Makamu
wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Mhe. Othman Massoud Othman amevitaka vikundi vya
mazoezi nchini kuweka kanuni na miongozo ya maadili ambayo itasaidia kuondoa
mitizamo hasi kwa jamii juu ya ushiriki wa makundi yote katika vikundi vya
mazoezi na michezo.
Ametoa wito huo wakati
akizungumza na vikundi vya mazoezi katika halfa ya kuhamasisha ushiriki wa
jinsia zote kwenye mazoezi na michezo ikiwa ni maadhimisho ya kutimia
miaka kumi ya klabu ya mazoezi Gombani kisiwani Pemba.
Alisema, kuwepo kwa kanuni
zinazosimamia maadili katika mazoezi na michezo kutasaidia watu wengi hasa
wanawake kuona eneo hilo ni salama kwao na kuondoa dhana potofu iliyojengeka
katika jamii.
Alieleza, "niwaombe tuweke
kanuni za kusiamamia maadili zitakazo ondoa dhana potofu kwa jamii ili tuweze
kuwavutia watu wengi kushiriki mazoezi kwasababu hili jambo ni jema
zaidi."
Aidha, makamu huyo wa kwanza wa
Rais ambaye aliongoza matembezi na mazoezi ya wanamichezo hao alifahamisha kuwa
taifa linapata hasara kubwa kugharamia matibabu ya maradhi yasiyoambukiza
yanayosababishwa na mfumo wa maisha ambapo iwapo jamii itakuwa na mwamko wa
kushiriki katika mazoezi na michezo itasaidia kupunguza gharama hizo.
"Jambo hili ambalo
mnaliendeleza kwetu sisi wengine linatupa faraja sana kwasababu tunajua
mnafanya jambo kubwa kwa jamii na nchi yetu kwani kama kuna jambo ambalo nchi
inapata hasara ni kwenye matibabu. Na matibabu ya maradhi yasiyoambukiza
kwahakika ni ya ghali sana na nyinyi nyote ni mashahidi," alieleza, Mhe.
Othman Masoud.
Katika hatua nyingine alihimiza
jamii kupewa elimu ya matumizi lishe ili kujiepusha na ulaji holela unaopelekea
athari kiafya.
Mhe. Othman Masoud alisema,
“twende mbali zaidi kutoa ya elimu ya lishe kwa jamii. Kwasababu hili wengi
bado huko tuna tatizo. Tumeacha sasahivi vyakula asilia. Mwingine anaona
pengine vyakula asilia sio usasa. Lazima twende katika hatua ya kujitunza na kujipenda
kwa kutambua kipi kibaya na kipi kizuri cha kula.”
Naye Mkuu wa wilaya ya Chake
chake, Abdalla Rashid amemshukuru Mhe. Othman kwa kuwa miongoni mwa washiriki
katika bonanza hilo na kuwahimiza wananchi kuhakikisha kwamba wanahamasishana
ili wajenge utamaduni wa kufanya mazoezi katika kujiepusha na maradhi
mbalimbali yasiyoambukiza.
Akitoa salamu za wadau, afisa
programu ya michezo kwa maendeleo kutoka Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake
Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ), Khairat Haji alieleza bado kuna changamoto
kwenye jamii ya uelewa kuhusu umuhimu wa mazoezi na kupelekea vikwazo kwa
makundi yote hasa wanawake kushiriki kikamilifu katika mazoezi na michezo.
Aidha aliongeza, ukosefu wa
miundombinu na vifaa wezeshi vya mazoezi ni kikwazo katika ufikiaji wa usawa wa
kijinsia kkwenye michezo na kuomba serikali na wadau kusaidia kuboresha
miundombinu hiyo ili kuwezesha kila mmoja kushiriki bila kikwazo.
"Kuna changamoto kadhaa
ambazo tumeziona ikiwemo ukosefu wa vifaa na miundombinu wezeshi kwaajili ya
makundi yote kushiriki katika michezo mbalimbali," alifahamisha afisa
huyo.
Kwa upande wake mwenyekiti wa
klabu ya mazoezi Gombani, Hamad Malengo aliomba wadau kuungana pamoja kushiriki
katika michezo na mazoezi ili kuondoa dhana hiyo potofu iliyojengeka katika
jamii kuwa kushiriki michezo ni kujifunza uhuni.
Alisema, "elimu kwa jamii
inahitajika zaidi ili kutoa mwamko wa watu kushiriki kwenye mazoezi na kuachana
na dhana kwamba michezo ni uhuni. Ni lazima tusimame pamoja ili kila mmoja wetu
aweze kushiriki mazoezi kwaajili ya afya yake.”
Hafla hiyo ya kuhamasisha
ushiriki wa jinsia zote kwenye mazoezi na michezo ikiwa ni maadhimisho ya
kutimia miaka kumi ya klabu ya mazoezi Gombani kisiwani Pemba iliyoandaliwa kwa
kushirikiana na TAMWA-ZNZ na Shirika ka Bima la Zanzibar imevishirikisha
vilabu zaidi ya vitano vya mazoezi kutoka Unguja, Tanga na wenyeji Pemba.
0 Comments