Ticker

6/recent/ticker-posts

FAWE Yagawa Vifaa Vya Skuli Kwa Wanafunzi Wenye Uhitaji Tumbatu Uvivini

Mjumbe wa Bodi FAWE, Sabrina Omar Abdulla Akimkabidhi vifaa vya Skuli Mmoja wa Wanafunzi wa Skuli ya msingi Tumbatu Uvivini


Na Ahmed Abdulla, Zanzibar:

SHIRIKA la Kuwawezesha Wanawake Kielimu na Kiuchumi Zanzibar (FAWE) limesema litaendelea kuunga mkono adhima ya serikali katika kuhakikisha wanafunzi wanapa elimu katika mazingira mazuri.

Mjumbe wa Bodi ya FAWE Sabrina Omar Abdulla alisema hayo alipokuwa katika hafla fupi ya kukabidhi vifaa vya skuli kwa wanafunzi wenye mazingira magumunwa ngazi ya msingi na sekondari wa skuli ya Tumbatu Uvivini.

Alisema kundi kubwa la wanafunzi hususani wa vijijini hali zao duni hivyo kupitia hatua hiyo itawasaidia kupata elimu bora kwa maslahi yao ya badae.

Alisema wanafunzi wanapopata mahitaji yao kwa wakati huwasaidia kuwa imara na kupata faraja hatua ambayo huwawezesha kusoma kwa bidii na kufanya vizuri katika masoomo yao na kuiletea nchi maendeleo kupitia nyanja mbalimbali.



Sabrina alisema kabla ya kutoa msaada huo walifanya utafiti na kuona mahitaji ya watoto hao hivyo hatua hiyo itawawezesha wanafunzi hao kupata elimu bora na kutimiza ndoto zao.

Alisema taasisi hiyo pamoja na mambo mengine lakini pia malengo yake ni kuhakikisha kwamba inasaidia watoto hao ili kupata haki zao za msingi ikiwemo elimu hivyo wanaamini kwamba sadaka hiyo itawafariji na kusoma vizuri kama wanafunzi wengine.

Hivyo alitumia fursa hiyo kuwaomba watu wenyeuwezo kutoa sadaka na kuwasaidia watoto hao kwasababu mahitaji yao makubwa.   

Nae Sheha wa Shehia ya Tumbatu Uvivini Ngwali Sheha Haji aliwataka wazazi na wadau wengine wa elimu kuunga mkono jitihada zinazochukuliwa katika kuimarisha upatikanaji wa elimu ili kuhakikisha wanafunzi wanakuwa katika mazingira mazuri ya kujisomea.

Alisema hatua iliyochukuliwa na taasisi hiyo ya kuwekeza katika sekta ya elimu ni yakupigiwa mfano kwasababu itasaidia wanafunzi kuwaweka katika mazingira rafiki ya kujisomea.

“Katika shehia yangu kunawananchi wanaishi kwa mazingira tofauti wengine hali zao duni za kipato na wengine mayatima hivyo hupitia wakati mgumu kutokana na kushindwa kumudu sare za skuli lakini kupatiwa msaada huu utawapa moyo na ari ya kuendelea vyema na masomo yao,”alisema.

Mbali na hayo aliwataka wazazi na walezi kuutunza msaada huo waliokabidhiwa ili kuona watoto hao wanasoma katika mazingira mazuri.

Kwa upande wake Msaidizi Mwalimu Mkuu wa Skuli hiyo Majaliwa Khamis Juma alisema sare ni nyenzo muhimu za kujifunzia hivyo hatua hiyo itawafanya wanafunzi hao kujiamini katika masomo yao.



Alisema taasisi hiyo haikukurupuka kupeleka msaada huo lakini imeamua kufanya hivyo kutokana na uhalisia wa maisha duni ya watoto hao.

“Kunabaadhi ya wanafunzi tunawavumilia huja skuli na nguo za nyumbani na wengine hukatisha masomo kutokana na kukosa mazingira rafiki ya kujisomea ikiwemo yunifomu hivyo sadaka hii itawawezesha kufikia malengo yao,”alisema.

Alifahamisha kuwa jitihada zilizofanywa na taasisi hiyo za kuiunga mkono jitihada za serikali za kuwekeza katika sekta ya elimu ili kuongeza kiwango cha ufaulu na kufikia malengo ya kuwa na taifa bora la wasomi.

Baadhi ya wanafunzi waliokabidhiwa msaada huo walishukuru fawe kwa hatua hiyo kwani itawasaidia kwenda skuli wakiwa katika mazingira mazuri na kutumia muda huo kuahidi kusoma kwa bidii ili kufikia malengo yao.

Zaidi ya wanafunzi 52 waliyopo katika mazingira magumu wa msingi na sekondari kutoka skuli hiyo walikabidhiwa msaada wa sare za skuli ikiwemo mkoba, viatu, unifomu na vitu vingine kutoka kwa taasisi ya FAWE.

Post a Comment

0 Comments