Na Nafda Hindi
Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Dk Khalid Salim Mohammed ametangaza viwango vipya vya mwendo kwa barabara za Zanzibar.
Akizungumza na waandishi wa habari huko Ofisini kwake Kisauni Dk Khalid amesema kuanzia sasa mwendo utakaotumika kwa barabara za Mjini,kwenye vivuko,sehemu za biashara,school,hospital na maeneo ya Mji Mkongwe ni kilomita 30,Mji wa Chake Chake, Mkoani na Wete ni kilomita 50 na kilomita 80 kwa barabara za vijijini kwa saa.
Amesema maagizo hayo ya Serikali yamezingatia Sheria ya Usafiri na Usalama barabarani no 7(2003) kifungu 144 kwa lengo la kupunguza ajali za barabarani zinazosababishwa na mwendo kasi.
“Sheria zetu za barabarani tunazotumia kwa sasa za toka mkoloni tangu miaka ya sitini,na kipindi hicho idadi wa watumiaji ilikuwa ndogo ni laki tatu na khamsini kwa kipindi hicho, kwa sasa barabara zetu zina urefu wa kilomita elfu moja,mia tatu na khamsini na tatu na idadi ya watu imeongezeka,” alisema Dk Khalid.
Aidha Dk Khalid amelitaka jeshi la polisi kusimamia amri hiyo kwa vitendo na kuchukuwa hatua za kisheria kwa dereva yeyote atakaekiuka agizo hilo.
“Jeshi la polisi naomba musimamie agizo hili na sheria zifate mkondo wake kwa dereva yeyote atakae kaidi agizo hili,”Amesisitiza Khalid.
Hata hivyo amewaomba watembea kwa miguu kuwa makini na kufuata sheria za barabarani wakati ili kuepuka ajali.
Sheria hiyo mpya ya viwango vipya vya mwendo wa barabarani itaanza kutumika rasmi wiki moja baada ya kutoka agizo hilo.
0 Comments