WAANDISHI
wa habari wametakiwa kupaza sauti zao kuwatetea wananchi kupitia vyombo vya
habari kwa maslahi ya kukuza uhuru wa habari na uhuru wa kujieleza ambao
utasaidia kuleta maendeleo ya haraka kwa taifa.
Uhuru huo unaweza kupatikana endapo kutakuwa na
sheria rafiki za habari sambamba na waandishi wenyewe kufanya kazi kwa kufuata
maadili ya tasnia yao na kuendeleza jukumu la huleta maendeleo kutokana
na kuwa kiungo cha kupaza sauti kwa wasio na sauti .
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Chama cha
Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania Zanzibar (TAMWA-ZNZ) Dkt Mzuri Issa
Ali wakati wa mafunzo ya siku moja ya kupitia Mikataba ya kikanda na ya
Kimataifa na kujadili mapungufu ya sheria zinazokwamisha uhuru wa habari
Zanzibar.
Ameeleza kuwa lengo la mafunzo hayo
yaliyowakutanisha watendaji wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Vijana
na Michezo , Tume ya kurekebisha Sheria Zanzibar, Tume ya Utangazaji na
waandishi wa habari ni kukumbushana umuhimu wa kuangalia ni kwa kiasi gani kama
nchi imeweza kuzingatia mikataba hiyo ili kupata sheria na sera bora
zitakazo simamia masuala ya haki ya kupata habari na kutoa maoni na
kukuza demokrasia nchini .
Aidha amebainisha kuwa pamoja na kuridhia
Mikataba ya bado sauti za wananchi hazipewi kipau mbele kusikika katika
vyombo vya habari ukilinganisha na sauti za viongozi jambo ambalo linawanyima
wananchi haki yao ya kikatiba ya kutoa maoni.
Miongoni mwa mikataba hiyo ni pamoja
na Tamko la Kimataifa la Haki za Binadamu (Universal Declaration of Human
Rights (UDHR), Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa (The
International Covenant on Civil and Political Rights (ICCPR) na Mkataba wa Haki
za Binadamu na Haki za Watu wa Umoja wa Afrika (African Charter on Human and
Peoples Rights - ACHPR)
“Nchi nyingi za Afrika zimeweza kupiga hatua za
kimaendeleo kwa kuvitumia vyema vyombo vya habari kwa uhuru na kupelekea
kuinua uchumi wa nchi ambapo ni pamoja na Ghana, Afrika ya kusini
na Mozambique.
Mapema akiwasilisha mada kuhusiana na
“Mapungufu ya Sheria za habari” Bibi Hawra Shamte ambae ni
mwandishi wa habari mkongwe amesema ingawa kuna sheria zinazosimamia sekta ya
habari bado zinaonekana kiuhalisia hazifanyi kazi ipasavyo kwa kulinda usalama
wa waandishi wa habari na wananchi hivyo zinahitaji kufanyiwa marekebisho.
“Baadhi ya sheria hizo ni pamoja na Sheria
ya Usajili wa Wakala wa Habari, Magazeti na Vitabu No. 5 ya mwaka 1988
iliyofanyiwa marekebisho na sheria No. 8 ya mwaka 1997 na Sheria ya Tume ya
Utangazaji Zanzibar No. 7 ya mwaka 1997 iliyofanyiwa marekebisho na sheria No 1
ya 2010”, alieleza muwasilishaji huyo.
Wakichangia katika mafunzo hayo, miongoni mwa
waandishi wahabari wamesema wamaekuwa wakikutana na vikwazo mbalimbali katika
kufanikisha majukumu yao, hali inayosababisha kukosa uhuru na
kutowajibika ipasavyo.
Mafunzo hayo yametolewa na TAMWA-ZNZ kwa
watendaji wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Vijana na
Michezo,Tume ya kurekebisha Sheria Zanzibar, Tume ya Utangazaji na waandishi wa
habari yenye lengo la kuonesha umuhimu wa kuzingatia mikataba ya kikanda
na ya kimataifa ili kuwa na sheria na sera bora zitakazo simamia
masuala ya haki ya kupata habari na kutoa maoni kwa uhuru.
0 Comments