Ticker

6/recent/ticker-posts

Wajasiriamali Wanwake Watakiwa Kuchukua Nafasi Za Uongozi Kwenye Vikundi Na Vyama


NA ASIA MWALIM

USHIRIKA wa kikundi cha wanawake wanaolima mwani "Ukweli nia safi" Umewataka wanawake wa vikundi mbali mbali kujitoa kikamilifu ili kushiriki vyema katika nafasi za uongozi wa vikundi na vyama vyao.

Walisema wanawake wanaweza kugombea nafasi za uongozi sehemu tofauti kwani wao ndio watatuzi wakubwa wa shida za wanawake wenzao na jamii iliyowazunguka.

Katibu wa ushirika huo, Safia Hashim Bakari, (52) alitoa wito huo wakati akifanya mahujiano na gaazeti hili, huko kijiji cha Bweleo, wilaya ya Magharibi B Unguja.

Alisema katika kikundi chao wamejikusanya wanawake pamoja na wanajishughulisha na kilimo cha mwani ambao unawasaidia katika mambo mbali mbali ya maendeleo.

"Katika kikundi chetu tupo wanawake watupu na tunajiongoza wenyewe bila ya usaidizi wa mwanamme kwani uwezo tunao" alisema

Mbali na uongozi wa kikundi chao kuwa mzuri alisema, wanakabiliwa na changamoto ya kukosa mitaji ya kununua vifaa vya Kielektroniki kwa ajili ya shuguli zao za vikundi na nafasi nyengine za uongozi.

Wakizungumzia suala la mikopo ya uviko 19 iliyotengwa kwa ajili ya wajasiriamali wanawake alisema mikopo imewakatisha tamaa wajasirimali wanawake, kwani hawana uhakika wa kupatiwa.

Wanawake wa kikundi hicho, walisema awali walieka imani ya kupata mkopo wa Uviko 19, kutokana na kutangazwa kutolewa kwa wajasirimali, lakini matokeo wanayopata ni tofauti na mategemeo ya wajasirimali.

"Wajasirimali wengi tulifurahishwa na kauli za Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi,  alipokua akizungumza na sisi lakini sijui kama tutafanikiwa"  alisema.

Mshika fedha wa kikundi hicho,  Aisha Bakar , alisema tayari wamekamilisha tararibu zote, ikwemo kufungua akaunti, kusajili kikundi chao na kufikisha barua zao wilayani, ili kupatiwa mkopo.

Alieleza matarajio yao baada ya kupata mkopo wa shilingi milioni 12, ni kununua mashine ya kukatia sabuni ili kuendeleza shughuli zao na kusaidia jamii iliyowazunguka.

"Kwa kua kikundi chetu kinaongozwa na wanawake hatuoni sababu ya kunyimwa, kwani familia zetu zinatutegemea kwa hali na mali" alisema.

Wajumbe wa kikundi hicho, walisema kwa muda mrefu wanafanya shughuli za utengenezaji sabuni kutumia vibati vya mkono, tayari wamepatiwa mafunzo kuhusu fedha hizo, wanatarajia kununua mashine kupitia mkopo huo ili kuimarisha vipato vya wanawake.

Katibu Tawala Wilaya ya Magharibi B, Sahim Haroun Haji, alisema tatizo la kucheleweshwa fedha za mikopo kufika kwa wajasirimali ni kutokana na utaratibu wa kibenki kuchukua muda mrefu ili kujiridhisha wahusika wanaotaka mikopo.

Alieleza kuwa wilaya inatekeleza wajibu wake kwa kutoa muongozo namna ya kupatiwa usajili, ni vyema viongozi wa vikundi na wanawake kuwa mstari wa mbele kufatilia kwani ni utaratibu unaohitaji muda.

Afisa Mikopo wilaya ya Magharibi B,  Safia Khamis alisema changamoto kubwa inayojitokeza ni kushindwa kujaza fomu kwa usahihi, na kugundua baadhi ya vikundi sio waaminifu.

Kaimu Meneja wa Benki ya CRDB, tawi la Zanzibar, Mamertus Luena, alisema benki hiyo inatoa mikopo kwa kuzingatia vigezo vilivyowekwa na serikali.

Alisema sababu ya kucheleweshwa mikopo kwa baadhi ya wajasirimali ni kukosa vigezo, kulingana na viwango vikubwa wanavyohitaji ambavyo haikidhi kulingana na biashara zao.

Post a Comment

0 Comments