Na Ahmed Abdulla Othman
Baadhi ya maafisa wa Jeshi la Polisi wanaofanya kazi
katika madawati ya jinsia visiwani Zanzibar wamesema licha ya uwepo wa zuio la
Rais la kutaka kutopewa dhamana watuhumiwa wa kesi za udhalilishaji lakini
wamekua wakikabiliwa na chanagmoto ikiwemo ya kukosekana kwa maandiko ya
kisheria.
Walioyasema hayo katika mkutano wa wadau wa kupambana na
udhalilishaji ulioitishwa na TAMWA-ZNZ huko Tunguu Wilaya ya kati Unguja na
kuwashirikisha wadau mbalimbali ikiwemo kutoka kisiwani Pemba.
Akitoa ushuhuda Afisa dawati la jinsia kutoka mkoa wa
kusini Unguja Ali Mohamed Othman alisema wao kama maafisa wa dawati wanakutana
na chanagmoto hizo ambazo kwa kukosa maandiko ya kisheria baadhi ya wakati
huwawia vigumu.
Alisema ni hivi karibuni walipata taarifa za kubakwa kwa
mtoto wa kike na wakamkamata mtu alietuhumiwa kufanya hivyo hatimae kumuweka
ndani kama sehemu ya kazi zao lakini baada ya muda walipata barua ikiwataka
wakajieleza kwanini wamemzuia mtuhumiwa huyo bila ya kumpa dhamana.
Alieleza hayo yote yalitokea akiamini ni kwa sababu
sheria halisi ya zuio la dhamana haipo na ndio maana imekua ikitokea hali hiyo
iwapo mtu atazuiliwa na kuwekwa ndania.
Wakati hayo yakijiri miongoni mwa washiriki wa mkutano
huo akiwemo mzazi ambae ni miongoni mwa waliowahi kubakiwa mtoto wake alisema
suala la dhamana kwa watuhumiwa linapaswa kuwekwa sawa na lisiachwe kwa kupitia
tu kauli ya Rais.
Alisema kuna haja ya mabadiliko ya sheria na kifungu
hicho kiwekwe wazi kuwa sheria inamzuia mtu yoyote anaetuhumiwa kufanya makossa
hayo asipewe dhamana hadi pale uchunguzi utakapobainika na kisha hatua za
kisheria kuchukuliwa.
0 Comments