Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt.Damas Ndumbaro |
WAZIRI wa Maliasili na
Utalii, Dkt.Damas Ndumbaro amewataka Watumishi wote wanaofanya kazi katika
Taasisi zote zilizo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii wajiandae
kisaikolojia kupitia mfumo wa mafunzo ya Kijeshi.
Ametoa agizo hilo
mwishoni mwa wiki wakati alipokuwa akizungumza na Watumishi wa Chuo cha
Misitu Olmotonyi kilichopo Jijini Arusha ikiwa ni ziara ya kikazi Chuoni hapo
ya kuwatembelea na kuzungumza na Watumishi hao ili kujua changamoto
zinazowakabili na kuzitafutia ufumbuzi
Amesema mabadiliko ya
mfumo wa utendaji kutoka ule wa kiraia kwenda katika mfumo wa Jeshi Usu,
yanalenga kuleta suluhisho la kudumu katika kukabiliana na changamoto za
usimamizi wa rasilimali misitu na nyuki pamoja na wanyamapori nchini.
Amesema hakuna
Mtumishi yeyote wa Taasisi hizo atakayekwepa mafunzo hayo kwa vile hiyo
ni sera ya Wizara huku akisisitiza kuwa hilo halikwepeki na yeyote ambaye
hayupo tayari basi ahame wizara hiyo ndiyo itakuwa salimika yake
" Leo unaweza
kuhamishwa kutoka Olmotonyi kwenda Shirika la Hifadhi za Taifa ( TANAPA) au TFS
wenzako kule washakamilika tayari ni wanajeshi, wewe utakuwa raia"
alihoji Dkt.Ndumbaro
Amesisitiza kuwa
kila mtumishi aliyeko katika Taasisi hizo lazima apitie mafunzo hayo kwa sababu
watakuwa wakihamishwa kutoka Taasisi moja hadi nyingine ndani ya Wizara hivyo
endapo hajapitia mafunzo hayo itamuwia vigumu katika kutekeleza majukumu yao
wakati akiwa raia katika mfumo wa kijeshi.
Amezitaja Taasisi hizo
kuwa ni Mfuko wa Misitu Tanzania (TFF) Mfuko wa Wanyamapori Tanzania (
TWPF) Bodi ya Utalii Tanzania ( TTB) Chuo cha Taifa cha Utalii ( NCT) Chuo cha
Misitu Olmotonyi, Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori Mweka, Chuo cha Taaluma ya
Wanyamapori Pasiansi, Makumbusho ya Taifa (NMT), ChUo cha Nyuki Tabora
(BTI), Taasisi ya Utafiti ya Wanyamapori Tanzania (TAWIRI) Taasisi ya
Utafirti wa Misitu (TAFORI) TAWA, TANAPA na TFS
Kupitia agizo
hilo,Dkt.Ndumbaro amezitaka Taasisi hizo kujiandaa kushiriki katika mafunzo
hayo ambapo amesema mafunzo hayo yatatolewa kwa awamu awamu.
Akizungumza na
Watumishi hao wa Chuo cha Olmotonyi, Dkt.Ndumbaro amesema anataka
wanavyowafundisha wanafunzi wao ambao wataajiriwa TFS inayoendeshwa kijeshi ni
lazima wakufunzi wao wawe wanajeshi kwanza
" Haiwezekani
mnawafundisha Wanafunzi waende kuajiriwa huko TFS kama wanajeshi wakati
ninyi sio wanajeshi, mnawafundisha nini " alihoji Ndumbaro
Awali, Kamishna
Uhifadhi wa TFS, Prof.Dos Santos Silayo alieleza kuwa kwa vile TFS ndo imekuwa
muajiri mkuu wa Wahitimu wa Chuo hicho hivyo wameanza utaratibu wa kuhakikisha
baadhi ya kozi katika Chuo hicho ziwe na mafunzo ya kijeshi ili kuwaandaa
wanafunzi wa Chuo hicho wanapoajiriwa na TFS
Alisema ili
kuhakikisha hilo linafanikiwa wao kama TFS imekichagua Chuo hicho kuwa mojawapo
ya kituo cha Mafunzo ya kijeshi kwa baadhi ya Maafisa kutoka TFS.
0 Comments