Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
George Simbachawene akitia baraka matarajio ya washiriki wa Programu ya Mafunzo
ya Uongozi ya Ngazi ya Cheti Awamu ya Nne kwa kuweka saini kwenye ubao
unaoonyesha matarajio hayo kabla ya kufungua programu ya mafunzo hayo leo
katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Mwalimu Nyerere (JNICC) jijini Dar
es Salaam
Dar Es Salaam
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma
na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene amesema Uongozi sio
kubadilisha watu uliowakuta badala yake ni kujenga ushawishi wa kubadili
mitazamo ya wale unaowaongoza kwa kuonesha njia ili kufikia malengo makubwa ya
kuwahudumia wananchi.
Mhe. Simbachawene ametoa kauli hiyo leo jijini Dar es Salaam
wakati akifungua Programu ya
Mafunzo ya Uongozi kwa Njia ya Mtandao Ngazi ya Cheti Awamu ya Nne inayotolewa
na Taasisi ya UONGOZI kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Aalto, cha nchini
Finland.
Mhe. Simbachawene amesema kuna tabia imejengeka kwa baadhi ya
Viongozi mbalimbali nchini pindi wanapopewa uongozi huanza
kuwaondoa baadhi ya Watumishi waliowakuta katika Ofisi za Umma kwa
kisingizio kuwa hawaendani na kasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Amesisitiza kuwa, Kiongozi bora hahitaji kujitambulisha kuwa
yeye ni nani bali hutambuliwa kwa jinsi anavyojiweka na anavyoendesha
mambo yake kwa wale anaowaongoza.
''Ukiona Kiongozi anajitambulisha kuwa yeye ni nani tambua kuwa
hapo kuna walakini, Kiongozi hutambuliwa na watu kwa jinsi anavyojiweka katika
jamii kwa matendo yake mema yanayozingatia maadili'' amesisitiza Mhe.
Simbachawene.
Akizungumzia Programu hiyo ya uongozi ngazi ya cheti, Mhe.
Simbachawene amewataka washiriki kusoma kwa bidii kwani Programu hiyo ni muhimu
kwa vile inalenga kuisaidia Serikali katika kuimarisha utendaji kazi na
hatimaye kuwaletea wananchi maendeleo.
Ameongeza kuwa mafunzo hayo yamelenga kuunga mkono jitihada
za Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu
Hassan katika kuimarisha utawala bora, nidhamu, uwajibikaji na maadili katika
kada zote za uongozi.
Amesema mafunzo hayo yamehusisha washiriki
kutoka sekta ya umma na sekta binafsi ambao kimsingi jukumu lao kuu
ni moja ambalo ni kuhudumia wananchi kwa kuzingatia sheria, kanuni na haki.
Mhe. Simbachawene amewahimiza washiriki kuzingatia mafunzo hayo ili
yakawe nyenzo muhimu ya kuwakumbusha mipaka ya utendaji kazi wao na
kutatua changamoto zinazowakabili wananchi na hatimaye kuwa na utawala bora
wenye kuzingatia sheria, maadili na haki.
Kwa upande wake Balozi wa Finland nchini Tanzania, Mhe. Theresa Zitting ameisifu Tanzania kwa kupiga
hatua kubwa kwenye suala la Uongozi hususan, kwenye idadi kubwa ya
wanawake ambao ni viongozi wakubwa kwenye sekta ya umma na binafsi.
''Kwa mwelekeo huu, Mimi kama Balozi nitaendelea kuishawishi
nchi yangu kuendelea kufadhili Taasisi ya UONGOZI ili kuibua wanawake wengi
zaidi katika ngazi za juu za maamuzi'' amesema Mhe. Balozi.
Awali, Mtendaji Mkuu, Taasisi ya UONGOZI, Bw. Kadari
Singo amesema Taasisi yake imejielekeza kuandaa Viongozi wenye maarifa na
wanaojua wajibu wao kwa wanaowangoza na wananchi na sio wanaotaka kupata vyeti
tu.
Jumla ya washiriki takriban 70 kutoka sekta ya umma na sekta
binafsi wanashiriki programu ya mafunzo hayo yatakayofanyika kwa muda wa miezi
sita.
0 Comments