Na Nihifadhi Abdulla Issa :
Nilikwenda kijiji cha Kibele, karibu kilomita 30
kusini mwa mji wa Unguja, na kujikuta nafurahia upepo mwanana wa miti
iliyokuwepo kila pembe ya kijiji hiki.
Hapo nikakutana na mama mja mzito akifanya mazoezi
mepesi kwa kufanya shughuli za nyumbani huku akijitayarisha kwenda kliniki
kuangalia afya yake na kupata ushauri wa wataalamu wa afya ya uzazi.
Mwana mama huyu Mwatum Haji ni kijana wa miaka 35, aliniambi
aliona mabadiliko katika mwili wake ambayo yameambatana na uchovu wa mwili na
kizunguzungu kilichosababisha kupoteza hamu ya kula na kulala mara kwa mara.
Hali ya mama huyu ilidumu kwa takriban wiki moja bila kuona
mabadiliko yoyote jambo lilomshangaza hadi palipotokea mabadiliko ya ya
mzunguko wake wa hedhi.
Aliniambia alipata mshituko na kuamua kwenda kituo cha Afya cha
Tunguu, kilichopo masafa mafupi na kijiji chake na kukutana na wataalamu wa
Afya ambao walimpima mkojo ili kujuwa kama ni mjamzito au anasumbuliwa na
maradhi mengine.
Baada ya vipimo aligundulika ameshika ujauzito wa
mwezi mmoja na kushauriwa mambo muhimu yanayohusu afya yake, ikiwa pamoja na
kuhudhuria kliniki mapema na kwa wakati.
Tokea wakati huo akawa kiguu na njia kila baada ya muda kufunga
safari yake ya kwenda kliniki ambapo alikuwa anapata vipimo na ushauri kwa
usalama wa afya yake na kiumbe kilichokuwa tumboni mwake.
Alisema amejifunza umuhmu na faida ya kuhudhuria kituo cha afya
mapema kwa mama mja mzito kwani mimba inapokuwa changa matatizo yanakuwa mengi
.
“Nimepata somo katika mimba yangu hii ya tatu kwani kwa mimba
zilizopita nilichelewa kuhudhuria kliniki mapema.
Matokeo yake nilipata matatizo mbali mbali, ikiwemo kupoteza
damu mara kwa mara lakini kwa mimba hii kwa kwenda kliniki mapema
nimepata elimu ilionisaidia kuondokana na matatizo ya mimba ziliopita,” alisema
huku akitabasamu.
MTAZAMO WA WANAUME KWA WAKE ZAO KUHUDHURIA KLINIKI MAPEMA
Juma Ali (37) (sio jina lake rasmi) wa Tunguu, alisisitiza
kwamba upo umuhimu wa mama wajawazito kuhudhuria kliniki mapema kwa sababu
kufanya hivyo kuna faida nyingi na kuchelewa kuna athari zake.
Aliwataka wanawake wasifanye uvivu wa kuchelewa kwenda
kliniki na kuwashauri kuwasikiliza wataalamu wa afya.
Juma ambaye amesomea taaluma ya afya ya uzazi alitahadhaisha
kwamba mtu ambaye hafuati maelekezo ya madaktari anaweza kupata matatizo ambayo
yangeweza kuepukika.
Omar Abdalla (40) mkaazi wa Ndijani, alisema humshauri mke wake
kuhudhuria mapema mara tu anapona viashiria vya ujauzito ili kupata elimu ya
ziada ya namna nzuri ya kuilea mimba.
“ Mtoto ni neema na baraka kutoka kwa Allah wanikuna watu
wanatamani kupata watoto, lakini hawajaaliwa. Nikiona viashiria tu vya ujauzito
kwa mke wangu jambo la kwanza namshauri aende kliniki kupata ushauri juu ya
afya yake na namna gani tutashirikiana kulea hiyo mimba,” alieleza
Omar Abdalla, Mkaazi wa Ndijani.
Bashir Rajab Mtumweni (32) pia wa Tunguu , alisema umuhimu wa
wajawazito kuhudhuria kliniki mapema ni kugunduwa athari za kiafya, kama
zipo, mapema ni kupata kinga na matibabu maema kwa mama na mwanawe
aliyembeba tumboni.
Alieleza kwamba mke wake wakati akiwa mjamzito alipata matatizo
ya fuko lake la uzazi kuwa jepesi, lakini alipohudhuria kliniki mapema alipewa
ushauri wa kupunguza kufanya kazi za nguvu na kutumia muda mwingi kupumzika na
hii ilimsaidia.
“Baada ya kuarifiwa hali hio nilimpunguzia mke wangu majukumu ya
kazi na kuwajibika mwenyewe kwa majukumu ya ndani, alieleza Bashir
Rajab, Mkaazi wa Tunguu.
Katika hii ziara maalum ya vituo vya afya vyaWilaya
ya Kati na Magharibi “B” tulifika kituo cha Afya Mwera na kuwakuta mama
wajawazito waliopanga foleni kusubiri zamu zao za kuonana na
daktari.
Hapo Mwera nilizungumza na Samir Salim (40) ambaye alisema
anatoa mashirikiano mazuri kwa mkewe anapogundua ni mjamzito na
humsaidia majukumu ya nyumbani, ikiwa pamoja na kuhudumia watoto.
“Majukumu ni ya kwetu sote, lakini mke wangu anapokuwa mjamzito
nafanya kazi za nyumbani ili apumzike na kulea ujauzito akiwa na amani.Hii ni
kwa sababu na kiumbe kilichopo tumboni nacho kinahitaji kupumzika vyemaili afya
yake iimarike’’, alisistiza.
Bi Asha Faki (34), mkaazi wa hapo Mwera ni mama mwenye watoto
wawili na alikuwa na uja uzito wa tatu uliokua na miezi mitano. Hii ilikuwa
mara yake ya kwanza kuhudhuria kliniki.
Mama huyu alisema hakuwa anahudhuria kliniki mapema pindi kwa
kuhofia aibu ya kusemwa na wanawake
wenzake, hivyo husubiri angalau miezi mitano pale tumbo likianza kuchomoza.
Alikiri wakati akivuta muda wa kwenda kliniki alikuwa
anakabiliwa na matatizo, ingawa sio makubwa. Haya ni kujiona mchofu, hasa anapoamka
asubuhi, miguu kuvimba na anakosa hamu ya
kula.
USHAURI WA WATATALAMU WA AFYA
Khatib Ramadhan Haji, Afisa Tabibu na Mkuu wa kituo
cha Afya cha daraja la kwanza cha Tunguu ambacho kinahudumia shehia za Tunguu,
Jumbi, Binguni na Bungi , zenye wastani wa wagonjwa 10,000 alisema wanawake
wenye matarajio ya kubeba ujauzito ama wenye uwezo wa kujifunguwa ni
4,200.
“Sisi tunatoa e elimu ya afya ya uzazi na kuhimiza waja wazito
kuhudhuria kliniki mapema ili kuepuka athari zinazoweza , kama vile
magonjwa yanayoweza kutibiwa au kukingwa
mapema,” alieleza Khatib Ramadhan Haji, Afisa Tabibu wa
Kituo cha Afya Tunguu.
Kituo cha Tunguu kinatowa huduma za upimaji wa mama
wajawazito, chanjo zote kwa wasichana na watu wazima, upimaji na
lishe kwa watoto na elimu ya afya ya uzazi ambayo inajumuisha chakula
kinachowajenga kiafya mama wajawazito.
Afisa Muelimishaji na Muhamasishaji wa Afya ya Uzazi, Mama na
Mtoto katika Wizara ya Afya Zanzibar, Kitengo Shirikishi cha Mama na Mtoto,
Fatma Ussi Yahya, alisema kitengo kinatowa elimu kupitia vyombo vya
habari ili kuelimisha jamii kujuwa afya zao mapema kwa sababu
kipindi cha mwanzo cha ujauzito huwa na mabadiliko ya mwili.
Alisema wanelimisha akina baba wanapogunduwa wake zao
waja wazito ni vizuri kuwasindikiza hospitali kupata pamoja elimu ya afya ya
uzazi na kufahamu athari za kuchelewa kuhudhuria kliniki mapema.
Vile vile wanatoa ushauri kupitia ujumbe ama taaluma kutoka kwa
madaktari ili kulea familia yake na kupata muda wa kufanya majukumu yake kwa
kupanga uzazi.
Daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake na uzazi kutoka Hospirali
ya Rufaa Mnazi Mmoja, Ummulkuthum Omar, alisema wanatoa taaluma kwa mama
wajawazito kuhudhuria kliniki mapema wakati wakigunduwa tu wameshashika
ujauzito ili kuepuka athari.
“Tunawahamasisha mama waja wazito kufika kliniki kuanzia wiki
moja ya ujauzito lakini baadhi yao ni wakaidi na wanakuja
mimba ikiwa ni ya miezi mitano mpaka sita.
Akiwa na tatizo, basi hali huwa ngumu kidogo kuishughulikia,”
alifafanua Dk Ummulkulthum Kwa mujibu wa Takwimu mama wajawazito
waliohudhuria klinikic mapema kutoka Kituo cha Afya cha Mwera
2020/2021 ni 147 ambapo kwa mwaka 2022/2023 kuanzia January hadi Augosti 150.
MIKAKATI YA WIZARA YA AFYA ZANZIBAR
Katika hotuba yake ya bajeti ya 2021/22, Waziri wa Afya, Ustawi
wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto Zanzibar, Mh. Nassor Ahmed
Mazrui, alisema katika kuhakikisha vifo vya mama wajawazito
vinapunguwa Wizara inafanya juhudi mbali mbali
zae kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi.
Miongoni mwa juhudi hizo ni kuhakiki vifo ili kubaini sababu
zilizopelekea kutokea na kuchukua hatua stahiki.
Katika kipindi cha Julai 2020 hadi Machi 2021, vifo vya mama 44
na watoto wachanga 1,201 viliripotiwa katika hospitali zinazotoa huduma za
uzazi.
Vifo vya mama ni 28 (asilimia 63) na vya watoto wachanga 446
(asilimia 37) vilihakikiwa. Matokeo ya uhakiki huo yamebainisha sababu za vifo
ni pamoja na watoto kukosa hewa wakati wa kuzaliwa; uzito pungufu; njiti;
kupoteza damu na maambukizi kwa watoto wachanga.
Kwa upande wa vifo vya mama ni kifafa cha mimba, upungufu
wa damu wakati wa ujauzito, kupoteza damu wakati wa ujauzito, kisukari na
maradhi mengine sugu wakati wa ujauzito.
Ingawa jitihada zinafanywa na Wizara husika ya
kuwahamasisha akina mama wajawazito kuhudhuria kliniki bado elimu ya
ziada inahitajika.
Takwimu za Wizara ya Afya, Jinsia, Wazee na Watoto Zanzibar
zinaonesha mama wajawazito 46,050 walihudhuria kliniki ya upimaji mimba angalau
mara moja katika kipindi cha ujauzito kwa mwaka 2020/2021 ukilinganisha na 40,177
wa mwaka 2019/2020.
Katika kipindi hicho, akina mama waliojifunguwa walikuwa
ni 33,057, sawa na asilimia (61.3%) Kwa hospitali za Unguja ni
Unguja ni 22,164 na Pemba ni 10,893.
Mradi wa Afya ya Uzazi Wasichana na Wanawake
umefadhiliwa na Shirika la Wellspring Philanthropic Fund la Marekani.
Kwa sasa mradi huu unatekelezwa na Chama cha Waandishi wa Habari
Wanawake kwa Upande wa Bara na Zanzibar kwa lengo la kuongeza ushawishi na
utetezi kwa kupitia vyombo vya habari juu ya umuhimu wa upatikanaji wa huduma
ya Afya ya Uzazi kwa wasichana na wanawake
0 Comments