Na Ahmed Abdulla, Zanzibar:
Wanawake wametakiwa kujiamini na kuwa na misimamo
imara yenye lengo la kuleta mabadiliko katika nchi.
Hayo yamesemwa na Dk Mzuri Issa Ali wakati akizungumza
na wanawake wenye kutia nia kugombea nafasi za Uongozi kutoka vyama mbali mbali
vya siasa katika hafla iliofanyika huko Tunguu Wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini
Unguja.
Dk Mzuri amesema wanawake wasirudi nyuma na kubabaisha
na maneno ya baadhi ya watu wasiopenda maendeleo ya wanawake kwa kuwakatisha
tama na kuwaekea vikwazo mbali mbali ili wasiweze kutimiza adhma yao hiyo.
Amesema utafiti uliofanywa kisayansi wanawake wana
uwezo wa kufanya mambo mengi kwa wakati mmoja ukilinganisha na wanawake hivyo
wanawake waitumie fursa hiyo ili kufikia malengo yao.
“Mwanamke anaweza kuwa mke,mama,kiongozi na wakati huo
huo pirika za nyumbani zinamsubiri kama vile kulea watoto huku akiwa anafuwa
nguo,anachota maji,anapika na kazi zote hizo anazifanya kwa wakati mmoja
tofauti na mwanamme yeye akiwa anasoma gazeti hata kumsemesha hakujibu kwake
inakuwa ni shida,” Dk Mzuri.
Naye Mwakilishi mstaafu wa Jimbo la Magomeni Bi Hafsa
Said amesema katika kupigania nafasi ya Uongozi alikutana na vikwazo mbali
mbali lakini si jambo ambalo lilimkatisha tama bali alipambana na hatimae
kushika nafasi hiyo kwa kipindi cha miaka kumi.
Bi Hafsa amesema jambo ambalo lilimfanya kudumu katika
nafasi hiyo kwa kipindi chote hicho ni kujiuamini ,kujiheshimu pamoja na
mashirikiano na wananchi bila kujali rangi, dini, kabila wala kujali itikadi
zao za kisiasa bali alihudumia watu wa aina zote.
“Mimi sikujali watu wa chama changu tu kwa sababu hata
wananchi wa chama cha upinzani walinipigia kura kwa hiyo wote ni wananchi wangu
na maendeleo niliyaleta kwa wote, na nikauunda kamati ya sheha nikashirikisha watu
wa chama changu cha CCM na chama cha Upinzani tukafanya kazi” Bi Hapsa.
Nae Kiongozi wa Dini ya Kiislam Ukhti Amina Salum
Khalfan amesema dini ya kiislam haijakataza mwanamke kuwa kiongozi bali baadhi
ya watu hutumia kipengele cha dini kwa lengo la kuwakandamiza wanawake kwa
malengo yao binafsi.
“Aya ya mwanzo katika kitabu kitukufu cha (Qur an) ilimfikia Bibi Khadija ambae alikuwa mke
wa bwana Mtume Muhammad (S.A.W) kama vile Suratul Mujadila na Nnisai ni mfano
dhahir uliotumika kuonesha mwanamke ni kiongozi , hata masahaba waliambiwa wachukuwe
Elimu(kusoma) kwa bibi Aysha (R.A.), Siasa isiwe sababu ya kunyoosheana vidole
“, Ukhti Amina.
Mapema mratibu
wa mradi wa kuinuwa wanawake katika harakati za Uongozi kutoka TAMWA,ZANZIBAR Maryama Ame Choum
amesema wametowa mafunzo kwa wanawake wapatao themanini kwa Unguja na Pemba
kutoka katika vyama vya siasa na wanafunzi kutoka vyuo vikuu , ambapo kupitia
mafunzo hayo wanatarajia wanawake wengi
Zanzibar watajitokeza kugombea nafasi za Uongozi katika Uchaguzi mkuu wa
October 2025.
Nao baadhi ya wanawake
watia nia ya kugombea nafasi za Uongozi
wamesema watasimama imara kuondosha hofu na kuhakikisha wanagombea
nafasi za Uongozi kuanzia jimbo hadi Taifa kwa lengo la kuleta mabadiliko
katika Taifa hili.
0 Comments