Ticker

6/recent/ticker-posts

Wakulima Wa Mradi Wa Viungo Wakabidhiwa Vifaa

 


Na Nafda Hindi

 Wakulima wanaojishughulisha na kilimo cha  mboga mboga, matunda na viungo kupitia  MRADI wa  VIUNGO (AGRI-CONNECT)  wamekabidhiwa vifaa vitakavyowasaidia kuongeza nguvu katika uzalishaji wa bidhaa bora zitakazokidhi masoko.

Akizungumza katika hafla ya kukabidhi vifaa hivyo iliofanyika katika jengo la Kificho Mwanakwerekwe Meneja Mkuu wa mradi huo Simon Makobe alisema  vifaa hivyo vitatumika kusaidia kuongeza uzalishaji na kufikia malengo ya utekelezaji wa mradi huo.

Alisema MRADI wa VIUNGO ulilenga mambo mbalimbali ikiwemo kufungua fursa na kuongeza mnyororo wa thamani ya mazao hapa Zanzibar pamoja na kupatiwa vifaa kwa lengo la kuwawezesha wakulima kuwa na nyenzo muhimu ili kulima kilimo bora kitakachowasaidia kujikwamua kiuchumi,”alisema.

 “Ugawaji wa vifaa hivyo ni moja ya mikakati ya utekelezaji wa mradi huo pamoja na kutumia ujuzi mulioupata juu ya matumizi ya teknolojia muliyojifunza kipindi chote cha utekelezaji wake,” alisema Makobe.

Alifahamisha kuwa lengo la mradi huo ni kuleta mabadiliko makubwa ya kiuchumi kwa wakulima na taifa hivyo kupitia hatua hiyo itasaidia kufikia malengo hayo.

Sambamba na hayo aliwataka wakulima walionufaika na vifaa hivyo kufuata maelekezo ya matumizi ya vifaa hivyo ili viweze kuleta tija kwenye shughuli zao za kilimo.

Kwa upande wake Meneja tathmini na ufatiliaji wa mradi huo Ali Abdalla Mbarouk alisema kukabidhiwa kwa vifaa hivyo itasaidia kuimarisha ustawi wa shughuli zao kwa kuondosha changamoto zilizokuwa zikijitokeza baina ya viongozi wa mradi huo na wakulima.

“Tulitegemea vifaa hivi vitolewe  kipindi cha utekelezaji wa mradi kwa bahati mbaya sasa mradi umemaliza ila tulikabiliwa na changamoto ya fedha kidogo,”Mbarouk alisema.

Mratibu wa mradi huo kutoka Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo Zanzibar Mashavu Said Sukwa alisema mradi huo pamoja na changamoto za hapa na pale zilizojitokeza katika utekelezaji wake lakini umeweza kuleta tija kwa wakulima kwa kupata elimu ya kuongeza uzalishaji na kuzalisha bidhaa bora.

Alisema endapo wakulima hao wakishindwa kuvitumia vifaa hivyo ni vyema kuvirudisha serikali na sio kufanya wanavotaka wao kwani kufanya hivyo ni kwenda kinyume na malengo ya matumizi ya vifaa hivyo na kutawasababisha kuingia katika matatizo.

“ Wakulima tunawaomba  kuvitunza vifaa hivyo na kuvitumia kwa mujibu wa matumizi yaliopangwa na si vinginevyo, mukenda kinyume na hayo kwa mujibu wa Sheria mutafanya kosa na kuingia hatiani,” Mashavu alisema.

 Kwa upande wa Ofisa elimu kutoka Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu wa Uchumi Zanzibar (ZAECA) Saumu Ramadhan Haji alisema watafatilia kwa karibu matumizi ya vifaa bivyo ili kuondosha ubabaifu unaofanywa na baadhi ya wakulima kwa kuvitumia kinyume na malengo ya vifaa wanavokabidhiwa.

Sheria ya ZAECA No 5, (2023), kifungu No 53 kinaeleza juu ya matumizi mabaya ya Umma, pindipo utatumia vibaya mali ya Umma utaingia hatiani na adhabu yake ni shilingi milioni 10 za Kitanzania, au utafungwa jela kifungo cha miaka 5 au vyote kwapamoja.



Kwa upande wa wakulima hao walishukuru kupatiwa vifaa hivyo na kuahidi kuvitumia kama walivyoelekezwa ili kwenda sambamba na malengo husika ya mradi.

 Walisema vifaa hivyo vitasaidia kuongeza kasi ya uzalishaji wa kilimo chao kutokana na kikwazo kikubwa kilikuwa ni kukosa nyenzo za kisasa za kuendeleza kwa shughuli zao hivyo kupitia hatua hiyo wataweza kufikia malengo yao.

Jumla ya wakulima 31 walikabidhiwa vifaa mbalimbali  vya kilimo na watatu (3) fedha taslimu ikiwemo matenki ya maji, mashine za kuvutia maji, mipira ya kusambazia maji na vifaa vingine kwa ajili ya kuendeleza shughuli zao za kilimo.

Mradi wa VIUNGO ulioanza mwaka 2020-2024 ni mradi wa miaka minne (4) uliomaliza mda wake, uliwafikia wakulima wapatao elfu hamsini na saba, mia tisa na sabiini na nne hapa Zanzibar kwa Wilaya tisa (9), tano (5) Unguja na nne (4) Pemba ambao  ulitekelezwa kwa pamoja na TAMWA,  People Developmend Forum (PDF) na Community Forest in Pemba (CFP)  kwa kushirikiana na Jumuiya ya Umoja wa Ulaya.

 

 

Post a Comment

0 Comments