Makamu wa Pili wa Rais
wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla ametoa muda wa wiki moja kwa
Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar {ZAECA} kukamilisha
uchunguzi juu ya Pampu Saba za kusukumia Maji zilizonunuliwa na Mamlaka ya Maji
Zanzibar {ZAWA} hivi karibuni.
Alitoa kauli hio
alipofanya ziara ya ghafla Makao Makuu ya Mamlaka ya Maji iliyopo Kinazini
jirani na Msikiti Mabuluu Mjini Zanzibar Mheshimiwa Hemed alisema
amefikia uamuzi wa kutoa agizo hilo ili Serikali Kuu ipate kujiridhisha kama
hakuna dalili yoyote ya harufu ya rushwa kwenye manunuzi hayo.
Mh. Hemed alisema
Serikali kamwe haitovumilia kuona Mamlaka ya Maji Zanzibar {ZAWA} ambayo
ni Taasisi muhimu inayogusa moja kwa moja maisha ya viumbe inazunguukwa na
uzembe unaoweza kuleta athari pamoja na kupungua kwa Mapato ya Serikali.
Aliutaka Uongozi wa
Mamlaka ya Maji kujisafisha kwa kuondoa hitilafu za migogoro ya Uongozi ndani
ya kipindi cha Mwezi Mmoja vyenginevyo Serikali italazimika kusafisha
safu hiyo ya Uongozi kwa maslahi ya Umma.
Mheshimiwa Hemed
alisema Wahandisi wa Taasisi hiyo wanapaswa kurekebisha miundombinu sambamba na
kuweka utaratibu utakaoharakisha Watendaji wa Mamlaka hiyo kuwajibika ipasavyo
ili kuwapa fursa Wananchi kupata huduma za maji safi na salama muda wote.
Alisema wazi kwamba
hali ya uwajibikaji kwa Watendaji wa Mamlaka ya Maji haiko vizuri kutokana na
tabia ya muhali inayochukuwa nafasi kubwa na matokeo yake hata makusanyo ya
Mapato yatokanayo na Huduma za Maji hayafikii lengo halisi lililokusudiwa.
Alieleza kuwa
suala hilo ni vyema likaenda sambamba kwa Watendaji hao kuhakikisha kwamba
Wananchi na Taasisi zote zinazotumia huduma hiyo zinawajibika kulipa huduma
hiyo ili Taasisi hiyo iweze kujiendesha badala ya kuendelea kupeleka maombi ya
kupatiwa fedha Serikali Kuu.
Mapema Mkurugenzi Mkuu
wa Mamlaka ya Maji Zanzibar {ZAWA} Nd. Mussa Ramadhan Haji alisema hali ya
upatikanaji wa huduma za maji safi na salama ndani ya Visiwa vya Unguja na
Pemba kwa sasa imefikia asilimia 80% hadi 85% kutegemea matumizi
yaliyopo.
Nd. Mussa alisema
wakati mwengine hali hiyo hushuka hadi asilimia 75% kutokana na baadhi ya
Visima kukumbwa na hitilafu za Umeme lakini pia baadhi ya mashine za kusukumia
Maji huharibika kutokana na kutumika kwa muda mrefu hasa katika baadhi ya
maeneo yasiyo na Matangi ya kuhifadhia Maji.
Hata hivyo Mkurugenzi
Mkuu huyo wa Mamlaka ya Maji Zanzibar alibainisha kwamba katika kukabiliana na
changamoto zinazotokana na huduma za usambazaji Maji Wataalamu wake wameanza
kufanya Utafiti wakianzia eneo la Nungwi Mkoa wa Kaskazini Unguja ili kubaini
kasoro zinazochangia uwepo wa changamoto hizo.
Nao kwa upande wao
Wakurugenzi wa vitengo mbali mbali vya Mamlaka hiyo walimueleza Makamu wa Pili
wa Rais wa Zanzibar kwamba muitiko wa Wananchi kuendelea kulipa huduma za Maji
ni mdogo wakitoa sababu za kutokupata huduma hiyo kwa uhakika.
Walisema hivi sasa
wapo katika utaratibu wa kujiandaa kufunga Mita kwa watumiaji wote wa Huduma
hiyo mpango ambao utatoa uhalisia wa upatikanaji wa maji kwa wateja licha ya
kwamba wapo baadhi yao hulalamikia ukosefu wa huduma hiyo wakati majumbani mwao
yamejaa.
0 Comments