Ticker

6/recent/ticker-posts

GEF Yataka Ushiriki Wa Wadau Kufikia Usawa Wa Kizazi Cha Jinsia.

 


Na Ahmed Abdulla

Mwenyekiti wa kamati ya Jukwaa la  Usawa wa Kijinsia (GEF) Tanzania Bibi Angellah Kairuki amesema kuna umuhimu mkubwa wa kuwekwa kwa mikakati imara ya uwepo wa usawa wa kijinsia katika pande zote mbili za Jamuhuri ya Muungano Tanzania kwa lengo la kurahisisisha kufikia usawa wa kizazi cha jinsia katika uchumi pamoja na maendeleo ya taifa kwa ujumla.

 

Aliyasema hayo wakati alipokua akizungumza na Spika wa Baraza la Wawakilishi (BLW) Mh. Zuber Ali Maulid kufuatia ziara maalumu ya kujitambulisha iliyofanywa na kamati hiyo ndani ya ukumbi wa Baraza la wawakilishi Chukwani nje kidogo ya mji wa Zanzibar.

 

Alisema kamati hiyo ambayo imelenga kushughulikia mambo 11 imejiwekea tayari mpango kazi wake wa miaka mitano ambao wadau watapata fursa pia kuuchangia ili kuhakikisha kuwa inapata mpango mzuri na wenye maono mapana.

 

Kamati hiyo yenye wajumbe 26 kutoka Bara na Zanzibar imetokana na juhudi za kimataifa za kuelta usawa wa kijinsia ambapo imeundwa na kuzinduliwa mwaka jana na Mh Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mh Samia Suluhu Hassan ambaye ndiye kinara wa masuala ya usawa wa kiuchumi kwa Afrika.

Mwenyekiti Angela, akiyataja mambo hayo 11 alisema ni pamoja na vituo vya kulea watoto ili mama waweze kufanyakazi vizuri na kuhudumia watoto, upatikanaji wa maji safi, umeme, teknolojia rahisi, kukuza ajira zenye stara, kuzalisha bidhaa zenye ushindani, uwekezaji katika elimu hasa kwenye masomo ya sayasansi, hesabu na uhandisi, kuimarisha mifuko ya kina mama, kuhamasisha mabadiliko ya mila potofu, kuimarisha mifuko ya fedha jumuishi, ulinzi wa hifadhi ya jamii na utambuzi wa kazi zisizo kuwa na malipo hasa majumbani (unpaid works).

 

Hivyo, Mwenyekiti amesema maeneo hayo yatahitaji kuwa na takwimu za kuanzia katika kila sekta na pia kuwa na ripoti za maendeleo yake kila mwaka ambapo wadau wa sekta zote kutoka kwenye Serikali na wasio na Serikali wakiwemo na wajumbe wa BLW wanahitaji kushiriki kikamilifu.

 

Mmoja miongoni mwa wajumbe wa kamati hiyo Bibi Abeida Rashid Abdalla ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara Ustawi wa Jamii,Wazee,Jinsia na Watoto,alimuomba Spika wa Baraza la wawakilishi Zanzibar(BLW) kuwashauri wajumbe kuzingatia usawa wa kijinsia katika bajeti pamoja na ripoti zinazowasilishwa Barazani hapo ili kufikia malengo hayo ya usawa wa kijinsia.

 

Kwa upande wake Spika wa Baraza la wawakilishi Zubeir Ali Maulid alisema ameipokea kamati hiyo na ameishauri kutenga muda maalum wa kuonana na wajumbe ili kuwaeleza vizuri mikakati ya kufikia usawa huo wa kizazi cha kijinsia.

Amesema pia Baraza liko tayari katika kushiriki katika utekelezaji wa mpango huo wa miaka mitano kwa sasa ili kutoa mchango wake unaostahiki na hivyo kuwa ni sehemu muhimu ya utekelezaji.

 

Kwa upande wa Zanzibar kamati hiyo inahusisha Naibu Spika wa BLW Mh Mgeni Hassan Juma,  Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Jinsia Bibi Abeida Rashid,  Mkurugenzi Mtendaji  Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ),  Dk Mzuri Issa, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Wanawake , Najma Hussein na aliyekuwa Mkurugenzi wa NMB, Zanzibar Bw Abdalla Duchi  Hassan Khatib ambae ni Mkurugenzi wa mwevuli wa Asasi za kiraia Zanzibar (ANGOZA).


Post a Comment

0 Comments