Mkurugenzi wa Taasisi ya Panje Zanizbar Muhammad Said |
SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar inatarajia kuanzisha mpango maalum wa kuzuia matukio ya kuzama hapa nchini.
Mpango huo utakaoshirikisha wadau mbalimbali watakaoweza kukaa pamoja na kuweka mikakati madhubuti itakayosaidia kuongeza uelewa kwa jamii ili kujikinga na matukio hayo na kubakia salama.
Ofisa Kiungo wa Masuala ya Kupinga Kuzama kutoka Kamisheni ya Kukabiliana na maafa Zanzibar, Saleh Abdalla Mohammed, alisema hayo alipokuwa katika kikao cha pamoja na wadau mbalimbali wa kukabiliana na masuala ya kuzama hapa nchini ikiwa ni moja ya kuelekea maadhimisho ya siku ya kuzama duniani.
Alisema Zanzibar ni kisiwa kilichozungukwa na bahari ambapo shughuli nyingi za wananchi ikiwemo za kiuchumi, usafiri na mambo mengine yanatumika katika maeneo hayo, hivyo kunahatari kubwa ya kukutwa na matukio ya kuzama na kupoteza maisha au mali zao.
Sambamba na hayo alisema kamishen hiyo kwa kushirikiana na wadau hao wameona kuna kila sababu hivisasa kuwa na mpango huo kutokana na kuwepo kwa idadi kubwa ya wananchi kupoteza maisha katika maeneo ya maji.
Ofisa huyo alisema kupitia hatua hiyo itasaidia kujenga uelewa kwa jamii na kujikinga na matukio mbalimbali ili kuweka ustawi mzuri wa maisha yao na mali zao.
Mapema Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa wa Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar Muhidin Ali Muhidin alisema lengo la kikao hicho na wadau mbalimbali ili kuongeza uelewa kwa jamii juu ya kujilinda na matukio hayo ambayo yanaendelea kutokea kila siku katika mazingira wanayoishi na kwenye shughuli zao za kiuchumi.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Taasisi ya Panje Zanizbar Muhammad Said alisema licha ya taasisi yao kujikita zaidi juu ya kutoa elimu inayohusisana na masuala ya usalama kwenye maji kujua kuogelea na kujiokoa lakini bado nguvu za pamoja zinahitajika ili kuongeza uelewa unaongezeka kwa jamii juu ya kujikinga na matukio hayo kama ilivyo katika matukio mengine.
Washiriki wa mafunzo hayo walisema Zanzibar hivisasa inatekeleza sera ya uchumi wa buluu ambapo eneo hilo linakusanya idadi kubwa ya wananchi katika kuendeleza shughuli za kiuchumi hivyo mikakati na elimu zaidi inahitajika ili kuona watu hao wanakuwa salama wakati wote wanapokuwa katika harakati zao.
Siku ya kuzuia kuzama duniani hufanyika kila mwaka ifikapo Julai 25 ikiwa na lengo la kuongeza uelewa kwa jamii ili kujiweka salama na kujikinga na matukio hayo.
0 Comments