kufanya juhudi za maksudi za kuongeza idadi ya wanawake  katika nafasi za uongozi  katika sekta mbalimbali.

“Woga unaturudisha”

Mkitu Suleiman ni mwanachama wa Chama Cha Mapinduzi –CCM   Mkitu  mkaazi MjiMwema Mwera amesema kuwa miongoni mwa vikwazo ambavyo wanawake hushindwa kufikia nafasi za uongozi ni kutokujiamini  katika kutafuta nafasi za uongozi hii lakini hofu na woga walionao hushindwa kufika nafasi hiyo.

“Asili ya mwanamke ni kuwa na uwezo mkubwa wa kiutendaji lakini akitawaliwa na woga na hofu hushindwa kufikia nafasi za uongozi na kujitokeza mbele kwenye masuala ya uongozi” Amesema Mkitu.

Kwa upande wa mwanachama wa chama cha ACT-WAZALENDO Rehema Abdalla mkaazi wa Bububu amesema “Upendeleo wa kijinsia na ubaguzi ni miongoni na vikwazo tunapojaribu kutafuta nafasi za uongozi lazima utavikuta wa watu ambao tunawategemea”Ametoa maoni yake Rehema

“Wadau wataka haya”

Dkt Mzuri Issa ni Mkurugenzi  Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania upande wa Zanzibar TAMWA-ZNZ  amesema  wanawake wanakabiliwa na mambo mengi lakini kubwa zaidi linaloathiri ni rushwa ya ngono hivyo chama hicho kipo mstari wa mbele katika kuhakikisha wanawake wanaondokana na changamoto mbalimbali ambazo huwasababisha kukosa kupata nafasi za uongozi.

"Tunatoa elimu tunawafikia na kuhakikisha tunaona mabadiliko kwenye wao kujitokeza na kuwa na uthubutu na kupunguza woga”

Huku akiomba kuwa suala la utekelezaji wa Sera jinsia ya Zanzibar ikitekelezwa ipasavyo basi wanawake watapata fursa sawa na wanaume katika nafasi za uongozi

Mkurugenzi wa Tasisi ya Kupambana na Changamoto za Vijana Zanzibar- ZAFAYCO Abdallah Abeid amesema wanawake wengi  wana majukumu ya nyumbani na familia ambapo wanabeba mzigo mikubwa wa majukumu hayo  jambo ambalo linaweza  kuwazuia  kutumia muda wao  kikamilifu  kwa ajili ya kazi zao au maendeleo  ya kitaaluma.

“Katika mazingira mengi  wanawake wanatarajiwa  kusimamia familia  na kazi za nyumbani  huku wanaume  wakipewa nafasi  zaidi  ya kufuatilia  malengo yao ya uongozi, hali hii  ya kutokuwa na usawa wa mgawanyo wa  majukumu ya nyumbani  inachangia   wanawake kukosa muda  wa kujitosa  katika masuala ya uongozi”

Abdallah amezitaka familia kuangalia suala la malezi lisiwe na athari za kuwarudisha nyuma wanawake kuwa viongozi.


 


 



Post a Comment

0 Comments