Baadhi ya wanachama wa Chama cha Wananchi CUF wakiwa kwenye mkutano wa hadhara katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 ambapo wengi wa waliohudhuria katika mkutano huo ni wanawake.Picha kwa Hisani mtandao |
Na Ahmed Abdalla
Wakati Dunia ikiendelea
kupaza sauti juu ya ushiriki wa wanawake katika nafasi mbali mbali za uongozi
Zanzibar nayo haipo nyuma katika
harakati hizo kupitia chama cha Waaandishi wa habari wanawake Tanzania (TAMWA-ZNZ)
na wadau wengine wamekua wakiendelea na harakati za kuwapigania wanawake bila
kuchoka, usiku na mchana ili kutumiza ndoto za walio wengi zinazojaribu
kukatishwa kila leo na watu wenye dhamira zao binasi zikiwemo za kuwadumaza
wanawake na kuendelea kuwafanya ngazi ya kutimiza malengo yao. Muendelezo wa matakwa haya ya
Dunia.Nchini Tanzania ambayo Zanzibar ni sehemu iliyounda Jamuhuri hiyo,inatiliwa
mkazo na ibara ya 13.(1) ya katiba ya Tanzania ambayo inasema watu wote ni sawa
mbele ya sheria na wanayo haki, bila ya ubaguzi wowote, kulindwa na kupata haki
sawa mbele ya sheria.
Kwa msingi huu wa
katiba ni wazi kuwa katiba ya Nchi inatambua
haki ya kila mtu kuwa kiongozi hivyo hakuna budi wanawake wengi zaidi kupewa nafasi
za uongozi ili kutekeleza haki hii muhimu ya kikatiba.
Msingi huu wa katiba
unatiliwa mkazo kila leo na wadau mbali mbali ikiwemo TAMWA-ZNZ, katika
utekelezaji mradi wa kuwawezesha wanawake kushika nafasi za uongozi (SWIL) ambapo
hadi sasa imefanikiwa kuwafikia wananchi
wapatao 8793 kati yao wanawake
wakiwa 5276 na wanaume 3217 katika maeneo mbali mbali Unguja
na Pemba. Licha ya kuwa jitihada
kubwa zimefanyika lakini nguvu kazi zaidi inahitajika ili kufikia malengo
ambayo ni kuleta usawa katika nafasi mbali mbali za uongozi kwa wanaume na
wanawake sambamba na ushiriki wa wanawake katika demokrasia. Itakumbukwa kuwa katika
siku za hivi karibuni wakati akitangaza matokeo ya idadi ya sensa ya watu na
makaazi Rais wa Jamuhuri ya Muungano Tanzania Dkt,Samia Suluhu Hassan alisema
Zanzibar kama sehemu ya Jamuhuri ya Muungano, ina watu wapatao 1,889,773 kati yao wanaume ni 915,492 sawa na asilimia 48.4 na wanawake ni 974,281 sawa na asilimia 51.6 ambapo licha ya matukio hayo ya sensa kuonesha kuwepo kwa uongezeko la idadi
kubwa ya wanawake kuliko wanaume lakini bado hali halisi ya ushiriki wa wanawake
katika uongozi haijaridhisha.
Wakati hayo yakijiri
kwa upande wa takwimu za tume ya uchaguzi Zanzibar (ZEC) katika uchaguzi mkuu
uliofanyika mwezi oktoba mwaka 2022 Zanzibar ilikua na idadi ya wapiga kura
wapatao 566352 kati, yao wanawake ni 294237 na wanaume ni 272115 pamoja na takwimu hizi pia
kuonesha wanawake ndio waliokua wapiga kura wengi zaidi katika uchaguzi huo
bado nafasi nafasi za ushiriki wanawake
katika nafasi za uongozi haziendani na uhalisia wa wingi wao jambo ambalo, linawafanya wadau kukosa usingizi kila leo. Kwa mfano kupitia
utafiti mdogo uliofanywa na mwandishi wa
makala haya umebaini kuwa Zanzibar katika majimbo yote 50
ya kupigiwa kura kwa nafasi za uakilishi ni wanawake 8 pekee ndio walipata nafasi ya kuchaguliwa kati ya wanaume 42 na kwa nafasi ya Ubunge kutoka
majimbo haya ni wanawake 4 tu ndio
walipata nafasi ya kuchaguliwa kati ya wanaume 46. Huku hayo yakijiri kwa
nafasi za ubunge na uakilishi kwa upande wa madiwani Zanzibar ina madiwani 25 wanawake kati ya wanaume 110 na kwa upande wa masheha wanawake
ni 64 kati ya wanaume 389 hii, ni wazi kuwa bado jitihada
zaidi zinahitajika katika kumkomboa mwanamke. Je
tunakwama wapi? Ndilo swali ambalo
linaendelea kugonga vichwa huku wanaharakati wengi wakiendelea kujiuliza ni
wapi haswa Zanzibar inakwama katika kuongeza idadi kubwa ua ushiriki wa
wanawake kwenye uongozi na demokrasia. Wasemavyo
wahusika Halima Ibrahim aliewahi
kuwa Mgombea Ubunge Jimbo la Malindi mjini Unguja kupitia chama cha ACT Wazalendo anasema kuna
changamoto mbali mbali ambazo zimekua zikiwakwamisha wanawake wengi wanapotaka
kugombea kushika nafasi za uongozi. Akitaja changamoto hizo
alisema ni pamoja na mifumo ya kutoa maamuzi kwenye vyama vya siasa kuwa na
idadi kubwa zaidi ya wanaume kuliko wanawake kamati ambazo ndio zenye majukumu
ya kuteuwa nani awe mgombea na nani asiwe mgombea. Alisema kuwepo kwa
idadi kubwa ya wanaume ndani ya kamati hizi ni wazi kuwa nafasi ya wanawake
haitapewa kipao mbele badala yake wagombea wengi watapitiswwa kuwa wanaume
kwani wengi wao hutengeneza urafiki na wajumbe hao. ‘’Kuna wakati hata
ukiona mwanamke kapitishwa basi unaweza kumkuta mwanamke kawekwa kwenye jimbo
gumu zaidi huku chama chake kikijua kabisa kuwa hawezi kushida na haya ndio
yanayotokea kwa mfano utaona majimbo mengi au karibu yote ya Pemba hakukua na
mgombea mwanamke’’alifafanua. Jine Shaame ni
mwanachama wa chama cha wananchi CUF aliewahi kuomba ridhaa ya chama chake
jimbo la Chonga Wilaya, ya chake chake mkoa wa kusini Pemba alisema aliomba ridhaa
ya chama hicho lakini kabla kujua sababu, madhubuti ambayo ilikifanya chama hicho kuondoa jina lake na kurudisha jina la
mgombea mwanaume ambae anaamini kuwa
hakua, sehemu ya mwenye kukubalika na
jamii kuliko yeye na inawezekana ndio sababu ya mgombea wa chama hicho
kutoshinda kwenye jimbo hilo. ‘’Hata wazo langu la
kuomba ridhaa ya chama changu kuniteuwe lilikuja baada ya kuombwa na wananchi
ambao ndio wakaazi wa eneo husika na nilikua na hakika naweza kushinda kwenye
jimbo hili lakini sikurudishwa na chama na kupelekea wananchi kununa na
kutomchagua alierudishwa na chama changu’’aliongezea. Kwa masharti ya
kutotajwa jina wala chama amabacho aliwahi kuomba alisema wakati anataka kuomba
ridhaa alikuatana na changamoto kubwa ambayo ilimkatisha tamaa na kutotamani
kuwa kiongozi hata wa nafasi ya chini kwenye chama chake. Alisema alikumbwa na mazingira magumu ya kuomba rushwa ya ngono
na watu ambao huwezi hata kuamini kwenye vyama vyao kutokana na nafasi walizonazo
lakini anashangaa watu kuwaamini na kuona ni watu wema. Alisema anaamini kuwa
kuna viongozi kwenye vyama hawakupaswa kuwa na nafasi hizo kwani wamekua
wakizitumia vibaya na kuwapa wakati mgumu wanawake wenye ndoto za kugombea na
kuwakomboa wanawake wengi zaidi. ‘’Lazima tukubali
ukweli ili wanawake wengi wawe viongozi lazima wavutwe na wanawake wenzao ambao
nao pia watakua viongozi ni lazima tupambane na tupambaniwe’’aliongezea. Pamoja na changamoto hizo zipo pia simulizi zinaeleza kuwa baadhi ya mitazamo potofu ya dini imekua ikiwafanya wanawake kutokukubalika katika maeneo mbali mbali wakiamini kuwa dini imekua ikikataza wanawake kuwa viongozi hata wa ngazi za awali. Kauli
za viongozi wa dini Kwa muktadha wa kutaka
kujua undani wa mtanzamo huu Sheikh Khamis Abdulatif kutoka mkoa wa kaskazini
Unguja anasema hakuna sehemu ambayo dini imekataza mwanamke kuwa kiongozi. Anasema baadhi ya watu
kwenye jamii wamekua wakichukua vipengele vya dini kwa matakwa yao wenyewe
lakini uhalisia dini haikukataza mwanamke kuwa kiongozi na kueleza kuwa hata
Bwana Mtume Muhammad (S.W) aliwaamuru watu enzi za uhai wake wachote elimu kupitia
pia kwa mke wake Bibi Aisha kuashiria
kuwa alikubali na kuwaamini wanawake kama sehemu ya chemchem ya elimu na
viongozo. Kwa upande wake
Kiongozi wa dini ya ‘’Chrstian’’ kutoka kanisa la minara miwili Zanzibar Askofu
Michael Hafidh alisema kuendelea kuwanyima wanawake fursa za uongozi kwa
kisingizio cha dini ni kuwanyima haki zao muhimu ambazo anaamini hakuna dini
iliozuia mwanamke kuwa kiongozi. Wasemavyo
wanasiasa Mwenyekiti wa Chama cha
ADC Hamad Rashid Mohamed akifanya mahojiano na mwandishi mwa Makala haya
alikiri uwepo wa shida kwenye ushiriki wa wanawake kwenye nafasi za uongozi
sambamba na kunasibisha mambo mbali mbali ambayo wenyewe huwa kama sehemu ya
tabia zao. Akitaja miongoni mwa
sababu hizo alisema pamoja na ubinafsi unaofanywa na watu wenye maamuzi ndani ya vyama vya siasa
pamoja na yale anayoyajua yeye katika historia yake ya siasa ambapo alisema
si rahisi kuweza kuyataja hadharani lakini tu alisisitiza jitihada zaidi
zinahitajika. Akizungumza kwa njia ya
simu Katibu mkuu chama cha ACT Wazaledo Ado Shaibu alisema chama hicho
kimejipambanua kuanzia kwenye katiba ya chama chao kuhusu kuleta usawa katika
nafasi za uongozi. Alisema inawezekana
kumekua na changamoto kwenye mamlaka za teuzi na kuahidi kuwa changamoto hizo
zitafanyiwa kazi na pia kuongeza ushawishi kwa vyama vyengine vya siasa
vitambue umuhimu wa wanawake katika nafasi za uongozi. Katibu wa itikadi na
uendezi chama cha Mapinduzi CCM Katerina Peter Nao alikiri kuwepo kwa
changamoto na kusema kuwa licha ya changamoto hizo wanawake wanapaswa kusonga
mbele. Alisema kuna wakati
watu wenye nafasi kwa matakwa yao wanaweza kuweka vizingiti vya wengine kusogea
mbele lakini wasirudi nyuma na watafute njia mbadala kuona ni kwa namna gani
wanaweza kushinda na kutimiza melengo waliojiwekea. Je
wasomi wanasemaje kuhusu hili? Dkt Yahya Mzee kutoka
chuo kikuu cha Zanzibar University,anasema kuna haja ya wanawake wenyewe
kujitambua na kujua wanachokitaka,akisema kuwa si ajabu kumuona mgombea
mwanamke akishindwa kujua hata vipao mbele vyake kwenye jimbo analoishi na
kuwafanya wafuasi kuwa wenye mshangao mkubwa ikiwa mtu anaeomba ridhaa hajui
changamto za wananchi wenye jimbo lake. Alisema wanawake
wanapaswa kujengewa uwezo zaidi kwenye siasa na kuzitaka asasi mbali mbali
kujikita zaidi ikiwa ni pamoja kuwatengeneza mapema wanawake ambao wana nia ya
kugombea, na kuwasisitiza pia kujiongeza kielimu kwani wataongeza upeo na
kupambanua mambo mbali mbali ambayo yatawafanya kuwa wabobezi wazuri wa siasa
na wajengaji imara wa hoja zenye kukubalika. Pamoja na hayo
alizitaka taasisi mbali mbali zilizojikita kuwasaidia wanawake kuweka mkakati maalumu wa kuwatambua mapema,wanawake ambao wana nia ya kugombea na kuwajengea uwezo ambao anaamini
utawasaidia hata kusimama na kuzungumza mbele za watu jambo ambalo linahitaji
ujasiri. Mtalamu wa maswala ya
uchumi ambae pia mi mjumbe katika kamati ya utafiti ya chuo cha Zanzibar
University. Hafid Ali aliwashauri wanawake wenye nia ya kutaka kugombea kufanya pia
shughuli mbali mbali, za kijasiriamali, kwa lengo la kujingizia kipato na kuweka akiba
ili fedha hizo ziweze kuwasaidia wenyewe. Alisema kwa mazingira
yaliopo sasa imefika wakati jamii kuamini zaidi kwenye fedha unapotaka kugombea
hivyo wanawake wengi wanashidwa kwa sababu ya kukosa fedha ambazo zingewasaidia
hata kuendesha mikutano ya kampeni na mambo mengine. Mkurugenzi
TAMWA-ZNZ atoa ushauri wake Kwa upande wake
Mkurugenzi wa TAMWA-ZNZ Dkt,Mzuri Issa anasema wamekua wakifanya harakati hizo
kwa muda mrefu na kwa kiasi fulani wameanza kufahamika kwenye jamii. Alisema wakati wanaanza
harakati za kuwapigania wanawake jamii iliwashangaa sana na kuwaona kama watu
wa ajabu wasiojua watendalo lakini leo hii watu wameanza kuelewa ukweli na
kuwaunga mkono ingawa kwa asilimia ndogo sana. Hata hivyo alisema
jitihada za pamoja kwa wananchi wote na Asasi za kiraia zinazhitajika kumkomboa, mwanamke katika makucha ambayo yamewafanya kuwa watu wa kuongozwa na sio wakuongoza, jambo ambalo
anaamini kuwa ni kutowafanya wanawake wengi kushindwa kupiga hatua za
kimaendeleo. Akifafanua zaidi
alisema pamoja na jitahada mbali mbali za
maendeleo zinazoendelea kufanyika hazitaweza kufanukiwa kwa asilimia mia
iwapo ushiriki wa wanawake hautaongezeka na kuwa mkubwa zaiid ikiwezekana kutia
kwa falsafa nzima ya hamsini kwa hamsini.
Mwisho.
|
0 Comments